Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga, Azam FC ni vita na kisasi

Sopu Azam Fc.jpeg Yanga, Azam FC ni kisasi

Mon, 12 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mabingwa watetezi wa Kombe la Shirikisho la Azam, Yanga wanashuka dimbani kutetea taji lao kwa kuikabili Azam FC, mchezo wa fainali utakaopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga leo.

Hatahivyo, Yanga inashuka dimbani bila ya wachezaji wake wawili nyota, Fistol Mayele na Stefan Aziz Ki, ambao wamekwenda kuzitumikia timu zao za taifa kwa ajili ya mechi za kufuzu kwa Kombe la Mataifa Afrika (Afcon 2023).

Hii inakuwa fainali ya pili kuzikutanisha timu hizi katika mchezo wa kwanza uliochezwa 2016, ambapo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 3-1 yaliyofungwa na Amissi Tambwe mawili na Deus Kaseke.

Mara ya mwisho timu hizo kukutana kwenye mchezo wa kimashindano ilikuwa mechi ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa Desemba 25, 2022 na Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 3-2.

Safari ya Yanga kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam ilianzia raundi ya pili kwa kuivurumisha Kurugenzi mabao 8-0 kwenye dimba la Benjamin Mkapa huku mzunguko wa 32 bora ikiindosha Rhino Rangers ya Tabora kwa kuibugiza mabao 7-0 kwenye uwanja huo huo.

Hatua ya 16 bora Yanga iliiondosha Tanzania Prisons kwa kuichapa mabao 4-1 na kutinga hatua ya nane bora ambapo iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Geita Gold kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Wakati Azam ilianzia raundi ya pili kwa kuivurumisha Malimao mabao 9-0, mzunguko wa 32 bora ikaibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Dodoma Jiji.

Hatua ya 16 bora iliiondoa Mapinduzi kwa kuifunga mabao 2-0, Robo fainali iliibuka na ushindi wa bao 1-0 huku nusu fainali ikiibuka na ushindi wa mabao 2-1 mbele ya Simba.

Akizungumza jana Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, alisema licha kuwa hawajafanya maandalizi yoyote, hawataingia kinyonge kwenye mchezo huo kwani wataenda kutetea ubingwa.

“Tunafurahi kuwa hapa kwa ajili ya mchezo wa fainali dhidi ya Azam tutafanya kila jitihada kuhakikisha tunatetea ubingwa wetu

“Tunaenda kwenye mchezo huu tukiwakosa wachezaji wawili, Fiston Mayele na Stefan Aziz Ki, tulipojulishwa tarehe ya mchezo wa fainali tulijaribu kuongea na mashirikisho yao ili waturuhusu tuwatumie wachezaji waondoke baaada ya mchezo, lakini Congo na Burkina Faso waligoma ila Uganda, Mali na Zambia walikubali, “alisema Nabi.

Aziz Ki atacheza mchezo huo wa kufuzu Afcon akiwa na Burkina Faso itakayocheza na Cape Verde huku Mayele anayecheza DR Congo atapambana na Gabon, ambapo michezo yote hiyo itachezwa Juni 18.

Mbali na kukosa mchezo huo mastaa hao pia watakosekana katika Usiku wa Tuzo za Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) zitakazofanyika leo jijini Tanga baada ya kuisha kwa fainali ya ASFC.

Naye Kocha Msaidizi wa Azam FC, Kali Ongala, alisema mchezo wa fainali haujawahi kuwa rahisi, itakuwa mechi ngumu wanaingia kwenye mchezo huo wakiiheshimu Yanga anaamini timu bora itaenda kushinda mchezo huo.

“Yanga wana wachezaji wazuri tunaingia kwa tahadhari kuwakosa wachezaji wawili hakuwezi kuiathiri timu, wana kikosi kizuri kama tukicheza vizuri tuna uwezo wa kuchukua ubingwa.

“Tumejiandaa kiufundi na kiakili fainali ni mchezo wenye utofauti tunaamini itakuwa mechi ngumu tunaingia kwenye mchezo huu tukiwa kwenye kiwango kizuri baada ya kushinda michezo yetu miwili iliyopita kikubwa ni kupunguza mihemko,” alisema Ongala.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live