Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga, Geita shoo ya kisasi

Yanga Tizi Geita Yanga, Geita shoo ya kisasi

Sat, 8 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Yanga inarejea michuano ya nyumbani baada ya kuweka rekodi mpya kimataifa. Saa 2 usiku wa leo watavaana na Geita Gold katika mechi ya kisasi ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC) kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Ni mechi ya kisasi kwa vile ni wiki chache zilizopita kwa timu hizo kukutana kwenye pambano la Ligi Kuu Bara na Yanga kuishindilia Geita mabao 3-1, kitu ambacho wageni hao wametamba hawataki kurudia tena makosa wakitaka kwenda nusu fainali ya michuano hiyo.

Hii ni mara ya pili katika misimu miwili mfululizo kwa Yanga na Geita kukutana robo fainali ya ASFC baada ya ile ya April 10, mwaka jana iliyokuwa na mvuto wa aina yake dakika 90 zikiisha kwa sare ya 1-1 na zikaenda kwenye mikwaju ya penalti na Yanga kushinda 7-6 na kwenda nusu.

Katika mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Geita ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 88 kupitia kwa Offen Chikola, lakini dakika za nyongeza Amos Kadikilo aligusa mpira katika harakati za kuokoa na Yanga kupata penalti iliyofungwa na Djuma Shabani ndipo zikapigiana penalti na Geita imetamba wanataka kujiuliza walipotezaje mchezo ule!

Hata hivyo, ukiachana na robo fainali hiyo ya mwaka jana, rekodi bado zinaonyesha Yanga na Geita zinapokutana inakuwa mechi ya ushindani wa hali ya juu, japo mara zote Yanga imeibuka na ushindi.

Tangu msimu uliopita ilipopanda daraja na kucheza Ligi Kuu Geita na Yanga zimeshakutana mara nne na zote Yanga imeshinda, mara tatu ikiwa kwa bao 1-0 mtawalia na mara ya mwisho wiki chache zilizopita ikashinda 3-1.

Rekodi hizo hazijaishtua Geita, kwani benchi la ufundi na wachezaji wa timu hiyo wana matumaini makubwa kwenye mechi ya leo kutokana na maandalizi iliyoyafanya, pia inaipa Yanga hali ya kujiamini zaidi sababu zinazoweza kuifanya mechi hiyo kuwa ngumu na ya kuvutia kutazama.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha mkuu wa Geita, Fred Felix ‘Minziro’ alisema; “Tunajua ubora wa Yanga na mara zote tulipokutana nao tulipoteza mechi. Kuna utofauti wa mechi hizi za ASFC na ligi kwani katika hatua hii ukifungwa unatoka.”

Kocha msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze atakayesimamia mechi hiyo baada ya Mkuu wake Nasreddine Nabi kuwa nchini Ubelgiji akifuatilia hati yake ya kusafiria, alisema; “Tunahitaji kutetea taji hili tulilolichukua msimu uliopita, hivyo lazima tucheze kibingwa na kushinda.

“Geita ni miongoni mwa timu nzuri na kila tunapokutana mechi inakuwa ngumu, tunaiheshimu lakini tunaamini tutakuwa na mchezo mzuri na mwisho kuondoka na ushindi utakao tupeleka nusu fainali,” alisema Kaze.

Yanga inataka kuchukua ubingwa wa ASFC msimu huu ili kuifikia Simba kuwa timu zilizobeba kombe hilo mara nyingi zaidi (3). Timu nyingine zilizowahi kubeba kombe hilo ni Azam na Mtibwa Sugar kila moja ikilichukua mara moja.

Chanzo: Mwanaspoti