Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yaliyojiri mzunguko wa 29 Ligi Kuu Bara

Yanga Kombe Mkapa.jpeg Yaliyojiri mzunguko wa 29 Ligi Kuu Bara

Sat, 25 May 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Yanga imekabidhiwa taji la ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa staili ya aina yake kwa kombe hilo kushushwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jana kwa chopa, tukio ambalo halikuwahi kufanyika katika ligi hiyo misimu iliyopita, huku ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Tabora United.

Tukio hilo hapana shaka ndilo lilikuwa likisubiriwa kwa hamu na umati wa mashabiki wa Yanga waliojitokeza katika uwanja huo kushuhudia timu yao ikikabidhiwa kombe ambalo inalitwaa kwa mara ya tatu mfululizo.

Saa 8:48 mchana, chopa hiyo ilishuka katikati ya eneo la kuchezea la Uwanja wa Benjamin Mkapa, kisha likashushwa kombe la ubingwa likiteremshwa na mrembo mmoja akisindikizwa na maofisa wa Benki ya NBC ambao ndio wadhamini wa Ligi Kuu Bara.

Awali, kabla ya chopa hiyo kushuka, ilizunguka juu ya uwanja huo mara tatu katika kile kilichoonekana ni kuashiria kitendo cha timu hiyo kutwaa taji mara tatu mfululizo kisha baadaye kushuka taratibu katikati ya uwanja huo.

Wakati wote ikizunguka hadi ilipotua mashabiki maelfu wa Yanga waliokuwa majukwaani walikuwa wakishangilia kwa nguvu.

Baada ya Kombe hilo kushuka dakika tatu baadaye chopa hiyo ikiruka na kuondoka uwanjani hapo huku taji hilo likaingizwa ndani.

Sherehe hizo za kukabidhiwa ubingwa zilinogeshwa zaidi na ushindi wa mabao 3-0, ambapo mabao ya washindi yaliwekwa kimiani na Joseph Guede katika dakika ya 19, Maxi Nzengeli katika dakika ya 48 na la dakika ya majeruhi la Stephane Aziz Ki.

Namba hazipingwi

Ni taji la 30 la ligi kuu kwa Yanga ambalo linaifanya iendeleze rekodi yake kama timu iliyochukua mara nyingi zaidi ubingwa huo ikifuatiwa na Simba ambayo imetwaa taji hilo mara 22 huku Mtibwa Sugar ikilibeba mara mbili.

Timu nyingine ambazo zimewahi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa nyakati tofauti ni Azam FC, Tukuyu Stars, Cosmopolitan, Mseto na Coastal Union ambazo zimechukua mara mojamoja.

Yanga imetwaa ubingwa ikiwa ndio timu iliyovuna idadi kubwa ya pointi ugenini ambapo katika mechi 15, imepata pointi 35, ikifunga mabao 31 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara nane ikifuatiwa na Simba ambayo imepata pointi 34 katika mechi 15, ikifunga mabao 29 na nyavu zake kutikiswa mara 13.

Mchezo wa jana ulikuwa ni wa 46 mfululizo kwa Yanga kucheza nyumbani bila kupoteza mechi ya Ligi Kuu ambapo katika mechi hizo 46, imeibuka na ushindi mara 41 na kutoka sare tano.

Mara ya mwisho kwa Yanga kupoteza mechi ya Ligi Kuu ikiwa uwanja wa nyumbani ni Aprili 25, 2021 ilipofungwa bao 1-0 na Azam FC na hivyo leo imetimiza siku 1128 bila kuonja ladha ya kupoteza mechi nyumbani katika Ligi Kuu.

Hii ni mara ya tatu kwa Yanga kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara tatu mfululizo ambapo mara ya kwanza ilifanya hivyo kuanzia 1968 hadi 1972, ikafanya hivyo tena kuanzia msimu wa 2014/2015 hadi ule wa 2016/2017.

Yanga pia imeweka rekodi ya kuonja ushindi na kufunga angalau bao dhidi ya kila timu iliyopo Ligi Kuu msimu huu.

Kiungo Jonas Mkude anaingia katika kundi la wachezaji waliowahi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara nyingi zaidi ambapo hii ni mara ya sita kwake, mara tano akinyanyua kombe akiwa na Simba na mara moja akiwa na Yanga.

Mtibwa Sugar kwaheri ya kuonana

Kichapo cha mabao 3-2 kutoka kwa Mashujaa FC jana kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika kiliishusha rasmi daraja Mtibwa Sugar kutokana na timu hiyo kubakia na pointi zake 21 ambazo hata zikiongezeka katika mchezo mmoja ambao timu hiyo imebakiza dhidi ya Namungo FC, haitoweza kumaliza juu ya nafasi mbili za mwisho kwenye msimamo wa ligi.

Mabao yaliyoizamisha Mtibwa Sugar ambayo imedumu kwenye Ligi Kuu kwa miaka 28 mfululizo bila kushuka yalifungwa na Reliants Lusajo aliyepachika mawili na moja la Mundhir Vuai huku yale ya kufutia machozi ya wageni yakiwekwa kimiani na Seif Karihe.

Coastal Union rasmi Shirikisho Afrika

Sare tasa ambayo imetoa nyumbani kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga imeihakikishia Coastal Union kumaliza katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi kutokana na kufikisha pointi 42 ambazo haziwezi kufikiwa na Tanzania Prisons wala KMC ambazo ilikuwa ikiwania nazo nafasi hiyo.

Lakini kana kwamba haitoshi, kwa kumaliza katika nafasi ya nne, Coastal Union imejihakikishia tiketi ya kuiwakilisha Tanzania katika Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao na inasubiri kuona itaungana na nani kati ya Simba au Azam FC kushiriki mashindano hayo msimu ujao.

Azam mguu mmoja ligi ya mabingwa Afrika

Kwenye Uwanja wa Azam Complex, wenyeji Azam FC walijiweka katika nafasi nzuri ya kumaliza katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi na kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 5-1 dhidi ya Kagera Sugar.

Mabao mawili ya Feisal Salum ‘Fei Toto’ na mengine matatu yaliyofungwa na Djibril Sylla, Iddi Seleman ‘Nado’ na Kipre Junior yalitosha kuifanya Azam iendelea kusalia katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikifikisha pointi 66 sawa na Simba ambayo iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya KMC.

Hata hivyo Azam ina utofauti mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa ambapo imefunga 61 na kufungwa 21 hivyo utofauti wake wa mabao ni 40 wakati Simba imefunga mabao 57 na kufungwa 25 hivyo ina utofauti wa mabao 32.

Matumaini pekee yaliyobaki kwa Simba ili imalize katika nafasi ya pili ni kupata ushindi dhidi ya JKT Tanzania katika mechi ya mwisho na kuombea Azam ifungwe au itoke sare na Geita Gold au kama zote zikishinda, ipate ushindi ambao utaifanya ilifikie na kulipita pengo la mabao nane ambalo imezidiwa kwa sasa.

Tanzania Prisons uhakika

Sare ya mabao 2-2 dhidi ya Namungo ugenini, imeihakikishia Tanzania Prisons kusalia ligi kuu ambapo imefikisha pointi 34 zilizoifanya iwe salama.

Chanzo: Mwanaspoti