Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga, Azam zishindwe zenyewe, JKU, Uhamiaji mmh

UYFUFFY Yanga, Azam zishindwe zenyewe, JKU, Uhamiaji mmh

Sat, 24 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Timu tatu za Tanzania leo zitakuwa katika viwanja tofauti barani Afrika zikicheza mechi za marudiano za raundi ya kwanza ya mashindano ya klabu Afrika huku kukiwa na mategemeo tofauti kutokana na matokeo ya mechi za mwanzo zilizochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita.

Katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, Yanga itaikaribisha Vital'O ya Burundi kuanzia saa 1:00 usiku ikihitaji matokeo ya sare, ushindi au hata kupoteza kwa idadi ya mabao chini ya manne ili isonge mbele.

Urahisi wa Yanga kusonga mbele unatokana na ushindi mnono wa mabao 4-0 ambao iliupata katika mechi ya kwanza ambayo ilihesabika iko ugenini dhidi ya wapinzani wao hao kutoka Burundi.

Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi amesema kuwa matokeo ya mchezo wa kwanza hayawezi kuwafanya waidharau Vital'O leo na ameandaa kikosi chake ili kipata matokeo mazuri leo.

“Tunajiamini na matokeo tuliyopata mechi iliyopita lakini bado tunaheshimu kuwa tuna dakika 90 nyingine za kupambana, kipaumbele chetu ni kufuzu hatua unayofuata.

"Huwa sipendi kusikiliza mpinzani anawaza au kuongea nini. Mara nyingi natumia muda wangu kuandaa timu yangu bora. Nina timu bora ambayo imekamilika kila idara. Kwenye mpira lazima uwe na weledi kwa kuheshimu wapinzani.

Siwezi kusema kuwa hatuwezi kufungwa goli tano, lakini sio jambo ambalo natarajia kuliona likitokea. Nina matumaini makubwa sana na wachezaji. Nafahamu watakuja kwa nguvu kutafuta magoli nasi tumejiandaa kwa kila mbinu," alisema Gamondi.

Katika mchezo huo, Azam FC inahitaji ushindi au sare ya aina yoyote ili iweze kutinga hatua inayofuata baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 katika mechi ya kwanza Jumapili iliyopita.

Ni mechi ambayo Azam inaonekana imeipa uzito mkubwa kutokana na msafara mkubwa ambao imesafiri nao kwenda Kigali kuhakikisha hakuna kitakachoharibika nje na ndani ya uwanja katika dakika 90 za mchezo.

Msafara huo unajumuisha wachezaji 25 na waliobakia wakiwa ni maofisa wa benchi la ufundi, wawakilishi kutoka shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) na viongozi wa timu hiyo.

Kocha wa Azam FC, Youssouf Dabo alisema kuwa wamejipanga kupata ushindi wa ugenini dhidi ya APR.

"Mchezo wa kwanza hatukupata ushindi mkubwa kama tulivotarajia kutokana na staili ya wapinzani wetu ambao muda mwingi waliutumia kujilinda lakini pia walicheza soka la kutumia nguvu lakini tunaamini mchezo wa marudiano utakuwa tofauti na tutaingia kwa staili ya kitofauti.

"Tunaamini kilichojitokeza katika mechi ya kwanza hakitojirudia tena na tutafanya vizuri zaidi kwani tumeshawasoma na kufanya kazi kile ambacho tumekifanyia tathmini," alisema Dabo.

Kuanzia saa 2:00 usiku mabingwa wa Zanzibar, JKU watakuwa na mlima mrefu wa kupanda ili waweze kufanya maajabu ya kusonga mbele dhidi ya Pyramids baada ya kuchapwa mabao 6-0 katika mechi ya kwanza ambayo walikuwa nyumbani japo ilichezwa Misri.

JKU inahitaji ushindi wa kuanzia mabao 7-0 ili iingie hatua inayofuata jambo ambalo halionekani kama linaweza kutokea kutokana na ubora wa Pyramids FC.

Mchezo huo wa Pyramids FC dhidi ya JKU utachezwa katika Uwanja wa Juni 30.

Chanzo: Mwanaspoti