Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga: Liwake jua, inyeshe mvua hawatoki

Yanga Mjinange Sehemu ya Wachezaji wa Yanga

Thu, 28 Apr 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Wakati Simba ikiingia kambini jana kwa maandalizi ya mechi na watani zao, Yanga nao wameingia kambini ingawa wao juzi walianza na mazoezi ya gym.

Hata hivyo, kuelekea mechi hiyo ya Ligi Kuu yenye ushindani na upinzani mkubwa itakayochezwa Jumamosi Uwanja wa Mkapa, mabosi wa Yanga jana usiku walishiriki chakula cha pamoja na wachezaji wao huko kambini kwao baada ya kuingia rasmi kwenye kambi hiyo jana.

Mabosi hao wakiongozwa na mdhamini wao - GSM walikula pamoja futari huku wakipanga mipango yao ya ushindi ya mechi hiyo ambayo wao ndiyo wenyeji.

Miongoni mwa mipango inayodaiwa kujadiliwa kwenye chakula hicho cha usiku ni namna ya kumpiga Mnyama na kuendelea kukaa kileleni mwa msimamo kwani hadi sasa wanaongoza kwa pointi 54 wakiwa wamecheza mechi 20 mbele mechi moja ya watani wao ambao wameondolewa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya robo fainali wenye alama 41.

Mbali na mkakati huo, pia kutokana na ukubwa na umuhimu wa mechi hiyo na kutaka kutoharibu rekodi yao ya kutofungwa hadi sasa msimu huu imeelezwa watajadili namna wachezaji watapewa motisha endapo wataifunga Simba.

“Mipango yote itajadiliwa leo (jana usiku) wakati wa Ifta huko kambini, watakuwepo mabosi wote pamoja na wadhamini wetu, hii ni mechi muhimu na tunahitaji ushindi hivyo ni lazima tuzungumze na wachezaji kuwaeleza umuhimu wa mechi hiyo,” alisema kiongozi huyo na kuongeza:

“Motisha lazima itakuwepo na ni jambo ambalo hufanywa kila mechi lakini hii inakuwa tofauti kutokana na ukubwa wake, hivyo kila kitu kitakwenda sawa.”

Alipotafutwa Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli kuelezea juu ya kambi yao alisema kikosi chao kimeanza mazoezi kuelekea mechi hiyo ambayo wao ndiyo wenyeji na wanatarajia ushindi.

“Jana Jumatatu (juzi) wachezaji walifanya mazoezi ya gmy, lakini leo (jana) wameingia rasmi kambini, kinachofuata ni programu za kocha kukiandaa kikosi chake kuelekea mchezo huo, ndiyo maana aliwapumzisha siku chache baada ya mechi na Namungo FC,” alisema.

Hii kwa Yanga itakuwa mechi ya mzunguko wa 21 baada ya kuifunga Namungo bao 2-1 katika mchezo wa mwisho wa ligi hiyo wakati Simba itakuwa mechi yao ya raundi ya 20.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz