Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga, Dodoma Jiji ni funga mwaka

0a69c900010e150953271c20594c2fbe.jpeg Yanga watafunga mwaka kwa style ya namna gani

Fri, 31 Dec 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Vinara wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara Yanga leo wanashuka dimbani kuwakaribisha Dodoma Jiji katika mchezo wa raundi ya 11 kwenye Uwanja wa Benjamin, Mkapa.

Mchezo huo wa kufunga mwaka unatarajiwa kuchezwa kuanzia saa 1:00 usiku.

Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo Dar es Salaam jana, Kocha Msaidizi wa Yanga Cedric Kaze alisema mchezo huo unaweza kuwa mgumu kwa sababu wanacheza na timu yenye uzoefu kwenye ligi na isiyokubali kufungwa kiurahisi.

“Ni mchezo wa mwisho wa kufunga mwaka, tunajua ugumu wa mechi hiyo, ni timu imeshakuwa na uzoefu kwenye ligi na mwalimu mwenye uzoefu, mara nyingi tukikutana nao hawafunguki sana,”alisema.

Alisema wamepitia mechi walizocheza nao mwaka jana na zile zilizochezwa msimu huu na kujipanga dhidi yao kuhakikisha wanashinda mchezo huo na kufunga mwaka salama.

Kaze alisema: “tumerekebisha mapungufu yetu tuna imani tumejiandaa vizuri tutaonesha kiwango kizuri ili tupate pointi tatu,”.

Alisema wachezaji watakaokosekana kutokana na sababu mbalimbali ni Djuma Shaban aliyeumia katika mechi dhidi ya Biashara na golikipa namba moja Djigui Diarra aliyekwenda kujiunga na timu yake ya Taifa ya Mali inayojiandaa na michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon).

Kocha huyo alisema kuna wachezaji wengi wazuri wana imani watafanya vizuri pia. Kwa upande wa Kocha Msaidizi wa Dodoma

Jiji Renatus Shija alisema wamejipanga vizuri kuwakabili Yanga na kulipiza kisasi baada ya msimu uliopita kuwafunga.

Msimu uliopita Yanga iliondoka na pointi nne kutoka kwa Dodoma Jiji, mchezo wa kwanza wakishinda mabao 3-1 Benjamin Mkapa na ule wa mzunguko wa pili wakitoka suluhu kwenye Uwanja wa Jamhuri Dodoma.

Shija alisema wanawajua wapinzani wao vizuri kuwa ni timu inayobadilika kulingana na mechi na kwamba wamejipanga kwa kuja na mbinu zitakazowamaliza mapema na kuibuka na ushindi.

“Yanga wanabadilika kufuatana na mechi. Wakifungwa ndio wanaamka.

Tumekuja na mipango tofauti. Na hata tukija kufungwa tunamaliza kazi dakika za mwisho,”alisema.

Nahodha wa Dodoma Jiji Mbwana Kibacha alisema

wao kama wachezaji watafanya kazi waliyoelekezwa ili waondoke na matokeo mazuri katika mchezo huo.

Yanga na Dodoma Jiji zinatofautiana pointi 10, vinara hao wakiongoza kwa pointi 26 huku wageni wao wakiwa na pointi 16 katika michezo 10 ikishika nafasi ya sita.

Atakayeshinda mchezo huo atakuwa amefunga mwaka vizuri na kwenda kula mwaka mpya kwa furaha.

Chanzo: www.habarileo.co.tz