Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wydad yamtimua kocha ikijiandaa kuja Dar

Kocha Mkuu Wa Wydad Casablanca, Adel Ramzi.png Kocha Mkuu wa Wydad Casablanca, Adel Ramzi

Fri, 15 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Timu ya Wydad Casablanca ya Morocco imemtimua kocha mkuu wa kikosi hicho, Adil Ramzi ikiwa ni miezi mitano tangu aanze kuinoa akitokea katika benchi la ufundi la PSV ya Uholanzi alikodumu kwa miaka minne kwenye soka la vijana.

Taarifa iliyotolewa na Wydad kwa mashabiki wake ilieleza: "Ilikuwa furaha bwana. Asante kwa kumbukumbu nzuri na tunakutakia kila la heri katika changamoto yako mpya."

Ramzi akiwa na kikosi hicho msimu huu alikiongoza katika michezo 20 ambapo alishinda 12, sare miwili na kupoteza sita huku katika Ligi Kuu Morocco 'Botola Pro' akikiongoza katika mechi tisa akishinda sita, sare moja na kupoteza mbili.

Mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu Morocco aliiongoza timu hiyo kushinda bao 1-0 mbele ya Union Touraga na kufikisha pointi 19 ikiwa katika nafasi ya nne, lakini ikiwa na michezo miwili mkononi nyuma ya vinara FAR Rabat waliocheza mechi 11 wakiwa na pointi 23.

Wydad iliyopo kundi 'B' na Simba katika Ligi ya Mabingwa Afrika zikitarajiwa kukutana Desemba 19, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ni ya tatu katika msimamo baada ya kushinda mechi moja kati ya tatu wakati ASEC Mimosas ya Ivory Coast ikiongoza na pointi saba.

Simba yenye pointi mbili itahitaji ushindi ili kufufua matumaini katika kundi hilo huku ikiwa na kumbukumbu ya kushinda bao 1-0 mara ya mwisho zilipokutana katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kwenye robo fainali ya michuano hiyo, Aprili 22 mwaka huu.

Hata hivyo, Mnyama alienda kuondolewa na timu hiyo katika mchezo wa marudiano kwa changamoto ya penalti, ugenini nchini Morocco baada ya kufungwa bao 1-0 katika muda wa kawaida kabla ya kugeukia mikwaju hiyo na Simba kufungwa mabao 4-3.

Licha ya kuwa miongoni mwa timu kubwa Afrika, katika siku za karibuni Wydad imekuwa ikihangaika kupata matokeo mazuri uwanjani, jambo ambalo limewafanya mashabiki wake kuendelea kuusakama uongozi wakiutaka kuchukua hatua.

Chanzo: Mwanaspoti