Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Xabi Alonso kuivurugia usajili Liverpool

Alonso Kwatuuuu Xabi Alonso kuivurugia usajili Liverpool

Sat, 22 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Liverpool imepambana sana kujaribu kumnasa Xabi Alonso akarithi mikoba ya Jurgen Klopp, lakini akawakatalia.

Imeona sio kesi, ikatua zake Uholanzi kwenda kunasa huduma ya Arne Slot, ambaye ndiye kocha wao mpya, akitua Anfield kuchukua mikoba ya Mjerumani Klopp.

Wakati ikiamini ishamalizana na mambo ya Alonso, Mhispaniola huyo ambaye aliwahi kucheza kwenye kikosi chao cha Anfield, anataka kuwavuruga zaidi, akiwa na mpango wa kutibua mawindo yao ya mchezaji wanayemsaka na kuhitaji saini yake kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi.

Alonso, ambaye amebaki kwenye kikosi cha Bayer Leverkusen alichokipa ubingwa wa Bundesliga msimu wa 2023-24 bila ya kupoteza mechi hata moja, amechukua uamuzi wa kumpigia simu mchezaji, Waldemar Anton ili akajiunge na mabingwa hao wa Ujerumani kwenye dirisha hili.

Beki huyo, Anton yupo kwenye mipango ya Liverpool ikihitaji saini yake kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi, lakini sasa Alonso anataka kuwatibulia mambo akimtaka staa huyo atue kwenye timu yake, ambayo itacheza kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Anton kwa sasa yupo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Ujerumani kilichopo kwenye fainali za Euro 2024 zinazofanyika kweye ardhi ya kwao na anakipiga katika kikosi cha VfB Stuttgart.

Jambo hilo la Alonso linaweza kumweka kwenye lawama kubwa na mashabiki wa klabu yake hiyo ya zamani ya Liverpool, ambayo alishinda nayo taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2005. Kwa hali ilivyo, Liverpool ipo kwenye hatari ya kukosa huduma ya beki huyo, Anton kwa sababu chaguo la kwanza ambalo anaweza kulifanya ni kubaki kwenye Bundesliga, huku kingine ni kwenda kucheza timu ya Alonso, mabingwa wa ligi hiyo waliocheza msimu mzima bila kupoteza.

Kwa mujibu wa Sky Deutschland, Alonso amempigia simu beki huyo wa kati na kumshawishi akajiunge na timu yake na kuachana na ofa nyingine.

Ripoti zinafichua kwamba Alonso amempigia simu mara mbili Anton, huku ikielezwa amemwandalia dili litakalofika tamati 2028.

Hakuna makubaliano ya mdomo yaliyofikiwa, lakini bei ya Anton ni kati ya Euro 20 milioni na Euro 25 milioni kwa mujibu wa kipengele kilichowekwa kwenye mkataba wake, kitu ambacho kinaweza kulipwa na miamba hiyo ya Ujerumani.

Liverpool ilikuwa ikipewa nafasi kubwa ya kumsajili beki huyo mwenye umri wa miaka 27 baada ya kuona anafaa kwenda kuchukua mikoba ya Joel Matip, aliyefunguliwa mlango wa kutokea mwishoni mwa msimu uliopita baada ya mkataba wake kufika tamati.

Anton ni moja ya wachezaji kadhaa wanaoripotiwa kuwa na mpango wa kuachana na Stuttgart kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi baada ya timu hiyo kumaliza katika nafasi ya pili nyuma ya Leverkusen ya Alonso kwenye Bundesliga msimu uliopita.

Slot amekuwa akikabiliwa na upinzani mkali sana kwenye kusaka saini ya Mjerumani huyo na sasa kocha Alonso anataka kutibua mambo zaidi.

Anton amejumuishwa na kocha Julian Nagelsmann kwenye kikosi cha mastaa 26 wanaoiwakilisha Ujerumani kwenye fainali za Euro na alikaa benchi kwenye mechi ya kwanza ya hatua ya makundi, ambapo timu hiyo iliibuka na ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Scotland.

Kwenye kikosi hicho cha timu ya taifa ya Ujerumani, Anton anashindania namba na mabeki wengine matata kama Antonio Rudiger, Jonathan Tah na Nico Schlotterbeck, ambao wamekuwa wakipewa kipaumbele zaidi na kocha Nagelsmann.

Chanzo: Mwanaspoti