Mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya Yanga na Dodoma Jiji umemalizika kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi kwa wenyeji kushinda mabao 4-2 na kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
Mabao ya Yanga yamefungwa na Kennedy Musonda dakika ya 39, Mudathir Yahya akifunga mawili dakika ya 70, 90 na Farid Mussa dakika ya 88.
Mabao ya Dodoma Jiji yamefungwa na Collins Opare dakika ya 59 huku la pili likifungwa na Seif Karihe dakika ya 67.
Zifuatazo ni dondoo kadhaa za mchezo huu.
Ushindi wa leo unaifanya Yanga kutetea tena ubingwa wa Ligi Kuu Bara ikiwa imefikisha pointi 74 ambazo hazitaweza kufikiwa na timu yoyote huku pia ikibakiwa na michezo miwili ambayo ni dhidi ya Mbeya City na Tanzania Prisons.
Ubingwa huu kwa Yanga ni wa 29 kwake kuuchukua tangu mwaka 1965 ikiwa ndio vinara ikifuatiwa na Simba iliochukua mara 22.
Bao la Musonda linamfanya nyota huyo kufikisha mabao mawili ya Ligi Kuu Bara hadi sasa baada ya awali kufunga katika ushindi wa mabao 3-1, dhidi ya Geita Gold, Machi 12, mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex.
Tangu Dodoma Jiji ipande Ligi Kuu Bara msimu wa 2019/2020 haijawahi kuifunga Yanga kwani katika michezo sita waliyokutana baina yao imepoteza mitano na kuambulia sare mmoja tu.
Katika michezo hiyo Dodoma Jiji imefungwa jumla ya mabao 15 huku Yanga ikiruhusu matatu tu.
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa Novemba 22, mwaka jana baina ya timu hizi, Yanga ilishinda pia kwa mabao 2-0, yaliyofungwa na mshambuliaji, Fiston Mayele.
Ushindi mkubwa kwa Yanga dhidi ya Dodoma Jiji ni ule wa mabao 4-0, ilioupata Desemba 31, mwaka 2021 kwenye Uwanja Benjamin Mkapa yaliyofungwa na nyota, Fiston Mayele, Jesus Moloko, Feisal Salum 'Fei Toto' na Khalid Aucho.
Seif Karihe mwenye mabao matano ya Ligi Kuu Bara akiwa na Dodoma Jiji ndiye mchezaji wa kwanza wa timu hiyo kuifunga Yanga wakati kikosi hicho kikipoteza mabao 3-1, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Desemba 19, 2020.
Katika mchezo huo Karihe aliipatia Dodoma Jiji bao la mapema tu dakika ya tatu huku yale ya Yanga yakifungwa na Lamine Moro, Saidi Ntibazonkiza 'Saido' ambaye anayeichezea Simba kwa sasa na Bakari Nondo Mwamnyeto.
Mchezo pekee baina ya timu hizi ambao haujaruhusu bao tangu Dodoma Jiji ipande Ligi Kuu Bara msimu wa 2019/2020 ni wa Julai 18, mwaka 2021 kwenye Uwanja wa Jamhuri Dodoma.
Juni 15, mwaka jana Yanga ilitangaza ubingwa wa 28 katika Ligi Kuu Bara baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Coastal Union kwenye mchezo uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Katika mchezo huo Yanga ilitangaza ubingwa huo baada ya kufikisha pointi 67 tena bila ya kupoteza kufuatia kucheza michezo 27 kwa mabao yaliyofungwa na mshambuliaji, Fiston Mayele aliyefunga mawili na nyota wa zamani wa timu hiyo Mkongomani, Chico Ushindi.
Katika michezo 28 ambayo Yanga imecheza imeshinda 24, sare miwili na kupoteza pia miwili ikiendelea kuongoza Ligi Kuu Bara na pointi 74 huku Dodoma Jiji ikishinda tisa, sare minne na kupoteza 15 ikiwa nafasi ya 10 na pointi 31.