Uongozi wa Klabu ya Young Africans umetamba kuendelea kuishi na ndoto yao ya kubeba ubingwa wa Afrika hata kama wataukosa msimu huu 2022/23.
Young Africans tayari imeshatinga Hatua ya Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika, baada ya kuifunga US Monastor ya Tunisia 2-0, jana Jumapili (Machi 19) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Makamu wa Rais wa Young Africans, Arafat Haji amesema wataendelea kuwa na ndoto hiyo ya kuwa timu ya kwanza ambayo italeta taji la Afrika nchini Tanzania.
“Malengo yetu sisi kama viongozi ni kuhakikisha kuwa tunafanikiwa kuuleta ubingwa wa michuano ya kimataifa hapa nchini na kuwa timu ya kwanza kufanya hivyo kwa timu kutoka katika taifa hili.”
“Hata kama sio msimu huu lakini itakuwa kwa misimu mingine, Young Africans tunayo nia hiyo ya kuhakikisha kuwa tunafikia malengo yetu na tunaamini kuwa inawezekana, kikubwa ni mashabiki kuwa na sisi bega kwa bega,” amesema kiongozi huyo.
Ushindi dhidi ya US Monastir umeiwezesha Young Africans kufikisha alama 10 ambazo zinaiweka kileleni mwa msimamo wa Kundi D, ikiizidi mabao aya kufunga na kufungwa miamba hiyo ya Tunisia.
Young Africans imebakisha mchezo mmoja wa Kundi D, ambapo itacheza dhidi ya TP Mazembe mwanzoni mwa mwezi April mjini Lubumbashi, DR Congo.