Uongozi wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Young Africans umesema kuwa baada ya kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu sasa hawatachomoka mpaka wanahakikisha kuwa wanaubeba ubingwa wa msimu huu 2023/24.
Young Africans wamepata nafasi ya kuendelea kuongoza ligi baada ya kufanikisha kuibuka na ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Simba SC katika mchezo uliofanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar.
Baada ya ushindi huo umewafanya Young Africans kufikisha alama 21 ambazo kama Simba SC akifanikisha kushinda mchezo wake wa kiporo utawafanya walingane alama huku Young Africans wakiwa na faida ya mabao 8 tofauti na Simba SC.
Ofisa Habari wa Young Africans, Ally Kamwe amesema kuwa watahakikisha kuwa wanaendelea kupata matokeo ya ushindi ili kuendelea kubakia kileleni baada ya kujihakikishia nafasi hiyo.
“Unajua mara ya kwanza tulikuwa tupo nyuma ya alama tatu dhidi ya wapinzani wetu lakini baada ya kuwafunga sasa tunauhakika wa kuendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi kwa kuwa tumelingana nao pointi lakini tunayo mabao mengi yakutosha.
“Hivyo kwa sasa wapinzani wetu ndio wasahau tena maana hakuna mzaha na mpinzani yoyote ambaye tutakutana naye, tutahakikisha kuwa tunashinda ili tusishuke juu ya msimamo mpaka tunaubeba ubingwa wa ligi kuu,”amesema Ally Kamwe.