Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga, Azam zaibeba Simba

27141 Pic+yanga.png Yanga, Azam zaibeba Simba

Mon, 22 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

***Ni katika mbio za kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kutoka suluhu kwenye...

YANGA na Azam FC zimeendelea kuisafishia njia ya ubingwa Simba baada ya kutoka sare ya bila kufungana katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini, Dar es Salaam jana.

Kwa matokeo hayo sasa, Simba inahitaji pointi nane tu katika mechi zake nane zilizosalia ili kufikisha pointi 83 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine kwenye ligi hiyo inayotarajiwa kumalizika Julai 26, mwaka huu.

Mabingwa watetezi, Simba wanaendelea kukaa kileleni katika msimamo wa ligi hiyo wakifuatiwa na Azam huku Yanga ikiendelea kubakia kwenye nafasi ya tatu.

Azam ambayo baada ya suluhu ya jana imefikisha pointi 58 na endapo itashinda mechi zake zilizobakia itafikisha pointi 82 wakati Yanga ambayo sasa ina pointi 56, yenyewe ikishinda michezo iliyosalia itafikisha pointi 80.

Mechi ya jana ilishuhudia timu zote zikikosa magoli mengi ya wazi ambayo kama zingetumia vema, basi kungekuwa na idadi kubwa ya mabao katika mechi hiyo.

Dakika ya tisa, Idd Kipangwile alimegewa pande safi na Richard Djodi, lakini kwa mshangao wa wengi alipiga shuti kubwa lililopaa juu ya lango na dakika tatu baadaye, Kipagwile kwa mara nyingine tena, akiwa amebaki na kipa wa Yanga, Metacha Mnata, alishindwa kufunga baada ya shuti lake kumgonga miguuni kipa huyo na baadaye kuokolewa na mabeki.

Baada ya hapo, Yanga ilicharuka na dakika ya 15 ilifanya mashambulizi mfululizo kwa dakika moja na kukosa magoli matatu ya wazi.

Alikuwa ni mshambuliaji, David Molinga aliyeshindwa kuunganisha krosi kutoka kwa winga wa kulia iliyopigwa na Patrick Sibomana, baada ya hapo kilitokea kizaazaa kwenye lango la Azam na mpira ukawa unakwenda wavuni huku kipa Banjamin Haule akiwa hayupo golini, lakini Mudathir Yahaya aliokoa kabla haujavuka mstari wa goli.

Sekunde chache baadaye mabeki wa Azam walijichanganya kwa kurudisha nyuma mpira kimakosa na kumkuta Molinga, akiwa yeye na kipa Haule, lakini shuti lake liliishia mikononi mwa kipa huyo.

Ilikuwa zamu ya Djodi naye kukosa magoli dakika ya 23, alipobaki yeye na kipa, Metacha lakini mpira ulimbabua kipa huyo na ulipomrudia na kupiga 'tiktak' ukaishia tena mikononi mwa kipa huyo.

Feisal Salum nusura aiandikie Yanga bao alipofumua shuti la umbali mrefu, lakini Haule aliudaka kwa ustadi mkubwa, huku Sibomana naye akipewa zawadi ya pasi kutoka kwa mabeki wa Azam, lakini kipa huyo wa Azam jana alikua imara na kuudaka mpira huo.

Kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko, huku mshambuliaji nyota wa Yanga, Bernard Morrison, naye akipata nafasi kipindi cha pili na kuifanya Azam kurudi nyuma na kuanza kuzuia kwa muda mrefu mchezo, ikionekana wakihitaji zaidi sare, tofauti na kipindi cha kwanza.

Ilikuwa ni dakika ya 49, wakati Morrison alipopiga krosi iliyokatika na kutaka kuingia wavuni, lakini Haule aliyeonekana kucheza vema jana aliokoa.

Mchezaji wa Azam aliyetokea benchi, Idd Chilunda aliikosesha timu yake magoli mawili, alipobaki na kipa Metacha, dakika ya 68 na 69, baada ya mashuti yake dhaifu kuishia mikononi mwa kipa wa Yanga wakati Nicholaus Wadada naye aliikosesha Azam bao, alipowapiga chenga mabeki wa Yanga, lakini shuti lake dhaifu lilidakwa.

Ligi hiyo itaendelea tena Jumatano kwa Simba kuwafuata Mbeya City jijini Mbeya wakati Yanga itawakaribisha Namungo FC kutoka Lindi na Azam itakuwa mgeni wa Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live