Kwamba Fiston Kalala Mayele anaondoka Yanga kwa dau kubwa la pesa lilikuwa suala la muda tu. Ni hadithi ya samaki mkubwa kumla samaki mdogo. Ni kama chakula zaidi kuliko kudai kuwa ni uonevu. Ndivyo dunia ya kibabe ya soka ilivyo.
Yanga inawauma. Hata kama wanapata pesa nyingi, lakini lazima iwaume. Naambiwa kwamba Wamisri - Pyramids wameweka zaidi ya Sh2 bilioni kwa Mayele. Nilitazamia hili. Waarabu waliokuwa wanamtaka Mayele hawajatazama sana rekodi ya mabao ya Mayele hapa nchini.
Wametazama zaidi mabao saba ambayo ameyafunga katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika. Inawezekana tukawa na ligi dhaifu kiasi kwamba Mayele amefunga mabao zaidi ya 16 kwa kila msimu katika misimu miwili aliyocheza Tanzania. Hilo hawajatazama sana.
Walichotazama ni mabao saba ambayo amefunga katika michuano ya Shirikisho na kuwa mfungaji bora. Achilia mbali mabao aliyowafunga Zalan pale Temeke ambayo hayahesabiki katika mbio hizi. Mabao saba ya kuwa mfungaji bora katika Shirikisho yasingewaacha Yanga salama.
Lakini zaidi ni namna ambavyo alikuwa anafunga mabao yenyewe. Mayele alikuwa anafunga mabao magumu hasa. Mabao machache ambayo yamefunga yalikuwa yanaonekana rahisi, lakini mengine mengi ameyafunga katika mazingira magumu.
Achilia mbali hilo kuna baadhi ya vitu vichache nje ya mabao ambavyo wametazama na wakaona inatosha. Sidhani kama imewahi kutokea ‘asisti’ nzuri katika michuano ya CAF msimu ulioisha kama pasi yake aliyompasia Kennedy Musonda katika pambano dhidi ya Marumo Gallants pale Rustenburg.
Kitu cha kukumbuka zaidi ni kwamba timu zetu mpaka sasa zipo katika nafasi ya kulisha wakubwa. Wazungu huwa wanatuita ‘feeder clubs’. Kwamba sokoni sisi ni watu wa kunyanyaswa na Wamisri, Wamorocco, Watunisia na mataifa mengine ambayo kiuchumi yapo mbele yetu na yana uwezo mkubwa wa kuwekeza katika soka.
Hizi timu zetu ni kubwa hapa ndani au Afrika Mashariki, lakini linapofika suala la Pyramids, Zamalek, Waydad Casablanca, Al Ahly na wakubwa wengineo kumtaka mchezaji wako bora lazima wakuonyeshe ukubwa wao. Lazima wakuonyeshe kwamba wao ni samaki wakubwa.
Kwa mfano, mbavu za wakubwa haziishi katika dau la pesa ambalo wanamtaka mchezaji mwenyewe. Hapana. Hili unaweza kukataa. Na unaweza kukataa kiasi kwamba mashabiki na wanachama wakakubali kwa sababu wanampenda mchezaji mwenyewe kuliko pesa.
Hautapata presha kubwa ya kumuuza mchezaji kutoka kwa mashabiki. Hata kwa Ulaya hali ipo hivi hivi. Ukubwa wa hawa unakuja pale mchezaji mwenyewe anapokuonyesha kiasi cha pesa ambacho atakwenda kulipwa kama akiuzwa.
Kama Mayele alikuwa analipwa Sh 17 milioni na Yanga, halafu Pyramids wameahidi kumlipa kiasi cha Sh70 milioni kwa mwezi. Akikuwekea ofa aliyonayo mezani lazima kibinadamu unyooshe mikono juu na kumruhusu aondoke.
Njia pekee ambayo unaweza kumzuia mchezaji asiondoke kwanza ni kukataa dau lililoletwa mezani na Pyramids, lakini pia kuahidi kumlipa Mayele mshahara ambao atakwenda kulipwa huko Misri. Hili la pili ni gumu zaidi. Utatanua goli katika hesabu zako za mishahara ya wachezaji na wafanyakazi.
Kufikia hapo hauwezi kukaa na mchezaji wa aina ya Mayele. Kitu ambacho ni kigumu zaidi kwa sasa ni kwamba dunia inakabiliwa na uhaba wa wafungaji. Hata Yanga wenyewe wamekuwa wakijiuliza kuhusu nani anaweza kuwa mbadala halisi wa Mayele.
Sidhani kama kuna mchezaji ambaye wanaweza kumchukua kwa sasa na akawa Mayele. Wanachoweza ni kuendelea kufunga mabao mengi ambayo yatachukua nafasi ya mabao ya Mayele. Hivi ndivyo inavyotokea kwa mchezaji mkubwa akiondoka.
Kunaweza kuwa na kipindi cha mpito kuelekea kumpata Mayele mwingine. Hakuna mchezaji ambaye pengo lake halizibiki. Kabla ya Mayele, Yanga wamewahi kuwa na kina Mohamed Hussein, Amissi Tambwe, Boniface Ambani na wafungaji wengi wa kariba yake.
Lakini kuna wakati huwa kinatokea kipindi cha mpito kabla ya kumnasa mshambuliaji ambaye atavaa viatu vyake katika usawa uleule. Mkiwa na bahati inaweza kuchukua muda mfupi, lakini mkiwa hamna bahati inaweza kuchukua muda mrefu.
Kwa Mayele mwenyewe huu ni mfano mzuri kwa wachezaji wetu wa wazawa waone kile ambacho kinaweza kufanywa na mpitanjia. Amekuja ametengeneza jina ameondoka zake akiwa anaelekea katika mshahara mkubwa.
Majuzi niliandika katika ukurasa huuhuu kwamba nilitegemea Yanga watapokea ofa kutoka katika klabu kubwa zaidi. lingebaki suala la Mayele mwenyewe kuendelea kupata sifa hapa nchini au kujaribu maisha mengine nje ya nchi yetu.
Naambiwa kwamba yeye na mke wake ni mashabiki wakubwa wa maisha ya Kitanzania, lakini hakukuwa na jinsi. Ameamua kuchukua nafasi ya kwenda kufuata mshahara mkubwa nje ya nchi. Umri wake umesogea na inawezekana hili likawa dau kubwa la mwisho katika maisha yake ya soka.
Mmoja kati ya wachezaji wa kizawa ambao waliwahi kuchukua nafasi hii ni Mbwana Samatta wakati alipokwenda TP Mazembe. Lakini pia tusisahau kwamba Simon Msuva naye alichukua nafasi yake kwenda Difaa Jadida ya Morocco.
Pamoja na Mayele kuondoka kitu ambacho nakifahamu ni kwamba jina lake halitafutika tena katika siasa zetu. Endapo atakuwa na msimu mmoja tu mbaya pale Misri basi atahusishwa kurudi nchini. Atahusishwa kurudi Yanga au kwa watani zao Simba.
Ni kama ilivyokuwa kwa Luis Miquissone. Ni kama ilivyokuwa kwa Clatous Chama wakati alipokwenda Morocco. Zamani ni kama ilivyokuwa kwa Emmanuel Okwi. Mayele lazima atahusishwa na siasa za soka letu mpaka tutachoka. Ndivyo maisha ya soka letu yalivyo.
Kwa sasa ni muda wa kumtakia kila la heri huko anakokwenda. Ameonyesha ubora mkubwa na zaidi ya kila kitu alikuwa mfano katika jamii. Hakuwa mkorofi, alikuwa muungwana na mcha Mungu.
Ingawa alikuwa staa mkubwa lakini hakuwa na maringo. Bahati mbaya kwetu ni kwamba samaki mkubwa amemla samaki mdogo.
Kama ambavyo Simba na Yanga wamezoea kuzionea Coastal Union, Polisi Tanzania, Singida Fontain Gate na wengineo, basi ni kama ambavyo na wao wameingia katika mtego wa wakubwa kutoka Afrika Kaskazini.
Huu ni ukweli ambao utatuandama kwa muda mrefu na sioni hali hii ikifutika hivi karibuni kwa sababu wenzetu wana pesa ndefu. Hiki wanachotoa kwa Mayele ni kwa mchezaji mmoja tu lakini kumbuka karibu timu nzima pamoja na benchi la ufundi wanalipwa hivi au wamenunuliwa hivi.