Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga, Kagera mahesabu tofauti leo

Yanga Vs Kagera Yanga, Kagera mahesabu tofauti leo

Tue, 11 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Achana na matokeo ya jana ya Ihefu dhidi ya Simba, leo Yanga itaikaribisha Kagera Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu utakaochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, saa 1:00 usiku.

Huu utakuwa mchezo muhimu kwa timu zote kwa kuwa Yanga wakipata ushindi watakuwa wanaukaribia ubingwa na Kagera wakishinda wataendelea kujiweka sehemu nzuri kwenye msimamo.

Yanga na Kagera Sugar zinapokutana timu hizi zimekuwa zikitoa mabao mengi iwe katika uwanja wa Mkapa au Kaitaba jambo ambalo linaonekana na leo linaweza kutokea. Kwenye mechi 10 zilizopita Yanga na Kagera zimetengeneza jumla ya mabao 27, huku Yanga ikifunga mabao 18 na Kagera Sugar 9.

Mechi hizo 10 ambazo Yanga imekutana na Kagera ugenini na nyumbani ni mechi nne tu ambazo timu moja imefunga bao pekee lakini kwenye mechi sita wamefungana. Yanga ikiwa nyumbani kwenye mechi tano imeshinda tatu, sare moja na kupoteza mchezo mmoja.

Msimu huu Kagera Sugar hadi sasa ipo nafasi ya saba ikiwa imefungwa mabao 25 na kufunga 22 ikiwa na pointi 32 huku Yanga yenyewe ikishika nafasi ya kwanza ikiwa na pointi 65, ikifungwa mabao 11 na kufungwa 45.

Yanga hadi sasa inaonyesha ni wazi kwenye eneo lake la ushambuliaji inafunga mabao huku mshambuliaji wao Fiston Mayele akiwa kinara wa kufunga kwenye Ligi akiwa na mabao 15 na Aziz Ki matano sawa na mshambuliaji wa Kagera Sugar, Anuary Jabir.

Upande wa Yanga wachezaji wote wapo vizuri kutokana na ripoti ya benchi la ufundi la timu hiyo huku upande wa Kagera Sugar yenyewe itamkosa Anuary Jabir ambaye ameenda nchini Ubelgiji kufanya majaribio kwenye timu ya KAA Gent.

Kukosekana kwa Jabir ni muendelezo wa Kagera kuwa kwenye wakati mgumu katika eneo la ushambuliaji kwani mshambuliaji Mbaraka Yusuph hajawa na wakati mzuri msimu huu. Akizungumzia mchezo huo, kocha msaidizi wa Yanga, Cedrick Kaze amesema wanatakiwa kuhakikisha wanapata pointi tatu kwenye mechi zilizosalia kwenye Ligi Kuu. Kaze alisema anajua mchezo utakuwa mgumu kutokana na ubora wa wapinzani wao lakini wanakiandaa kikosi chao kuwa sawa kiakili na utimamu ili wapate matokeo.

"Ratiba ni ngumu kwetu kwa hiyo lazima wachezaji wapate muda wa kupumzika, kutakuwa na mabadiliko kwenye kikosi lakini sio makubwa ya kufanya timu ikose uwiano mzuri;

"Tulicheza nao mchezo wa kwanza na ulikuwa mchezo mmoja mgumu, nakumbuka tulishinda 1-0, walipata penalti lakini walikosa kwa hiyo tunajua mechi itakuaje." Upande wa kocha msaidizi wa Kagera Sugar, Marwa Chamberi alisema wanajua mchezo utakuwa mgumu kwa sababu Yanga wana kitu wanakihitaji na wana ubora lakini na wao wanajipanga kuhakikisha wanafanya vizuri.

Chamberi alisema ukicheza na timu kubwa kila mmoja anakuwa anachukuliwa wanapoteza lakini hilo linawafanya wawe huru kucheza na kuonyesha mchezo wao kwa sababu wanahitaji pointi.

"Tunajua hii ni timu kubwa lakini haitusumbui, tupo hapa kupambana kuhakikisha tunapata pointi, watakuwa na wakati mzuri kwa sababu wapo nyumbani lakini tutapambana;

"Tutawakosa wachezaji watatu ambao ni Dickson na Yusuph (Mhilu) hawa wote ni majeruhi, Anuary atakosekana lakini yeye ameenda kufanya majaribio nje ya nchi." Wakati huo huo leo saa 10:00 jioni KMC itaikaribisha Kagera Sugar katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu Bara utakaochezwa katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Chanzo: Mwanaspoti