Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said amesema kuwa hawana jambo dogo linapokuja suala la kuboresha kikosi hicho kwa kuhakikisha kila wanayemhitaji anabaki.
Timu ya Yanga imekamilisha msimu wa 2022/23 ikiwa na mafanikio ya kutwaa taji la ligi, Ngao ya Jamii, Azam Sports Federation na imecheza fainali Kombe la Shirikisho Afrika.
Kuna wachezaji ambao wanatajwa kutaka kuondoka ndani ya Yanga ikiwa ni pamoja na Yannick Bangala, Djuma Shaban, Fiston Mayele licha ya kuwa na mkataba wa mwaka mmoja.
Sababu kubwa za nyota hao kutaka kusepa ndani ya Yanga ni kusaka changamoto mpya na kuendeleza malengo yao ya kuishi ndoto zao.
Injinia amesema kuwa hakuna mchezaji ambaye wakimhitaji ataondoka ila lazima makubaliano yawepo kati ya mchezaji na uongozi ikishindikana hapo watafanya maamuzi mengine.
“Ikiwa kuna mchezaji amefanya vizuri na anataka kuondoka hapo ni lazima tuzungumze naye kwani ambacho tunataka ni kuwa kwenye ubora uleule na kuendelea kuwaleta wengine bora.
“Kama kutakuwa na ofa kutoka timu nyingine hapo tutazungumza na mchezaji kisha kufanya makubaliano nasi tutakuwa na kazi ya kumtafuta mchezaji mwingine ambaye atakuwa ni mbadala wake,” amesema Hersi.