VINARA wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara Yanga leo wanashuka dimbani kuwakabili Mbeya City katika mchezo wa mzunguko wa pili utakaochezwa ugenini kwenye dimba la Sokoine.
Mara ya mwisho timu hizo kukutana katika mzunguko wa kwanza, Yanga ilipata ushindi wa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa huku Mbeya City ikionesha mchezo mzuri na wenye ushindani wa hali ya juu.
Kiufundi unaweza kusema Yanga iko vizuri kutokana na takwimu zake ikiwa imecheza michezo 18 na kati ya hiyo imeshinda 13 na sare tano ikiongoza kwa pointi 44.
Yanga inajivunia kuwa na safu bora ya ulinzi iliyofungwa mabao saba tu huku pia, safu ya ushambuliaji ikiwa sio mbaya sana imefunga mabao 29, ndio timu ya pili kwa kufunga mabao mengi baada ya watani zao wa jadi Simba wenye mabao 41.
Mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu watamkosa nyota wao Saido Ntibazonkiza anayesumbuliwa na majeraha lakini bado ina kikosi kipana ikiwa imefanya maboresho katika safu ya ushambuliaji na ulinzi kwa kuwaongeza Fiston Abdulrazak na Dickson Job.
Tofauti na Mbeya City ambayo inashika nafasi ya pili kutoka mwisho katika michezo 18 iliyocheza imeshinda miwili, sare nane na kupoteza michezo nane ikivuna pointi 14 tu.
Mbeya City udhaifu wake katika mzunguko wa kwanza ulionekana upo kwenye safu ya ulinzi baada ya kuruhusu kufungwa mabao 20 lakini pia, hata ushambuliaji huwa wanatengeneza nafasi wanakosa ufanisi kwani wamefunga mabao saba pekee.
Pengine baada ya usajili wa dirisha dogo watakuja kivingine na kuwashangaza wanaowabeza.
Mchezo huo unaweza kuwa mgumu kwasababu Yanga inataka pointi tatu ili kusalia juu bila presha kutokana kwa watani zao wanaowakaribia na kingine kujiweka karibu na taji ambalo wamelidhamiria kulichukua msimu huu baada ya kulikosa kwa misimu mitatu mfululizo.
Kwa Mbeya City inataka kujinasua kutoka nafasi za chini na kupanda juu hivyo, ikiwa mbele ya mashabiki itataka kuonesha mchezo mzuri kupata matokeo.
Mchezo mwingine utakaochezwa leo ni Mwadui dhidi ya Biashara United kwenye Uwanja wa Mwadui Complex. Ni mchezo mgumu kwa mwenyeji aliyeko nafasi ya tatu kutoka mwisho anahitaji matokeo kujiondoa huko.