Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga Mabingwa ni raha tu Dar

Mshabiki Yanga Parade Yanga Mabingwa ni raha tu Dar

Mon, 27 May 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Dar es Salaam ni kijani na njano, kwa sasa hakuna rangi ambayo imetawala zaidi ya rangi hizo baada ya Yanga kukabidhiwa kombe lao la ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara juzi.

Ubingwa huo wa Yanga msimu huu unakuwa wa 30 katika rekodi ya timu hiyo na kuzidi kuwaacha mbali watani zao Simba.

Yanga walikabidhiwa kombe lao juzi baada ya mchezo wao dhidi ya Tabora United uliochezewa Uwanja wa Benjamin Mkapa na kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-0.

Yanga waliendeleza sherehe zao jana kuanzia saa 4:00 asubuhi kwa mashabiki wao kunywa supu katika Uwanja wa Benjamin Mkapa ambapo kulianzia shamra shamra za kusherehekea ubingwa.

Baada ya kunywa supu wachezaji na baadhi ya viongozi walipanda kwenye basi maalum ambalo lilibeba kombe lao la ubingwa huku wakifunga barabara kwa kulitembeza kombe hilo kutoka uwanjani mpaka makao makuu ya klabu hiyo, Jangwani.

Walipita Keko, Tazara, Buguruni, Karume. Mitaa ya Msimbazi na safari kuishia makao makuu ya klabu hiyo huku maelfu ya mashabiki walijitokeza kwenye paredi hiyo.

Yanga walitumia saa tatu na nusu kufanya paredi kutoka Benjamin Mkapa hadi makao makuu ya klabu hiyo na kufika saa 7: 30 mchana.

Walipowasili makao makuu ya klabu hiyo, Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe alitambulisha benchi la ufundi linaloongozwa na Kocha Mkuu, Miguel Gamondi na viongozi wa kamati ya utendaji inayoongozwa na Rais, Hersi Said.

Pia walitambulishwa wachezaji wote ambao wamefanikisha kutetea taji lao kwa mara ya tatu mfululizo na kukata tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.

Nahodha Msaidizi wa timu hiyo, Dickson Job, aliwashukuru wanachama na mashabiki wa Yanga kwa kuwa nao pamoja kwa msimu mzima na kuendelea kuwasapoti katika michezo iliyosalia.

“Bado hatujamaliza na tunakibarua kingine mbele yetu, tuna deni lingine na tunatakiwa kwenda kulilipa visiwani Zanzibar katika fainali ya kombe la Shirikisho la CRBD Bank na kurejea Dar es Salaam na kombe," alisema Job.

Aidha, Rais wa timu hiyo, Hersi alisema wachezaji, benchi la ufundi na uongozi wamefanya kazi kubwa ya kuchangia ubingwa wa 30 na kutwaa mara tatu mfululizo.

“Kila mmoja anatambua kuwa Juni 2, mwaka huu kuna kibarua kigumu sana mbele yetu na tunaenda kupambana kuhakikisha tunafanikiwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho na kuja kulitambulisha kwa mara nyingi hapa klabuni.

Niwaahidi mashabiki na wanachama tunaenda kujenga timu yetu bora kuliko msimu huu kwa kusajili nyota wengine wenye uwezo na hatutaacha mchezaji yeyote yule ambaye atakuwa kwenye mipango yetu,” alisema Hersi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live