Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga, Azam haijawahi kutokea

51246 Yanga+pic

Wed, 10 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati baadhi ya timu za Ligi Kuu Tanzania Bara zimebakiza mechi tano kabla ya kumaliza mashindano, Yanga na Azam hazijacheza mechi zao mbili msimu huu.

Licha ya Yanga na Azam FC kutoshiriki mashindano yoyote ya kimataifa, hazijakutana katika mechi zote mbili za Ligi Kuu.

Kwa mujibu wa ratiba ya Ligi Kuu iliyofanyiwa marekebisho inaonyesha Yanga na Azam zilipangwa kucheza mechi yao ya mzunguko wa kwanza Aprili 29 kabla ya kurudiana kwenye raundi ya pili Mei 26.

Tangu kuanza kwa msimu huu, ratiba ya Ligi Kuu ilikuwa ikifanyiwa marekebisho mara kwa mara na kuibua mjadala kwa klabu na wadau wa soka nchini.

Yanga

Akizungumza jana, Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Omari Kaaya alisema hawakuwa na namna zaidi ya kukubali mechi zao kusogezwa mbele licha ya kutoshirikishwa katika uamuzi.

Kaaya alisema hawakuwahi kuitwa na Bodi ya Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kukaa meza moja na Azam kujadili mabadiliko ya ratiba.

“Kimsingi hatukuelezwa chochote kuhusu mabadiliko ya ratiba zaidi ya kuletewa, hatukuweza kukataa, tulikubali,” alisema Kaaya.

Alisema athari inayoweza kuikuta Yanga ni mashindano hayo kukosa ushindani wa kweli kutokana na mwenendo wa ligi ulivyo sasa.

Kaaya alisema Yanga na Azam zimekuwa na ushindani mkali tangu kuanza msimu huu, lakini kitendo cha kutocheza mechi zao kinaweza kuiathiri Yanga katika ushiriki wa Ligi Kuu.

Azam

Kitendo cha timu hizo kutocheza mechi zao hakikuiacha salama Azam, kocha wa timu hiyo, Idd Nassor ‘Cheche’ alisema kutochezwa mechi hiyo kumepunguza ari ya ushindani.

“Tunaweza kucheza wakati tayari matokeo yanajulikana kwamba huyu akishinda inakuwa hivi, hiki si kitu kizuri katika ligi,” alisema kocha huyo.

Kocha huyo alisema tangu kuanza msimu huu ligi imekosa msisimko kama zamani kutokana na ratiba hiyo kupanguliwa mara kwa mara .

Kauli Bodi ya Ligi

Akizungumza jana, Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi (TPLB), Steven Mnguto alidai kuwa kitendo cha Yanga na Azam ni tatizo katika mashindano hayo.

“Siyo Yanga na Azam hata sisi Coastal Union hatujacheza na Simba msimu huu, ratiba ya ligi ilichafuka wakati wa Kombe la Mapinduzi na mashindano ya kimataifa,” alisema Mnguto.

Yanga inaongoza Ligi Kuu ikiwa na pointi 71 baada ya kucheza mechi 30 na Azam ipo nafasi ya pili kwa pointi 62 katika mechi 29 ilizocheza.



Chanzo: mwananchi.co.tz