Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

YES! ZAHERA....Ndio basi tena

34182 Pic+yes Tanzania Web Photo

Tue, 1 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

KABLA Ligi Kuu Bara haijaanza msimu huu, mashabiki wa Yanga walikuwa kwenye stresi kubwa. Hii ni kwa vile chama lao lilivyomaliza msimu uliopita kinyonge.

Yanga ilipasuka mechi nyingi za kufungia msimu na kupoteza dira za mbio zao za kutetea taji kwa msimu wa nne mfululizo na kujikuta wakiliachia taji kwa watani zao wa Msimbazi.

Hata hivyo, kazi kubwa iliyofanywa na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mwinyi Zahera imewafanya mashabiki hao kurejesha afya zao, kwani stresi zote kwa sasa kwishnei.

Mtihani kwa sasa upo kwa mashabiki wa Simba ambao kila wakichungulia kasi ya watani zao, wanajikuta wakiishiwa pozi kwa pengo la alama 17 limewatenganisha mbali, japo timu yao ina michezo viporo vinne.

Shabiki gani wa Yanga anayeweza kuwa na stresi wakati chama lao limemaliza mwaka 2018 likiwa kileleni, huku wakiandika rekodi kadhaa za kusisimua ambazo kabla hazikuwepo Bara?

Ndio, Zahera ni kama ameshindikana kwa sasa katika ligi hiyo kwa namna alivyowaburuza wapinzani wake, huku akiendelea kusisitiza kuwa, huo ni mwanzo tu na mpaka msimu utakapofikia mwishoni atakuwa ameandikisha rekodi itakayochukua muda kufutika.

Akiwa ameiongoza Yanga katika mechi 18 akikusanya alama 50 kabla ya duru la kwanza kukamilisha kimemfanya kocha huyo Mkongo kuandika rekodi ambayo haijawahi kuandikwa tangu kuanza kwa Ligi ya soka Tanzania mnamo mwaka 1965.

Idadi hiyo ya pointi ni kubwa zaidi kuwahi kufikiwa na timu katika mzunguko wa kwanza kwani awali pointi nyingi ambazo zilikusanywa na timu katika nusu ya kwanza ya ligi zilikuwa ni 39 ambazo Yanga ilikuwa nazo katika msimu wa 2015/2016.

Ikumbukwe kabla ya mechi dhidi ya Mbeya City, Zahera tayari alishaweka rekodi tano kali ambazo hazijawahi kufikiwa na makocha wengine ambapo ya kwanza ni ile ya kukusanya idadi kubwa ya pointi katika michezo 15 ya mzunguko wa kwanza na ile ya timu kufunga bao katika idadi kubwa ya michezo ya mzunguko wa kwanza.

Katika msimu huu wa ligi, hadi sasa Yanga imefunga bao katika michezo 17 kati ya 18 iliyocheza na ni mmoja tu dhidi ya Simba ulioisha bila kikosi chake kutupia kambani.

Pia Yanga ndio timu ambayo imekusanya pointi nyingi ugenini msimu huu ambapo imevuna jumla ya pointi 19 katika michezo saba, ikishinda sita na kutoka sare mmoja, ikifunga mabao 11 na kufungwa mabao manne.

Mbali na hilo pia Yanga iliyoshinda idadi kubwa ya mechi za mzunguko wa kwanza ambazo ni 16 huku ikitoka sare michezo miwili tu.

Lakini wakati Zahera akitambia rekodi hizo tano, huenda akaweka rekodi mpya kuwa kocha aliyeiongoza timu kukusanya idadi kubwa ya pointi katika msimu mmoja wa ligi na kuvunja rekodi iliyowahi kuwekwa na Hans Pluijm msimu wa 2015/2016.

Katika msimu huo wa 2015/2016, Pluijm aliiongoza Yanga kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ikiwa na jumla ya pointi 73 ambazo sasa huenda zikafikiwa na kuvunjwa kirahisi na Zahera na kikosi chake cha msimu huu.

Kwa jumla ya pointi 50 walizokusanya hadi sasa, Zahera sasa anapaswa kuiongoza Yanga kuibuka na ushindi kwenye michezo nane tu kati ya 20 waliyobakiza ili kufikisha pointi 74 ambazo zitakuwa ni moja zaidi ya zile zilizofikiwa na Pluijm na kikosi chake 2015/2016.

Huenda Zahera akamudu kuvunja rekodi hiyo ya Pluijm na kuweka yake mpya kwanimechi za msimu huu ni nyingine kuliko msimu uliopita, pia ameonekana kukibadilisha akikijenga kikosi chake kucheza kitimu na kwa kulidhihirisha hilo, timu hiyo imekuwa haitegemei mchezaji mmoja mmoja katika kufumania nyavu.

Tofauti na timu nyingine, jumla ya wachezaji 11 wa Yanga wameshiriki katika kuifungia timu hiyo mabao 35, ambao ni mabeki, Kelvin Yondani, Andrew Vincent na Abdallah Shaibu, viungo Feisal Salum, Rafael Daud, Jaffary Mohammed, Ibrahim Ajibu na Deus Kaseke pamoja na washambuliaji Mrisho Ngassa na Heritier Makambo.

MSIKIE MWENYEWE

Kocha huyo amezungumzia pengo la pointi lililopo baina yake na watani zao wa Yanga, Simba na kudai wajipange kwelikweli kwani amini kama alala 17 walizonazo zitafikiwa kirahisi na wapinzani wao, japo anakiri bado habweteki na mafanikio hayo.

“Ligi ni ngumu na nashukuru vijana wangu wameendelea kuwapa raha mashabiki wa Yanga na sioni kama Simba wataweza kuziba pengo lililopo la pointi, hata hivyo tutaendelea kujipanga kusudi kupate matokeo mazuri kwa mechi zetu hasa za duru ya pili,” alisema.

Yanga imesaliwa na mchezo mmoja wa kukamilisha duru la kwanza dhidi ya Azam na kama watapata ushindi watafikisha alama 53, lakini wataandika rekodi ya kuzifunga 16, huku wakichemsha dhidi ya Simba na Ndanda waliotoka nao sare.

Alama walizonazo zinaifanya Simba kuhakikisha inashinda mechi zao zote nne za viporo kwanza ili angalau kupunguza pengo la sasa kwani ina pointi 33 zilizotokana na michezo 14 na kama watashinda ili kulingana michezo na Yanga itafikisha 45 na kusaliwa na deni la alama tano.

Ligi Kuu kwa sasa inasimama kwa muda kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi, inayoanza kesho visiwani Zanzibar, Simba na Yanga wakitarajiwa kutupa karata zao kati ya Januari 3-4.



Chanzo: mwananchi.co.tz