Baada ya kupata ushindi wa mabao 3-1 kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Jumapili, Yanga leo inatupa karata nyingine kwenye Ligi Kuu Tanzanjia Bara ikivaa KMC FC.
Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa ligi hiyo watajitupa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam kuanzia majira ya saa 1:OO usiku wakiwania pointi tatu.
Yanga ambao ni vinara wa ligi hiyo wana pointi 59, huku KMC ipo katika nafasi ya 12 ikiwa imecheza mechi 22 na kujikusanyia alama 23.
Yanga wanahitaji kupata matokeo mazuri na alama tatu ili kuendelea kuweka rekodi yao ya kushinda baada ya kushinda mechi 21 huku ikipoteza moja katika michezo 22 ambayo wamecheza msimu huu.
Katika mchezo wa leo KMC watakuwa nyumbani na wataendelea kumkosa mchezaji wao, Hans Masoud.
Kocha Msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze alisema maandalizi yanaendelea vizuri licha ya kupata muda mfupi wa maandalizi kwani kikubwa ni wachezaji kuwaandaa kisaikolojia.
Alisema walichokifanya ni kuwaandaa wachezaji wao kiakili na kusahau furaha ya matokeo mazuri ya mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya TP Mazembe.
"Tuko vizuri kiufundi, kisaikolojia na kimbinu kwa sababu tunahitaji matokeo mazuri katika mchezo wetu wa kutafuta pointi tatu dhidi ya KMC,” alisema Kaze.
Aliongeza: “Wachezaji wote wako fiti kasoro wale ambao hatukuwa nao tangu awali kutokana na Morrison na Mshery Abdultwalib ambao ni majeruhi."
Kwa upande wake Kocha Msaidizi wa KMC, Ahmad Ally, alisema wanakwenda kucheza na timu bora na nzuri, hivyo wataingia kwa tahadhari kubwa kwani wanahitaji pointi.
Alisema mchezo huo utakuwa mgumu na bora kwa sababu kila mmoja wao anahitaji matokeo na wamefanyia kazi kila idara ikiwamo safu ya ulinzi, ushambuliaji na ulinzi.
“Mpango mkakati wetu ni kupambana kuyafuta matokeo ili kujiweka katika mazingira mazuri na kuwa kwenye nafasi mzuri katika msimamo na kujiondoa katika nafasi ya chini,” alisema Ally.
“Kufungwa na Yanga haitakuwa habari, bali sisi kuwafunga Yanga ni habari kubwa, tunaenda kucheza kwa kuwaheshimu kiufundi.”
Alisema mchezo wa leo utakuwa wa kimbinu sana huku wachezaji wao wanahitaji kutuliza akili ili kufikia mipango mikakati yao.
Mwakilishi wa wachezaji wa KMC, Awesu Awesu, alisema morali yao iko juu kwa ajili ya mchezo wao wa leo ili kupambana kutafuta matokeo mazuri dhidi ya Yanga.
“Tumejiandaa vizuri na tuko tayari kwa ajili ya kutafuta matokeo chanya dhidi ya Yanga, itakuwa mechi ya ushindani mkubwa na kazi kubwa kwetu ni kuona timu inapata matokeo mazuri,” alisema Awesu.