Uhondo wa Ligi Kuu Bara mwishoni mwa wiki hii uko sehemu mbili tu ambazo ni Morogoro leo na Dar es Salaam kesho.
Baada ya kuahirishwa kwa mechi ya Simba na Mtibwa Sugar iliyokuwa ichezwe kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro kesho Jumapili, wakazi wa Morogoro na mashabiki wa soka nchini wamebakiwa na burudani mbili za aina yake ambapo moja wataipata katika mechi baina ya KMC na Yanga itakayochezwa kwenye Uwanja huo uliopo mkoani hapo.
Wakati Yanga ikikwaana na KMC, katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni, Dar es Salaam, JKT Tanzania iliyotoka kupoteza mbele ya Simba itaikaribisha Namungo FC katika mechi itakayoanza saa 10:00 jioni.
Mwendelezo wa matokeo mazuri ambayo Yanga imekuwa nao na hamu ya kulipa kisasi iliyopo kwa KMC dhidi ya wapinzani wao hao leo, bila shaka ndio yanafanya mechi ya leo isubiriwe kwa hamu.
Yanga inaingia katika mechi hiyo ya leo ambayo itachezwa kuanzia saa 10:00 jioni, ikiwa na rekodi nzuri ya kutopoteza mechi 11 mfululizo za Ligi Kuu na tangu ilipopoteza dhidi ya Ihefu kwa mabao 2-1, Oktoba 4, mwaka jana, imeibuka na ushindi mara 10 na kutoka sare moja katika mechi 11 zilizofuata.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa Yanga, mwenyeji KMC inaingia kwenye mechi hiyo ikiwa haina mwenendo mzuri katika mechi za Ligi Kuu siku za hivi karibuni na kudhihirisha hilo, haijapata ushindi katika mechi tano mfululizo zilizopita ikipoteza moja na kutoka sare nne.
Mbali na kuhitaji ushindi ambao utairudisha kwenye mstari, KMC hapana shaka inatamani kupata pointi tatu leo ambao utakuwa kama kisasi cha kupoteza kwa kipigo cha mabao 5-0 kutoka kwa Yanga kwenye mechi ya mzunguko wa kwanza ambayo ilichezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Agosti 23, 2013.
Pointi za hesabu Ushindi wa Yanga leo utaifanya ifikishe pointi 43 na hivyo kuifanya izidi kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi huku ikiongeza presha kwa Simba na Azam ambazo zinaifuata kwa ukaribu katika mbio za ubingwa wa ligi hiyo msimu huu.
Lakini kama itapoteza, Yanga itajiweka katika wakati mgumu zaidi na inaweza kutoa mwanya wa kufikiwa au kukaribiwa na wapinzani wake hao kwa vile timu zote hizo mbili zilizo nyuma yake zina faida ya kuwa na mechi mkononi.
Kwa KMC yenyewe ushindi utaifanya ichupe hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi kwani itafikisha pointi 25 na hivyo kuweka hai matumaini yake ya kumaliza katika nafasi nne za juu zinazoweza kuipa nafasi ya ushiriki kwenye mashindano ya klabu Afrika msimu ujao.
Ikiwa itapoteza au kutoka sare, itaipa fursa Coastal Union kubakia katika nafasi hiyo ya nne lakini itajiweka katika hatari ya kushushwa zaidi na Singida Fountain Gate, Tanzania Prisons, Namungo na Dodoma Jiji ambazo zinaikaribia kipointi.
Nambazinaongea
KMC ni mnyonge wa Yanga na pengine mechi ya leo inaweza kuwa nafasi nzuri kwao kuukataa utumwa ilionao dhidi ya mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu au ikaendeleza ubabe ambao Yanga imekuwa nao dhidi yao kwenye Ligi.
Mechi tano zilizopita za Ligi Kuu baina yao, zilimalizika kwa ushindi upande wa Yanga pasipo uwepo wa droo au ushindi kwa KMC.
Kana kwamba haitoshi, katika mechi hizo tano zilizopita baina ya timu hizo, Yanga imefunga mabao 11 ikiwa ni wastani wa mabao 2-2 kwa mchezo wakati KMC yenyewe haijafunga bao lolote katika mechi hizo tano zilizopita.
Vikosi vya moto
Urejeo wa Djigui Diarra na Stephane Aziz Ki ambao walikuwa wakitumikia timu zao za taifa kwenye fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) zilizofanyika huko Ivory unalipa wigo mpana benchi la ufundi la Yanga katika upangaji wa kikosi cha kwanza katika mechi ya leo.
Nyota 11 wanaoweza kuanza kikosini Yanga leo ni Diarra, Yao Attohoula, Joyce Lomalisa, Ibrahim Bacca, Dickson Job, Khalid Aucho, Maxi Nzengeli, Mudathir Yahya, Clement Mzize, Pacome Zouzoua na Stephane Aziz Ki.
Kikosi cha KMC leo kinaweza kuundwa na Wilbol Maseke, Rodgers Gabriel, Hance Masoud, Juma Shemvuni, Twalibu Nuru, Issa Ndala, Ibrahim Elias, Awesu Awesu, Waziri Junior, Fredy Tangalo na George Makang’a.
Makocha hesabu moja Kocha wa KMC, Abdihamid Moalin alisema matarajio yao ni kupata ushindi katika mechi hiyo.
“Wachezaji wapo katika morali nzuri na wamefanya mazoezi mazuri wiki hii. Tunajua ni mchezo mgumu dhidi ya mabingwa wa Tanzania. Tunategemea mechi nzuri ya soka kwa sababu timu zote zinapenda kucheza hivyo timu ambayo itatumia nafasi itakuwa na nafasi nzuri ya kushinda.
“Lengo letu ni kutorudia makosa ya mechi iliyopita. Ninaamini timu yangu na wachezaji wangu wako tayari kwenda kucheza mechi nzuri. Tumecheza Jamhuri katika mechi ya kirafiki hivyo tumeuzoea uwanja na kitu kikubwa ninachokifurahia kwa kundi hili la wachezaji ni kwamba hawachagui wapi pa kucheza,” alisema Moalin.
Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alisema kuwa wanachohitaji ni muendelezo wa kufanya vizuri kwa kupata ushindi dhidi ya KMC leo.
“Wiki hii kidogo tumepata muda wa kujiandaa kwani kabla ya hapo tulicheza mechi nyingi ndani ya muda mfupi. Tumepata nafasi ya wachezaji kupona na Aziz Ki amerejea hivyo tuna kikosi kamili. Tutajaribu kuanza mzunguko wa pili kwa kufanya vizuri na tumekuja hapa tukitaka pointi tatu.
“KMC ni timu nzuri, tunaiheshimu na napenda jinsi inavyocheza. Ni timu ya kiungwana. Hii ni mechi nzuri na nategemea itakuwa ngumu kwetu,” alisema Gamondi.