Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ya Lameck Lawi yanaendelea Tanzania tu

Lawi Msz Lameck Lawi.

Mon, 24 Jun 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kwamba mchezaji ametangazwa rasmi na klabu yake mpya halafu klabu yake ya zamani inatangaza kwamba mchezaji husika bado ni mchezaji wao, huwa inatokea Tanzania tu. Na imetokea kwa beki wa soka anayeitwa Lameck Lawi.

Nashindwa kumtambulisha kama ni staa mpya wa Simba au staa wa zamani wa Coastal Union. Ni jambo la aibu katika mpira wetu. Hili ni jingine badala ya lile la mchezaji kusaini mikataba miwili ya timu mbili tofauti. Mambo ya aibu ambayo yanashusha hadhi ya soka letu.

Nini kimetokea kwa Lawi? Nasikia yeye binafsi alishafikia makubaliano na Simba. Hapo hapo Coastal walishafikia makubaliano na Simba. Ilibaki suala la Coastal kuingiziwa kiasi cha fedha kwa ajili ya kukamilisha uhamisho huo. Hapo katikati kuna mambo mengi yalikuja kutokea.

Simba walikuwa wanajipanga mapema kwa uhamisho wa wachezaji wa msimu ujao kabla hata msimu huu ulioisha haujaisha. Wakamuona Lameck kama vile ni mchezaji ambaye atawasaidia. Ghafla katika mwendo huo huo Coastal wakafuzu kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika. Nadhani hapo ndipo mawazo yao yalipoanza kubadilika.

Waliweka mtego mdogo tu kwamba Simba wasitimize baadhi ya masharti ili waliruke dili zima. Simba walilazimika kwenda mbio kutimiza mambo mawili. Kwanza kumuwekea mchezaji mkwanja wake kwa wakati lakini pia kuilipa Coastal kwa wakati. Naambiwa kwamba Simba hawakutimiza hayo kwa wakati. Coastal wanajaribu kutumia mwanya huo huo kumbakisha Lawi.

Coastal wamerudisha pesa katika akaunti ya Simba. Sijui kama Lawi mwenyewe amerudisha au vipi lakini inatuachia maswali ya msingi kuhusu mustakali wa soka letu katika masuala ya uhamisho wa wachezaji. Ni wazi kwamba kuna kitu hakipo sawa katika weledi wetu kwa sababu migogoro hii hutokea kila msimu.

Mambo mawili kwa kila timu. Kwanza ni kwa Coastal wenyewe. Kwa nini wabadilishe msimamo wa kibiashara kwa sababu ya kufuzu kwenda Shirikisho? Biashara inabakia kuwa biashara bila ya kujali mabadiliko ya ghafla ya nafasi yao katika msimamo. Makubaliano ya kibiashara yalipaswa kusimama pale pale.

Uamuzi wa Coastal kutomuuza Lawi ulipaswa kufanyika kabla hajawafikia makubaliano na Simba. Suala la kukiuka makubaliano baada ya kufuzu sio uungwana. Labda kama wangeweka makubaliano maalumu kwamba biashara ingeweza kubadilika kama wangefuzu katika michuano ya kimataifa.

Lakini naweza kuthibitisha kwamba ghafla Coastal wakapokea ofa kutoka katika timu moja ya Ubelgiji. Kwamba dau ambalo wangepata katika dili hilo ni kubwa kuliko la Simba. Kwamba hata Lawi angepokea mshahara mkubwa kuliko ule anaopokea Aziz Ki Yanga. Angelipwa euro 8,000 kwa mwezi. Hata hivyo, unajiuliza, hilo linawahusu nini Simba?

Simba walipeleka dili lao wakakubaliwa. Mambo ya Ubelgiji yanawahusu nini? Wao walikuwa wameiwahi biashara mapema. Bahati yao. Timu ya Ubelgiji haikuwahusu chochote. Labda tu kama wangeamua kuwa waungwana kwa kumruhusu Lawi aende huko na wao wapate chochote kutoka katika biashara hiyo kwa makubaliano maalumu na Coastal.

Naambiwa pia kwamba baadaye viongozi wa Coastal walipatwa na wasiwasi usiowahusu. Kwamba Simba ilikuwa imepanga kusajili beki mwingine wa kati wa nje. Hii ingepelekea Lawi kupata nafasi finyu ya kucheza katika kikosi cha kwanza wakati huu Taifa likianza kumtegemea katika kikosi cha kwanza cha timu ya taifa.

Lakini hapo hapo tunaweza kuhoji weledi wa Simba katika masuala ya mikataba. Kwa nini wasilipe kwa wakati? Wanawakoroga mashabiki wao kuhusu mikakati yao ya usajili katika miaka ya karibu. Wamewakosa wachezaji wengi wazuri kwa kushindwa mikakati midogo kama hii. Fikiria namna ambavyo mashabiki watachukia kama Lawi akiishia kutokuwa mchezaji wao hasa baada ya kutangazwa kuwa mchezaji wa kwanza kutua klabuni hapo.

Naambiwa Simba walilazimika kumtangaza Lawi kwa haraka kwa sababu ya mgogoro huu wa chini chini ambao ulifukuta bila ya mashabiki kujua kilichokuwa kinaendelea. Kwa nini kuwa na mgogoro na kuviziana juu ya mchezaji ambaye tayari ana mkataba na klabu yake? Walipaswa kukaa mezani na Coastal na kumaliza jambo lenyewe kwa busara zaidi kuliko kutunushiana mabavu.

Vyovyote ilivyo tayari Lawi ana mikataba miwili. Ule alionao Coastal na huo mpya wa Simba. Ni mgogoro tayari. Nani atatoa barua ya kumruhusu (release letter) kwa ajili ya kwenda kucheza Simba. Coastal bado wameshika mpini na Simba imeshika makali. Lawi mwenyewe atataka kwenda wapi? Vipi aking’ang’ania kwenda Simba wakati Coastal hawataki?

Lakini hapo hapo kuna taswira mbaya inakwenda kutokea. Coastal ina watu wengi walioushika mpira wetu kwa sasa. Tunaanza na Rais wa TFF mwenyewe, Wallace Karia. Lakini Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Steven Mnguto ni Bosi wa Coastal. Hii ni achilia na watu wengine kina Said Soud. Katika hili kunaweza kutokea mgongano wa maslahi (conflict of interest).

Wakae chini tu na kumaliza. Kama ningekuwa kiongozi wa Coastal ningetumia nafasi hii kumpata Kennedy Juma ambaye uwezo wake sioni kama una tofauti kubwa na Lawi. Na hapa unajumlisha ukweli kwamba Kennedy ana uzoefu mkubwa wa mechi za kimataifa. Tusubiri tuone hawa wakubwa watafikia wapi.

Hii ni kesi mpya katika soka letu baada ya zile za mchezaji kusaini mikataba ya timu mbili. Hata hivyo, rafiki zetu wa Simba na Coastal huwa mabifu yao. Wanajuana. Tangu wakati ule wa Abdi Banda. Mara nyingi wanapenda kutunishiana misuli. Wakati mwingine bila ya sababu za msingi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live