Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga, Polisi mechi ya mabao ASFC

Yanga X Polisi Yanga, Polisi mechi ya mabao ASFC

Tue, 20 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Raundi ya 32 bora ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) inaendelea leo kwa michezo minne kupigwa ambapo macho na masikio yatakuwa Uwanja wa Azam Complex itakapopigwa mechi kati ya Yanga na Polisi Tanzania kuanzia saa 12:00 jioni.

Kitakwimu na timu zinavyoonekana hii ni mechi ya mabao. Katika Championship, Polisi Tanzania imekuwa dhaifu kiulinzi kwani katika michezo 22 imeruhusu mabao 23 ikiwa ni wastani wa bao moja katika kila mechi tofauti na Yanga ambayo imefunga 39 na kuruhusu manane kwenye michezo 16.

Yanga ambao ndio mabingwa watetezi wanaingia wakiwa na kumbukumbu nzuri ya kushinda kwa mabao 3-0, mechi iliyopita na KMC huku kwa upande wa Polisi ikitoka kuchapwa 2-0 na Biashara United wiki iliyopita.

Mchezo huo huenda ukawa na mabadiliko kadhaa ya wachezaji kwa Yanga kutokana na mechi ijayo ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya CR Belouizdad kutoka Algeria itakayopigwa Jumamosi, Uwanja wa Mkapa.

Timu hiyo inayolewa na Kocha Miguel Gamondi iko kundi ‘D’ la Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa nafasi ya tatu na pointi tano, hivyo ushindi pekee mbele ya Belouizdad utaweka matumaini hai ya kusonga robo fainali ya mashindano hayo.

Umuhimu wa mchezo huo huenda ukamfanya Gamondi kupumzisha baadhi ya wachezaji wa kikosi cha kwanza wanaocheza mara kwa mara ili kuwapa mapumziko yatakayowaweka fiti katika hali ya kiushindani kabla ya kukutana na Waalgeria.

Polisi Tanzania haina cha kupoteza zaidi tofauti na wapinzani wao kwani hakuna inachogombea hivyo itajitoa kwa asilimia 100 kujaribu bahati yao ingawa hata katika Ligi ya Championship inayoshiriki mwenendo wake sio mzuri sana.

Yanga ambao ni mabingwa wa michuano hiyo mara saba tangu ilipoanzishwa 1967 ikifahamika (FAT) na kubadilishwa jina hilo 2015 na kuitwa ASFC, iliitoa Hausung FC ya Njombe kwa kuichapa mabao 5-1 kwenye hatua iliyopita ya 64 bora.

Katika mchezo huo ambao ulipigwa Uwanja wa Azam Complex, shujaa wa Yanga alikuwa ni mshambuliaji Clement Mzize aliyefunga mabao matatu ‘hat-trick’ akiwa ni mchezaji wa sita kufunga hivyo tangu michuano ilipoanza msimu huu.

Kwa upande wa Polisi ilifika hatua hiyo baada ya kuiondosha Nyumbu FC ya mkoani Pwani inayoshiriki Ligi Daraja la Pili kwa mabao 2-1 huku nyota inayemtegemea zaidi ni Fred Mwamakula mwenye mabao matano Ligi ya Championship.

Katika Ligi ya Championship, Polisi imekuwa na safu mbovu ya ulinzi kwani michezo 22 iliyocheza imeruhusu mabao 23 ikiwa ni wastani wa bao katika kila mechi tofauti na Yanga iliyofunga 39 na kuruhusu manane kwenye michezo 16.

Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alikaririwa na gazeti hili akisema kila mchezo ulio mbele ni muhimu kwa ajili ya kupata matokeo chanya huku akiwataka wachezaji wa kikosi hicho kutobweteka bali wafanye kile walichoifanyia KMC, huku Kocha Mkuu wa Polisi Tanzania, John Tamba akisema licha ya ubora wa wapinzani wao, ila wamekuja kuonyesha ushindani.

Michezo mingine ya ASFC leo ni Mashujaa itakayoikaribisha Mkwajuni huku KMC ikicheza na Gunners ya Dodoma wakati Kagera Sugar itaikaribisha Pamba Jiji.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: