Miongoni mwa timu zilizonufaika na usajili wa dirisha dogo ni pamoja na Ihefu FC ambayo ilikuwa na mwanzo mgumu katika Ligi Kuu, lakini kwa sasa inatesa kila kona.
Timu hiyo ya wilayani Mbarali mkoani Mbeya ni miongoni mwa zilizosajili wachezaji wengi ikiwa nao saba wakiwamo wawili wa mkopo kutoka Simba.
Wachezaji waliotua kuongeza nguvu ni Nelson Okwa na Victor Akpan (mkopo kutoka Simba), Adam Adam, David Mwantika, Yacouba Sogne, Mudathir Abdallah, Rashid Juma na Hussein Masalanga.
Hata hivyo, kuingia kwa nyota hao Ihefu iliwapa mkono wa kwaheri wachezaji watano ambao ni Joseph Kinyozi, Evalijestus Mujwahuki, Wema Sadock, Ally Ramadhan ‘Oviedo’ na
Usajili huo umeonekana kuwalipa matajiri wa mpunga kutokana na matokeo wanayoyapata wakitisha wapinzani wao wakiwamo Yanga waliowafunga na kuweka rekodi ya kuwa timu pekee kufanya hivyo katika Ligi Kuu.
Lakini ieleweke licha ya juhudi za wachezaji wote uwanjani, ila usajili wa kiungo mshambuliaji mpya, Yacouba Sogne umezaa matunda zaidi.
Tangu atue Ihefu kiungo huyo amekuwa na kiwango bora akiisaidia kuvuna pointi nne na kuivusha kutinga robo fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC).
Yacouba aliyetemwa Yanga dirisha dogo amekuwa lulu huko Ihefu kwani katika mechi tatu alizocheza amehusika kwenye matokeo kwa kuwa kama hakufunga alitoa asisti.
Nyota huyo ambaye alitambulishwa nchini na Yanga misimu miwili iliyopita akitokea Asante Kotoko, alikuwa na mwendelezo mzuri kwenye kikosi hicho licha ya kutemwa baada ya kuwa nje kwa muda mrefu kutokana na majeraha ya goti.
MABAO, ASISTI, TUZO JUU
Raia huyo wa Bukina Faso katika michezo miwili aliyocheza ya Ligi Kuu amefunga mabao mawili. Alianza dhidi ya Singida BS katika mchezo wa sare 1-1 kisha dhidi ya Dodoma Jiji kwenye ushindi wa 2-1.
Yacouba hakuishia kufunga kwani alitengeneza bao lingine lililofungwa na Nelson Okwa na kuendelea kuwa msaada kikosini hadi kutwaa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Februari.
Kama haitoshi nyota huyo mwenye mbio na akili nyingi uwanjani, hakuishia hapo kwani katika mchezo wa Kombe la Shirikisho la Azam alihusika kwenye mabao yote mawili.
Bao la kwanza la mkwaju wa penalti lililofungwa na Andrew Simchimba, ilitokana na kiungo huyo kuangushwa ndani ya eneo la hatari.
Kama haitoshi Yacouba alitoa asisti tena kwa Simchimba katika mchezo huo.
Wakati akiwa na majeraha, mara kwa mara Yacouba alikuwa akikaa katika benchi la Yanga hadi alipoenda kufufukia tena kwenye Kombe la Mapinduzi.
Yacouba alijikuta nje ya Yanga kutokana na klabu hiyo kubanwa na kanuni kutokana idadi ya wachezaji wa kigeni kuzidi 12 ndipo timu hiyo ya Jangwani ikakata jina lake.
BADO ANA NAFASI YANGA
Kutokana na kasi ya nyota huyo ni kama anawajibu Yanga waliomtema kwamba bado ana uwezo wa kukipiga popote na timu ikanufaika naye ndani ya uwanja.
Labda kwa vile alikuwa na majeraha au idadi ya wachezaji wa kigeni kuzidi pale Yanga lakini kwa kiwango anachokionyesha akiwa Ihefu na ukiiangalia Yanga ya sasa, bado Yacouba anayo nafasi ndani ya kikosi hicho.
Hadi sasa Yanga inalia kwa kukosa winga mwenye makali. Mchezaji ambaye yuko katika lawama kubwa kwa mashabiki wa klabu hiyo kwa sasa ni Mkongomani, Tuisila Kisinda.
Kwa kazi anayoifanya Kisinda pale Jangwani ukimlinganisha na Yacouba utakuwa katili ukisema Mbukinabe huyo wa sasa hawezi kuitumikia timu hiyo.
Ni lazima viongozi wa Yanga watakuwa wakijiuliza mara mbili katika uamuzi walioufanya.
Zipo taarifa zinazosema Kocha Nasreddine Nabi humwambii kitu juu ya uwezo wa Yacouba akiamini bado ni kiungo mwenye ubora.
AMEWAACHA WENZAKE
Kitu tofauti ambacho Yacouba anajitofautisha na viungo wengi washambuliaji ni ubora wake wa kukimbia na kuingia ndani ya eneo la hatari la wapinzani. Mawinga wengi wamekuwa wakikosa kitu cha namna hii.
Yacouba pia anajua kufunga ana utulivu anapoingia ndani ya eneo la hatari na kama atakutana na ugumu ni rahisi kutoa pasi ya bao na hiki ndicho anachokiofanya pale Ihefu.
KOCHA AFICHUA
Yacouba alianza kibarua chake sambamba na Kocha wa Ihefu, John Simkoko akisaidiana na Zubery Katwila.
Ikiwa ni mechi ya kwanza ya kocha huyo, Yacouba alitokea benchi na kwenda kusawazisha bao dhidi ya Singida Big Stars.
Simkoko anasema mchezaji yeyote akiaminiwa anaweza kufanya vizuri na Yacouba ameonyesha anaweza kufanya.
Anasema hakuna cha ziada zaidi kilichoongezwa na benchi la ufundi isipokuwa kufuata maelekezo kama ilivyo kwa wachezaji wengine na Ihefu kila mtu anaweza kufanya makubwa.
“Ameonyesha umuhimu, anaweza na amekuwa na mwenendo mzuri tangu aanze kazi. Kitu kikubwa anajitambua na kufuata anachoelekezwa.
“Kila aliyesajiliwa kikosini ana jukumu la kuitumikia timu na kuipa kile kinachohitajika. Anayepata nafasi lazima aonyeshe kitu ndicho anachofanya Yacouba kuendana na falasafa,” anasema kocha huyo.
Simkoko anasema kwa mwenendo alioanza nao Yacouba na ushirikiano na wenzake kila upande utanufaika.