Siku moja baada ya fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC) iliyokutanisha Azam FC na Yanga, na wana Chamazi kupoteza kwa bao 1-0, ukurasa wa Instagram wa matajiri hao wa jiji ukaanza kupambwa na kifungu cha maneno ya Kiingereza cha THANK YOU.
Maneno hayo yalikuwa yakitumika kuwaaga watumishi wa klabu hiyo waliotoka kumaliza msimu. Ilianza na watu wawili kutoka benchi la ufundi; kocha wa makipa Dani Cadena kutoka Hispania na kocha wa utimamu wa miili, Moadh Hiraoui kutoka Tunisia.
Baadaye wakafuata wachezaji kadhaa kisha wakaja wengine wawili wazito, Agrey Moris ambaye katikati ya msimu alistaafu kucheza na kuwa kocha pamoja na Kally Ongala ambaye alimaliza msimu kama kocha mkuu.
Sote tunajua kwamba Azam FC imeshamtangaza Yousouph Dabo kutoka Senegal kama kocha mkuu kwa msimu ujao na baadhi ya makocha hupenda kufanya kazi na watu wao waliowazoea na kufanya nao kazi sehemu nyingine walikotoa. Kwa hiyo haishtui kuona kina Kally wakiondoka.
Lakini hii siyo hali halisi kwa Azam FC. Thank You hizi zinazomiminika kwenye Instagram yao zinatokana na sababu tofauti kabisa.
Ni hivi... Msimu huu wakati unaanza benchi la ufundi la Azam FC liliongeza watu watatu. Kali Ongala, kama kocha wa washambuliaji; Dani Cadena kama kocha wa makipa na Mikel Guillen akiwa ni kocha wa utimamu wa miili.
Wataalamu hawa wakaungana na waliokuwepo Abdihamid Moallin na Omar Abdikarim Nasser kama kocha msaidizi. Timu ikaenda Misri kwenye mji wa starehe wa Gouna kuweka kambi ya maandalizi ya msimu mpya.
Ikiwa kule, yakaanza mapinduzi ya ndani. Mikel Guillen akampindua Omar Abdikarim Nasser kama kocha msaidizi, akawa yeye. Fumba na kufumbua, raia huyo wa Hispania akawa na nguvu kwenye timu kuliko hata Moallin, kocha mkuu.
Hapo ndipo jahazi la Azam FC lilipoanza kuzama. Moallin akapoteza nguvu na baada ya mechi mbili za ligi akishinda moja na sare moja, akatimuliwa yeye na Omar wake.
Timu ikawa chini ya Mohamed Badru, kocha wa timu za vijana pamoja na Kally. Wawili hawa wakapewa jukumu la kuiandaa timu kwa ajili ya mchezo dhidi ya Yanga uliokuwa wiki moja mbele.
Wakati wa maandalizi hayo, Badru akatofautiana kauli na Mikel, yule aliyefanya mapinduzi kule Misri. Jamaa aliamini kwamba kuondoka kwa Moallin kungemfanya yeye kabidhiwe timu. Kwa hiyo alipokabidhiwa Badru akaanza kumletea chokochoko.
Ukatokea ugomvi mkubwa mazoezini. Badru na Mikel walikwaruzana pakubwa mno.
Habari zikafika kwa wamiliki wa timu ikabidi wote wakaitwa kujadiliana hilo. Baada ya mazungumzo, wakapata muafaka kwamba kila mmoja aendelee na majukumu yake ya msingi. Mikel abaki na utimamu wa miili akimuachia Badru na mbinu zake.
Na hii ndiyo sababu ya Azam FC kumtangaza haraka sana kocha mpya aliyekuja kuchukua nafasi ya Moallin, Dennis Lavagne. Lavagne alitangazwa siku ambayo Azam Ilikuwa inacheza na Yanga, ile mechi ya 2-2. Lengo lilikuwa kutuma ujumbe kwa wote waliopo kwenye benchi kwamba kati yao hakuna atakayekuwa kocha mkuu.
Mechi ikapita na kocha mpya akaanza kazi. Lakini Mikel hakutulia. Akaendelea na chokochoko ndani ya timu. Alianza kwa kugombana na Mhispaniola mwenzake, Dani Cadena kisha na wengine wengi akiwemo Nyasha Charandula, mtaalamu wa sayansi ya michezo wa timu.
Wenye timu wakagundua kwamba jamaa ni tatizo wakamtoa haraka sana, hata kabla ya mechi dhidi ya Al Akhdar. Timu ilipoenda Libya kwenye mchezo huo ndipo akaletwa Moadh Hiraoui, raia wa Tunisia ambaye alishafanya kazi na Esperance na Al Hilal ya Sudan.
Chini ya Lavagne hali ikazidi kuwa mbaya na kuzaa mpasuko mkubwa kwenye benchi la ufundi. Kuelekea mchezo dhidi ya KMC ambao Azam FC ilipoteza 2-1 kulikuwa na ugomvi mkubwa ndani ya basi kati ya Cadena na Lavagne...ugomvi mkubwa mno.
Baada ya huo mchezo, Lavagne akafukuzwa na nafasi yake kuchukuliwa na Kally akisaidiana na Morris. Kally alikaimu nafasi hiyo kwa mechi tano akama kanuni zinavyotaka. Mechi ya kwanza ilikuwa dhidi ya Simba na Azam ikashinda bao 1-0.
Itakumbukwa kwamba Azam FC haikuwahi kuifunga Simba tangu 2017 kwa hiyo ushindi huo ulikuwa na maana kubwa. Kally akaenda kushinda mechi zote tano kama kaimu kocha mkuu. Baada ya mechi hizo Azam ikatakiwa na kanuni za ligi itangaze kocha wake rasmi.
Ikataka kumtangaza Kally lakini hakuwa na vyeti vinavyokidhi hitaji la kikanuni la ligi ya Tanzania. Kanuni za uendeshaji wa ligi ya Tanzania zinataka kocha mwenye leseni A ya CAF au Pro License ya Uefa kwa waliosoma Ulaya. Kally alisoma Ulaya lakini hakuwa na Uefa Pro License, ambacho ndicho cheti kikubwa zaidi Ulaya.
Kumtoa Kally kukaleta ganzi, unamtoaje mtu aliyeshinda mechi zote hizo? Uongozi wa Azam kaona ni busara kumuacha aendelee kwa sababu ya matokeo lakini pia kuepuka mvurugano mkubwa kwa kuleta kocha mwingine kwa sababu hadi hapo ligi iko raundi ya 12, tayari Azam ilishakuwa chini ya wanne Moallin, Badru, Lavagne na Kally.
Kwa hiyo wakaongea na kocha wa makipa, Cadena ambaye ana cheti cha Uefa Pro License, aruhusu cheti chake kipelekwe TFF kama kocha mkuu lakini timu iwe chini ya Kally. Jamaa akakubali lakini kwa dau kubwa kuliko hata mshahara wake. Azam hawakuwa na namna, wakamlipa.
Japo alipewa hela nyingi ili kuruhusu cheti chake kutumika lakini Cadena hakupoa, aliona kuna fursa kwake kuwa kocha mkuu, hivyo akaanza harakati za kumpindua Kally. Badala ya cheti chake kutumika, atumike yeye. Vurugu mpya zikaanza ndani ya benchi la ufundi na kuzaa mipasuko mikubwa.
Benchi likagawanyika kila mmoja anaunga mkono upande fulani. Azam ikazidi kuzama.
Kwa kuwa suluhisho la kutumia cheti cha Cadena lilikuwa la muda mfupi hadi mwisho wa msimu, Azam ikaanza harakati za kutafuta kocha mkuu kwa ajili ya msimu uliokuwa unafuata. Wakampata Yousouph Dabo na kumtangaza. Kocha huyo akaja Tanzania, akasaini mkataba na kuondoka.
Baadaye, mwanzoni mwa Mei akaja tena kwa lengo la kuijua vizuri timu yake ili atakapoanza msimu mpya ajue pa kuanzia. Dabo hakuwa na mpango wa kubadilisha benchi lake kama ilivyotokea baadaye, bali hali aliyokutana nayo ndiyo iliyomshtua.
Alipokuja, akatambulishwa kwa wachezaji wote na benchi la ufundi. Baadaye kwa muda wake akawa anaongea na mtu mmojammoja kwenye timu kuanzia wachezaji hadi watu wa benchi la ufundi.
Ni hapo ndipo alipogundua kwamba hakuna umoja ndani ya timu. Anakuja huyu anamsema vibaya mwenzake, akiondoka na kuja mwingine naye anamsema vibaya mwenzake. Hapo ndipo Dabo akaona kwamba hawezi kufanya kazi na hawa watu aliowakuta.
Hapohapo akaomba kikao na wenye timu na kuwaambia kila kitu. Wenye timu wakamkubalia, kilichofuata baada ya hapo ni THANK YOU!