Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wydad huu ni mwaka wao dume

Wydad Mwaka Dumu Wydad huu ni mwaka wao dume

Thu, 14 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Ni mwaka wa taabu. Ndio, inashangaza. Wydad Casablanca ya sasa sio ile. Inapitia magumu nje na ndani ya uwanja. Kwenye msimamo wa Ligi Kuu Morocco, Botola Pro 1, inakamata nafasi ya tano ikiwa na pointi 33 baada ya mechi 21.

Kwenye msimamo huo, AS FAR inaongoza na pointi 55 baada ya mechi 23, hii ina maana Wydad ina mechi mbili mkononi.

Hata hivyo, hata kama Wydad itashinda mechi zote mbili itafikisha pointi 39, bado itakuwa nyuma kwa pointi 16 kwa vinara AS FAR.

Hata matumaini ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao ni madogo achilia mbali ubingwa.

Kama kuna mwaka mbaya kwa Wydad, ni huu. Kwanza imetolewa kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa, haifanyi vizuri kwenye ligi na inapitia hali mbaya ya kiuchumi.

Hapa tumekusogezea safari ya mapito magumu ya timu hii na undani wa matatizo inayoikabili.

KIMATAIFA

Mambo yalianza kuwa magumu kwenye michuano ya African Super League na ilipoteza mchezo wa fainali mbele ya Mamelodi Sundowns.

Licha ya kufika fainali Wydad, haikuwa na kiwango bora na kwenye nusu fainali dhidi ya Esperance ilisubiri hadi mikwaju ya penalti tano kufuzu fainali.

Kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, iliishia hatua ya makundi na ilimaliza nafasi ya tatu ikiwa ni mara ya kwanza kwenye historia ya klabu hiyo na mara zote ambazo ilifuzu robo.

Ilimaliza nafasi ya tatu nyuma ya Simba ambayo ilifungana nayo alama lakini utofauti ulikuwa ni kwenye matokeo pale timu hizi zilipokutana.

UKATA NA MIGOGORO KWENYE TIMU

Kwa sasa Wydad inapiti nyakati ngumu sana kiuchumi, hii kwanza inasababishwa na migogoro iliyopo na kukamatwa kwa rais wao, Said Naciri anayedaiwa ni mmoja ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya.

Taarifa kutoka SNRT News inaripoti, Naciri anakabiliwa na mashtaka mazito yakiwemo uuzaji na usambazaji wa kimataifa wa dawa za kulevya, kughushi nyaraka, utakatishaji fedha na matumizi mabaya ya nafasi zao kwenye serikali pamoja na jamii.

Kigogo huyu ambaye pia ni mbunge wa bunge la Morocco amefunguliwa mashtaka na serikali ya Morocco, desemba mwaka jana.

Mbali ya Nacir pia kuna watu wengine 25 waliokamatwa kwenye sakata hilo na hadi sasa wanashikiliwa kwenye gereza la Oukacha, Casablanca.

Kwa kiasi kikubwa kigogo huyu ndio alikuwa akiipa jeuri ya fedha Wydad, yeye ndio alikuwa akitoa mpunga wa kutosha kuhakikisha timu inasajili na kupata matokeo mazuri kwenye michuano mbalimbali.

Kitendo cha yeye kuanguka, kwanza kumekuwa na migogoro mbalimbali ndani ya timu, pia hata hali ya kujitolea kwa wachezaji inadaiwa kupungua kwa sababu hawapati tena yale mambo waliyokuwa wanayapata wakati Nacir yupo na timu ikiwa pamoja na bonasi kubwa kwenye mechi za kimataifa na ligi na bonasi nyingine pale wanaposhinda kwenye michuano mbalimbali.

MWAKANI WATAKUWEPO?

Inaonekana ni mgumu sana kuwepo kwenye Ligi ya Mabingwa msimu ujao, kwanza kwenye msimamo wa ligi yao timu zinazoenda Ligi ya Mabingwa ni zile zinashika nafasi ya kwanza na ya pili na kwa mwenendo wa Wydad inaonekana ni ngumu kuwafikia Raja na ASFAR ambazo ndio zinashika nafasi hizo, kwa sababu itakuwa na tofauti ya pointi 10 dhidi yao hata kama itashinda viporo vyote.

Ukiondoa, Ligi ya Mabingwa timu ambazo hufuzu kucheza kombe la shirikisho huwa ni mbili na yakwanza ni ile inayomaliza nafasi ya tatu kisha nyingine ni ile inayochukua ubingwa wa Throne Cup ambayo ndio sawa na FA Cup ya hapa Tanzania.

Kwenye msimamo timu inayoshika nafasi ya tatu ni FUS Rabat ambayo ina alama 38, kama Wydad ikishinda viporo itafikisha alama 39, hivyo itaivuka pointi moja lakini hiyo ni hadi itakaposhinda mechi zote.

Nafasi pekee inayoonekana kwao ni kucheza shirikisho mwakani kupitia ligi ama Kombe la Throne.

Chanzo: Mwanaspoti