Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga Kambi sasa Ulaya

Yangasc Bingwa 30 Yanga Kambi sasa Ulaya

Sun, 16 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Imepita misimu mitatu mfululizo Yanga ikijichimbia kambi ya maandalizi ya mpya mpya (pre season) ikiwa Avic Town, Kigamboni jijini Dar es Salaam, lakini safari hii huenda mambo yakabadilika baada ya klabu hiyo kupata mwaliko wa kwenda Ulaya kuweka kambi kujiandaa na msimu mpya.

Klabu hiyo ambayo leo usiku inazindua kitabu kiitwacho Klabu Yetu, Historia Yetu, imepata mwaliko mzito kutoka klabu ya CSKA Moscow ya Urusi kupeleka wachezaji kwa ajili ya kambi ya maandalizi ya msimu ujao.

Klabu hizo ziliingia makubaliano ya ushirikiano utakaoifanya Yanga kupeleka wachezaji wa timu ya vijana wenye vipaji.

Hivyo kwa kuanzia ni hapa katika kipindi cha pre-season na Yanga itaweka kambi huko na tayari wameshaanza kutengeneza mchakato wa safari hiyo kwa kuwaombea visa wachezaji.

Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Yanga kwenda huko, kwani kabla ya kuamua kujichimbia Avic, klabu hiyo ilikuwa na utamaduni wa kuipeleka timu Uturuki na mara moja ilienda Morocco ambako hata hivyo haikuwa kambi nzuri kwa afya ya timu hiyo.

Hata hivyo, kwa upande wa Kocha Miguel Gamondi hii itakuwa ni mara ya kwanza kutoka na kikosi hicho nje ya Tanzania kwa ajili ya mapumziko na maandalizi ya msimu mpya, kwani msimu uliopita hakutoka na hata ilipokuwa chini ya Nasreddine Nabi pia tangu ilipozinguliwa Morocco mwaka juzi hakuitoka kabisa nje.

Ofisa wa Habari wa Yanga, Ali Kamwe aliweka wazi, msimu huu utakuwa tofauti, kwani hawatakuwa na maandalizi ya pre season Avic Town.

“Rais wetu alishaweka wazi katika mkutano mkuu wikiendi iliyopita, tuna mialiko sehemu tatu, Afrika Kusini tumealikwa na Kaizer Chiefs baada ya kuwaalika katika kilele cha Wiki ya Wananchi, Kenya tulipokea mwaliko wa Raila Odinga na Ulaya, hivyo ni wazi msimu huu tutakuwa nje ya nchi,” alisema Kamwe na kuongeza;

“Wakati ukifika tutaweka wazi mahali kambi yetu inapoandaliwa na itakuwa Ulaya hivyo kila kitu tutakisema ila bado maandalizi yanaendelea.”

Katika misimu yote ambayo Yanga haikuweka kambi nje ya nchi ilifanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho mara tatu mfululizo na Ngao ya Jamii mara mbili pamoja na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita na robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliomalizika.

Tayari dirisha la usajili kwa klabu za soka nchini kwa ajili ya msimu ujao limefunguliwa jana na linatarajiwa kufungwa Agosti 15, hivyo inaweza kuirahisishia Yanga kuondoka na majembe yote itakayowasajili kabla ya kurejea nchini kuzindua msimu na Tamasha la Mwananchi na mechi za Ngao ya Jamii mapema Agosti.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: