Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga, Mbeya City moto utawaka

Yanga Afrika Leo Yanga, Mbeya City moto utawaka

Sat, 26 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Mashabiki wa Yanga wanatambia rekodi yao ya kutopoteza mchezo katika mechi 48 mfululizo za Ligi Kuu na ukiwagusa tu wanakutishia kwa jambo hilo, lakini sasa wanakwenda kukutana uso kwa uso na moja ya timu ambayo haijawahi kuachia pointi tatu kwao ndani ya rekodi yao hiyo.

Pale kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa mapema tu saa 12:15 jioni vinara wa ligi Yanga wataikaribisha Mbeya City ambayo inaungana na Simba kuwa timu pekee ambazo hazijawahi kuachia pointi tatu mbele ya Yanga kuanzia msimu uliopita.

Msimu uliopita Yanga kila ilipokutana na City walijikuta wakigawana pointi moja-moja katika kila mchezo kama ilivyokuwa kwa wekundu Simba na leo watakutana tena katika mchezo wa kwanza msimu huu.

Yanga iko katika kiwango bora ikisaka kuboresha rekodi yake ya kutopoteza mchezo katika mechi 48 mfululizo za ligi zilizopita huku kwa msimu huu Yanga imecheza mechi 11 za ligi imeshinda tisa na kutoka sare mara mbili tu -- inakutana na City ambayo inatoka kuivimbia Simba katika sare ya bao 1-1 kule kwao jijini Mbeya.

Kocha Nasreddine Nabi anajua ubora wa City ya kocha Mganda Abdallah Mubiru ambaye ameirudisha timu hiyo kuanza kuwa timu ngumu kufungika ingawa msimu huu ilishapoteza mechi mbili msimu huu ikiwa katika nafasi ya tano kwenye msimamo.

Yanga itamkosa kiungo wake fundi Feisal Salum ambaye anatumikia kadi za njano lakini habari njema kwao ni kurejea kwa Stephane Aziz KI aliyemaliza adhabu yake ya kufungiwa mechi tatu na tangu juzi alikuwa mazoezini na wenzake.

Sambamba na huyo wengine kiungo Yannick Bangala aliyekuwa akitumikia adhabu ya kadi za njano na kipa wao namba moja Djigui Diarra aliyeenda kuitumikia timu ya taifa ya Mali, nao wamerejea baada ya kukosa mechi iliyopita na wanarejea kundini na winga Bernard Morrison.

City watashuka kwenye Uwanja wa Mkapa wakitegemea kasi ya mshambuliaji wao Sixtus Sabilo anayeshika nafasi ya pili katika ufungaji akiwa na mabao 7 akizidiwa bao moja na kinara wa mabao, mshambuliaji wa Yanga Fiston Mayele.

Mbali na Sabilo Yanga wanatakiwa kuwa makini na kiungo Awadh Juma na mshambuliaji wao wa zamani Tariq Seif ambaye aliwatibulia Simba katikati ya wiki hii.

Akizungumzia mchezo huo, kocha msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze alisema wanajua wanaenda kukutana na Mbeya City ambao ni mshindani mgumu lakini wamejiandaa vizuri kuhakikisha wanapata pointi kwenye mchezo huo.

Kaze alisema Mbeya City ina matokeo mazuri ambayo yanawabeba wakiingia kwenye mchezo huo ambao utakuwa mgumu kutokana na rekodi ya timu hizo mbili zinapokutana.

Akizungumzia upande wa kutopoteza mchezo katika mechi 48, alisema ni kutokana na kutodharau kila timu ambayo huwa wanakutana nayo.

Upande wa kocha msaidizi wa Mbeya City, Anthony Mwamlima alisema licha ya kuwasili Dar es Salaam kwa basi juzi Alhamisi, jana Ijumaa walifanya mazoezi ya mwisho kwa ajili ya mchezo huo kuhakikisha wanapata pointi.

“Tunajua wamefanya maandalizi makubwa na sisi tumeandaa kikosi chetu vizuri kupata matokeo mazuri na kubwa zaidi ni wachezaji wetu waamke vizuri,” alisema Mwamlima.

Chanzo: Mwanaspoti