Klabu ya Pamba Jiji jana imeendesha harambee maalum ya kukusanya fedha za kuiwezesha kupanda daraja kwenda Ligi Kuu msimu huu, ambapo jumla ya Sh177.3 milioni zimechangwa na kuahidiwa katika hafla hiyo pamoja na kuuza jezi zaidi ya nakala 200 ambazo kila jezi moja inayouzwa Sh30,000 klabu hiyo hupata Sh8,000.
Hafla hiyo imefanyika Februari 11, 2024 kuanzia saa 12 jioni katika ukumbi wa hoteli ya Mwanza ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo, Amos Makalla na kushirikisha makundi mbalimbali ikiwemo viongozi wa taasisi za Serikali, wafanyabiashara, wadau wa michezo na viongozi wa wilaya na halmashauri za mkoa huo.
Katika harambee hiyo, mfanyabiashara maarufu jijini Mwanza na mjumbe wa bodi ya Klabu ya Pamba, Christopher Gachuma kwa kushirikiana na wenzake wamechangia Sh35 milioni, huku Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda akichangia Sh10 milioni.
Klabu ya Yanga kupitia kwa Rais wake, Hersi Said imechangia Sh2 milioni, huku Mjumbe wa kamati tendaji ya klabu hiyo, Yanga Makaga naye akichangia Sh2 milioni, huku mashabiki wa klabu ya Simba wakiongozwa na Aggy Simba wakichangia Sh200,000.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla, amesema mbali na Makonda viongozi mbalimbali wa Serikali wamechangia harambee hiyo akiwemo Naibu Wazuri Mkuu, Dotto Biteko aliyetoa Sh10 milioni, Wazuri wa Ulinzi na Jeshi la Wananchi, Stagomena Tax Sh5 milioni na Mbunge wa Nyamagana, Stanslaus Mabula akichangia Sh5 milioni, ambapo amewatoa wasiwasi akisema fedha hizo zitakuwa salama na zitatumika kwa matumizi yaliyokusudiwa.
Amesema lengo ni kuhakikisha kwamba katika mechi tisa zilizobaki timu hiyo inatangaza mapema kupanda daraja ambapo lengo ni kuhakikisha wachezaji wanaishi katika mazingira mazuri, wanasafiri vizuri na kupata motisha kubwa itakayowasaidia kufanya vizuri kwenye mechi zao na kutimiza lengo.
"Niwashukuru sana kwa kuja na kushiriki katika harambee yetu kwakweli mmetutia moyo na itaandikwa katika ukumbi huu kwamba Pamba ilipanda Ligi Kuu, chochote mlichotoa kina thamani sana Kila aliyetoa sisi tunamuona ni mtu muhimu katika safari ya mafanikio, siku nyingine tukiwaita tutakuja kutoa hesabu ya kile tulichokitoa leo. hatujakaa bure tumepata mafanikio, jumla ya fedha zote ambazo zimepatikana ni Sh177.3 milioni,"
"Katika mchanganuo ufuatao fedha taslimu Sh18.9 milioni, miamala iliyoko benki Sh48 milioni na ahadi Sh109 milioni, kwahiyo tuna nyenzo tuachieni kazi,Sh177 milioni tunazo tunawaambia pisheni njia tunakuja, wachezaji wetu wafurahie, waishi katika mazingira mazuri na katika mechi tisa zilizobaki tufanye vizuri na kwenda Ligi Kuu,"
"Utaratibu tulioweka watu wameshaanza kuweka hela, ndugu zangu nataka niwahakikishie hela zitakazochangwa zitakuwa salama, haiwezi kutoka bila mimi kuona, kwahiyo hela itakuwa salama na zitatumika kwa kile kilichokusudiwa," amesema Makalla.