Beki wa kushoto wa Ihefu FC Yahya Mbegu amevunja ukimya na kuweka wazi kuwaniwa na timu za Simba SC na Singida Big Stars, kuelekea mwishoni mwa msimu huu 2022/23.
Mbegu alitajwa kumalizana na Simba SC baada ya mchezo wa Robo Fainali Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ uliozikutanisha timu hizo jijini Dar es salaam mapema mwezi huu, lakini baadae alikanusha uvumi huo.
Mbegu anayesifika kwa ubora anapokuwa dimbani amesema viongozi wa timu hizo, wamekuwa wakimfuata lakini kinachomkwamisha mpaka sasa kufanya maamuzi ni maslahi yake binafsi.
“Bado sijasaini kokote ila kuhusu kuhitajika na timu ni kweli, ni timu nyingi zimekuja za Ligi Kuu na bado sijamalizana na yoyote, kuna timu nimefika nazo kwenye maongezi tu lakini bado hatujakubaliana.”
“Ishu kubwa ni maslahi yangu binafsi kama mchezaji, hapa Ihefu mkataba wangu unaenda mwisho na hata wao pia nimezungumza nao na kukubaliana nao kwa asilimia 80 ila bado tunazungumza,” amesema Mbegu.”
Mchezaji huyo aliyewahi kuitumikia timu ya vijana ya Simba SC, amekiri kuwa anapenda changamoto mpya lakini anahitaji kufikiria zaidi kabla ya kufanya maamuzi kuhusu mustakabali wake bila ya kuangalia ukubwa wa timu inayomhitaji.
Mbegu aliyewahi kukipigia Mwadui na Polisi Tanzania, alisajiliwa Ihefu FC kupitia usajili wa dirisha dogo msimu huu akitokea Geita Gold alikocheza kwa nusu msimu.