Yanga wanashuka dimbani kuwakabili Marumo Gallants ya Afrika Kusini katika mchezo wa marudiano wa nusu fainali Kombe la Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) Uwanja wa Royal Bafokeng leo.
Mchezo wa kwanza uliochezwa Benjamin Mkapa wiki iliyopita, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 yaliyofungwa kipindi cha pili na Stephane Aziz Ki na Bernard Morison.
Yanga itahitaji sare au ushindi wa aina yoyote kuingia hatua ya fainali kwa mara ya kwanza kwenye historia ya klabu hiyo kwenye michuano ngazi ya klabu Afrika.
Ingawa wapinzani wao Marumo Gallants wana rekodi nzuri kwenye uwanja wake wa nyumbani kwani hawajawahi kufungwa au kutoka sare katika michuano ya kimataifa msimu huu.
Katika dimba la Royal Bafokeng kwenye Kombe la Shirikisho, Marumo Gallants wameshinda bao 1-0 dhidi ya Pyramids ya Misri, mabao 3-2 dhidi ya Saint Eloi Lupopo ya DRC, 4-1 dhidi ya Al Akhdar ya Libya na kisha kuwafunga USM Alger ya Algeria mabao 2-0.
Huku Yanga wakiwa na rekodi nzuri katika michezo ya ugenini kwenye michuano hiyo kwani ukiondoa kufungwa mabao 2-0 na Monastri jijini Tunis na sare ya bao 1-1 na Real Bamako ya Mali, Yanga wameshinda mechi zao zote za ugenini.
“Kila mchezaji afanye jukumu lake kwa kufuata maelekezo tunayowapa kuanzia mazoezini. Naamini tumefanya maandalizi mazuri na jukumu lao kwenda kuipa timu matokeo mazuri,” alisema Kocha Nasriddine Nabi akizungumzia mchezo huo.
Meneja Mkuu wa timu ya Marumo Gallants, Rufus Matsena alisema waliwapa Yanga mabao mawili kwa ajili ya heshima ya Hayati Mwalimu Julius Nyerere hivyo Yanga watalazimika kuachia mabao matatu (3-0) kwa ajili ya kumuenzi Hayati Nelson Mandela.