Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yacouba, Okwa, Akpan waishuhudia Ihefu ikiua Sokoine

Ihefun Opic Yacouba, Okwa, Akpan waishuhudia Ihefu ikiua Sokoine

Sat, 21 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kwa mara ya kwanza wachezaji Victor Akpan, Nelson Okwa na Yacouba Sogne wameishuhudia timu yao mpya ya Ihefu leo ikiibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Tanzania Prisons.

Nyota hao wamejiunga na timu hiyo kuitumikia katika dirisha dogo lililofungwa hivi karibuni wakitokea katika klabu za Simba na Yanga.

Akpan na Okwa wamesajiliwa kwa mkopo wakitokea Simba huku Yacouba akitokea Yanga akisaini kandarasi ya miezi sita kukiwa na kipengele cha kuongeza mkataba iwapo timu hiyo itabaki Ligi Kuu msimu ujao.

Katika mchezo huo Ihefu ilitangulia kupata bao dakika ya pili kufuatia beki wa Prisons, Ezekiel Mwashilindi kujifunga wakati akiokoa hatari na bao hilo kudumu hadi mapumziko.

Prisons ilisawazisha bao hilo kupitia kwa kinara wa mabao, Jeremiah Juma (amefikisha matano) kwa penalti baada ya Kipa wa Ihefu, Fikirini Bakari kumkwatua Meshach Seleman.

Mchezaji wa Ihefu, Daud Raphael alifunga bao la pili dakika ya 90 na kuipatia timu yake pointi tatu ambazo zinaipandisha hadi nafasi ya 10 kwa alama 23.

Wakiwa uwanjani hapo, mastaa hao walikaa sehemu moja wakifuatilia mchezo huo na baada ya mechi walipongezana na mabosi wao.

Hata hivyo, hadi sasa Ihefu haijamtamburisha rasmi Yacouba, huku Okwa na Akpan wakiwekwa wazi na chama hilo la wilayani Mbarali mkoani Mbeya.

Kocha mkuu wa timu hiyo, Zuberi Katwila alisema usajili mpya umeanza kuwalipa na kudokeza mastaa ambao hawajatumika bado wanaendelea kumakilisha taratibu.

"Tunashukuru usajili umeanza kuzaa matunda japokuwa bado kuna wengine hawajaanza kucheza kutokana na kutokamilika kwa utaratibu," alisema Katwila.

Chanzo: Mwanaspoti