Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ya Yusuf Kagoma, akili yetu imegoma kufikiria zaidi

Edo Kagoma Ya Yusuf Kagoma, akili yetu imegoma kufikiria zaidi

Tue, 10 Sep 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Usimlaumu sana Yusuf Kagoma. Ilianza zamani. Miaka hiyo hadi sasa. Wachezaji kusajili timu mbili kubwa nchini, Simba na Yanga. Zamani ilichekesha kidogo. Wachezaji walikuwa wanasaini fomu. Nitakusimulia kitu.

Fomu moja ilikuwa na wachezaji 25. Kulikuwa na sehemu ya jina halafu sehemu ya kuweka saini. Basi. Hakukuwa na mkataba. Klabu ilikuwa inapewa fomu ya usajili na Chama cha Soka Tanzania (FAT). Siku hizi tunaita Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). Kila mchezaji ambaye alikuwa anatakiwa na klabu alikuwa hasaini mkataba. Alikuwa anaweka saini katika sehemu ya jina lake.

Kuna wachezaji wengi nawakumbuka waliwahi kuweka saini katika fomu za timu zote mbili. Kina Mohammed Mwameja, Idephonce Amlima, Kenneth Mkapa na wengineo kibao.

Kichekesho kilikuja kabla ya ligi kuanza ambapo wakati mwingine kutafuta suluhu ya kumaliza jambo lenyewe mchezaji aliambiwa achague timu ambayo angependa kuchezea.

Haikutokea sana mchezaji kufungiwa. Nadhani tulianza kudekeza wachezaji na tumeendelea kufanya hivi mpaka leo katika zama za mikataba.

Jaribu kufikiria namna ambavyo mchezaji anapewa mkataba wenye vipengele kadhaa. Na siku hizi wachezaji wana wasimamizi wao.

Hata hivyo mchezaji anaamua kusaini mikataba miwili. Ni kama ilivyotokea kwa Kagoma. Kwanini inatokea hivi? Kwanza ni tamaa ya pesa ya mchezaji mwenyewe. Lakini pia inatokea kwa sababu klabu ya pili huwa inamwambia mchezaji asaini mkataba huku wakimuahidi kwamba watamalizana na klabu ya kwanza.

Wakati wakimuahidi hivi, pesa ambao wanakuwa wameweka mezani inakuwa kubwa kuliko ile ambayo iliwekwa na klabu ya kwanza. Hapa ndipo wachezaji wanapoingia tamaa zaidi na kujuta ni kwanini walisaini mkataba katika klabu ya kwanza.

Katika suala la Kagoma kwanza namlaumu Kagoma mwenyewe kama ilivyo ada kwa wachezaji wetu. Hauwezi kusikia mchezaji wa kigeni amesaini mikataba miwili. Wanajua wanachofanya. Wanajua maana ya mikataba.

Masakata mengi ya wachezaji wa kigeni ambayo yamesisimua nchi ni yale ambayo yanahusisha kuhama kutoka kwa mtani mmoja kwenda kwa mtani mwingine. Ni kama ilivyotokea kwa Bernard Morrison na Clatous Chama.

Masuala ya kuvurunda kwa usajili yapo kwa wachezaji wazawa. Tazama tu katika dirisha hili. Kulikuwa na masakata ya Lameck Lawi, Awesu Awesu na hili la Kagoma. Wote hawa ni wazawa. Tumezoea kuona wakifanya mambo ya kitoto.

Upande mwingine wa sakata hili nawalaumu Simba ni kwa sababu walimpa mkataba baada ya Yanga kufanya hivyo. Nawalaumu kwa sababu za kisoka zaidi. Simba walipaswa kupiga hesabu mapema kuhusu usajili.

Binafsi naamini walikuwa na sababu zote za kumtaka Kagoma kabla ya Yanga. Hii ni kwa sababu Kagoma ni fundi hasa. Nilishuhudia ubora wake akiwa na Singida Big Stars. Katika lile eneo la kiungo ambalo lilikuwa na mastaa wengi bado Kagoma aliungana na Mbrazili Bruno kuviteketeza viungo vya timu pinzani.

Kagoma alikuwa mchezaji wa timu kubwa. Simba walipaswa kumuweka katika mipango yao hasa ukizingatia kwamba wao ndio ambao walipaswa kujenga timu zaidi kuliko watani wao ambao wameonekana kutimia katika idara zote hasa eneo la kiungo ambalo lina Khalid Aucho, Mudathir Yahya, Jonas Mkude na Salum Abuubakar ‘Sure Boy’.

Kulikuwa na kila sababu za kuachana na Babacar Sarr ambaye alionekana mzito uwanjani. Ni wazi pia Sadio Kanoute alionekana kuwa kiungo mvunja kuni zaidi na asingewasaidia zaidi ya vile ambavyo amefanya.

Kwanini Simba hawakumalizana na Kagoma mapema kabla ya Yanga? Hili ni tatizo kubwa kwa timu zetu. Kagoma yupo hapahapa nchini na uwezo wake unajulikana. Ni mchezaji ambaye angeweza kuisaidia Simba zaidi kuliko Yanga. Kwanini Simba haikumalizana naye mapema? Hata kinachoendelea kwa sasa ni Yanga kumkomkoa mtani wake. Taarifa za ndani katika sakata hili ni kwamba Yanga hawana mpango wa Kagoma. Wanajua kwamba wamesheheni katika eneo la kiungo ambalo kwa sasa ameongezeka na Duke Abuya.

Kinachoendelea kwa sasa ni Yanga kuwahakikishia mashabiki wake kwamba ni kweli walimsaini Kagoma. Lakini taarifa nyingine ambazo ninazo ni kwamba mabosi wa Yanga waliudhiwa na kauli za Ahmed Ally, msemaji wa Simba kuwatambia kuhusu Kagoma kwamba hawana ubavu wa kumpata.

Na katika hili hili nasikia kwamba Yanga wanataka Kagoma ajitokeze hadharani akiri kwamba alisaini kwao na awaombe wamuache aende Simba. Basi. Hapo wanaamini kwamba utakuwa ushindi kwao. Kagoma hajafanya hivyo.

Hatujui mwisho wa sakata zima lakini ninachofahamu ni kwamba hili halitakuwa sakata la mwisho kwa wachezaji wazawa. Wakati mwingine hawajui wanachofanya. Ukizungumza nao tu unagundua kwamba uwezo wao wa kufikiri mambo ya nje ya uwanja ni tofauti kabisa na uwezo wa kucheza soka. Vitu viwili tofauti.

Hata hivyo, hili nalo litapita kwa kile kinachoitwa busara kutumika. Atatokea waziri fulani ataomba busara itumike. Atatokea mkubwa fulani ataomba busara itumike. Kupitia suala hili la busara wachezaji huwa hawajifunzi kitu.

Mwingine atafanya hivi msimu ujao akiamini kwamba busara itatumika na ataendelea kucheza soka. Kuna kauli ambayo ni maarufu miongoni mwa wachezaji kwamba ‘Simba na Yanga huwa hazishindwi kitu’. Kauli zimelemaza wachezaji wetu.

Kama hatutachukua hatua madhubuti hali hii itaendelea mpaka mwisho wa dunia. Kina Ken Mkapa walikuwa hawaogopi fomu. Ilikuwa kitu rahisi kwao kuweka saini mbele ya jina. Leo wachezaji wetu hawaogopi mikataba. Ni kwamba sababu ya neno ‘busara kutumika’. Hawa kina Lawi na Kagoma wote wanapaswa kufungiwa. Labda linaweza kuwa fundisho kwa wachezaji wetu wazawa.

Chanzo: Mwanaspoti