Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga, Geita kusaka majibu leo

Yanga Warm Up Mbarali.jpeg Yanga wakipasha

Sat, 7 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baada ya kupoteza mechi zao zilizopita za Ligi Kuu kwa matokeo yanayofanana, Geita Gold na Yanga zinakutana leo kwenye mechi itakayofanyika Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza kuanzia saa 10:00 jioni.

Wenyeji Geita Gold walitandikwa mabao 2-1 nyumbani na KMC, wakati Yanga ikipokea kichapo kama hicho kutoka kwa Ihefu FC, mchezo uliofanyika Jumatano kwenye Uwanja wa Highlands Estastes, Mbarali.

Kupoteza mechi ya leo itakuwa ni matokeo mabaya kwa kila upande, kwani yataathiri harakati za kutimiza malengo ambayo zimejiwekea hasa kutokana na mwenendo wa wapinzani wao wengine katika ligi hiyo msimu huu.

Kwa Geita Gold, kuangusha pointi tatu kutazidi kupunguza uwezekano wake wa kumaliza katika nafasi nne za juu katika msimamo wa ligi, wakati kwa Yanga itaweka njiapanda katika vita yao ya kuwania ubingwa.

Mabadiliko makubwa yanategemewa kwenye kikosi cha Yanga leo, wakati Dickson Job, Joyce Lomalisa, Yao Attohoula, Khalid Aucho, Mudathir Yahya, Maxi Nzengeli, Clement Mzize na Aziz Ki wakitegemewa kuanza mbele ya Kibwana Shomari, Bakari Mwamnyeto, Zawadi Mauya, Salum Abubakar 'Sure Boy', Nickson Kibabage, Kennedy Musonda, Mahlatse Makudubela na Jesus Moloko.

Wenyeji Geita Gold wanapaswa kuimarika zaidi katika eneo la ulinzi, hasa kuepuka makosa binafsi ya wachezaji ambayo yameonekana kuwa na mwendelezo msimu huu ili waweze kuidhibiti safu ya ushambuliaji ya Yanga, ambayo imekuwa na wastani wa kufunga mabao matatu katika kila mchezo kwenye Ligi Kuu msimu huu.

Uwanja wa CCM Kirumba ambao mchezo huo utachezwa, umekuwa na neema kwa Yanga, kwani mabingwa hao watetezi wamepata ushindi katika mechi zao zote tano zilizopita za Ligi Kuu walizocheza hapo.

Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alisema licha ya kutopata muda wa kutosha wa kufanya maandalizi ya maana, anajivunia kuwa na wachezaji wenye haiba kubwa na ubora ambao wanaweza kupambana na kupata ushindi katika mazingira yoyote.

"Tumeshaiangalia timu kiufundi naamini tutafanya uamuzi sahihi kesho. Tunajua tutakuwa na mechi ngumu, itakuwa ngumu kwetu, lakini falsafa yangu ni kucheza mpira mzuri wa kuvutia kuwavutia mashabiki," alisema Gamondi.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa Yanga, Kocha wa Geita Gold, Hemed Suleiman 'Morocco' alisema amewaandaa vizuri wachezaji wake kukabiliana na Yanga, ingawa mchezo utakuwa mgumu mbele ya mabingwa watetezi.

"Sote tumepoteza mechi zilizopita, tunajua mechi itakuwa ngumu, lakini nimejaribu kuwatengeneza wachezaji wangu kisaikolojia sisi tumesimama vizuri naamini tutapata ushindia.

"Yanga ni timu nzuri, imekuwa na mtiririko mzuri wa kiwango na matokeo na mchezo utakuwa mgumu zaidi, lakini nasi tutapambana kupata ushindi na kuinuka. Najiamini kwa ajili ya wachezaji wangu jinsi tulivyojiandaa tumeangalia udhaifu wa Yanga," alisema Morocco

Katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, wenyeji KMC baada ya kupata ushindi katika mechi mbili mfululizo zilizopita dhidi ya JKT Tanzania na Geita Gold, watakuwa na kibarua kigumu mbele ya Ihefu FC iliyotoka kupata ushindi dhidi ya Yanga.

KMC inaingia katika mchezo huo ikimtegemea zaidi nyota wake, Waziri Junior, ambaye amekuwa moto wa kuotea mbali kwa kufumania nyavu siku za hivi karibuni, akifunga mabao mawili katika mechi mbili zilizopita.

Ihefu FC inaelekeza matumaini yakje kwa Charles Ilanfya, ambaye alipachika bao la ushindi dhidi ya Yanga kwenye mchezo uliopita.

Ligi Kuu itaendelea kesjo, Simba ikiwa ugenini dhidi ya Singida Fountain Gate, huku maafande wa Magereza,  Tanzania Prisons ikiikaribisha Mtibwa Sugar.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live