Vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara Yanga wamesema wanahofu mchezo wao na Biashara utakuwa mgumu.
Yanga itakuwa mwenyeji wa Biashara United ya Mara kwenye Uwanja wa Benjamin, Mkapa, Dar es Salaam kesho.
Kocha wa makipa wa Yanga, Razak Siwa amesekuwa, mchezo dhidi ya Biashara unaweza kuwa mgumu kwani timu hiyo mara nyingi wanapokutana nao inaonesha ushindani wa hali ya juu.
Amesema wataingia katika mchezo huo kwa kuwaheshimu wapinzani wakijua ni moja ya timu nzuri zenye upinzani na kwamba imetoka kushiriki kwenye mashindano ya kimataifa hivyo haipaswi kubezwa.
“Mechi dhidi ya Biashara haitakuwa rahisi kama mnavyojua Biashara ni miongoni mwa timu nzuri zenye ushindani, lakini sisi tunaendelea na maandalizi yetu kwa kufanya mazoezi, nina imani hadi kufika siku ya mechi tutakuwa tuko vizuri,” alisema Siwa.
Kwa upande wake, Kocha Msaidizi wa Biashara United, Omar Madenge alisema wako tayari kuikabili Yanga.
Alisema licha ya kutofanya vizuri katika michezo iliyopita wanaendelea na maandalizi na kikubwa kufanyia kazi tatizo la ufungaji ambalo limeonekana sugu na kuahidi mambo yatakuwa mazuri mchezo ujao.
Timu hiyo itacheza bila Kocha Mkuu Patrick Odhiambo aliyejiuzulu kutokana na uongozi kushindwa kumtimizia baadhi ya mahitaji ambayo yalichangia klabu hiyo kushindwa kufanya vizuri.
“Kikubwa ni kufanya vizuri, niwahakikishie mashabiki wawe na imani na timu yetu, najaribu kurudisha ari kwa wachezaji waweze kufunga mabao,” alisema Madenge.
Msimu uliopita timu hiyo ilivuna pointi sita kutoka kwa Biashara United, mechi ya raundi kwanza ikishinda bao 1-0 ushindi unaofanana na ule wa raundi ya pili.