Gwiji wa Klabu ya Arsenal, lan Wright amesema klabu hiyo itashindana na Manchester City katika mbio za ubingwa endapo itamsajili Mshambuliaji wa Brentford, Ivan Toney katika dirisha dogo la usajili la Januari 2024.
Arsenal ipo nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu ya England ikiwa na Point 20 sawa na na Tottenham Hotspur inayoongoza kwa tofauti na mabao ya kufunga na kufungwa. Mwishoni mwa juma lililopita Arsenal iliifunga Man City 1-0 .
Hiyo ni hatua nzuri kwa Kocha Mikel Arteta kutokana na ushindi huo wa kwanza Ligi Kuu Engand dhidi ya Man City tangu mwaka 2015.
Lakini lan Wright amedai Arsenal inatakiwa kufanya usajili wa Mshambuliaji mpya ambaye ataongeza nguvu katika kikosi na kumpendekeza Toney.
Ameongeza kuwa Arsenal haitafika mbali ikiendelea kumtegemea Eddie Nketiah na Gabriel Jesus ambao sio hatari zaidi wanapokuwa eneo la hatari.
“Tulipoteza mabao mengi na ikatuweka katika nafasi fulani. Nadhani Toney atafaa zaidi kwa sababu ni mchezaji anayejua kufunga.
“Ukiwazungumzia Nketiah na Jesus utarudi nyuma katika mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Tottenham, Jesus alikosa mabao mengi sana, kwa mchezaji mwenye uwezo kama wake maeneo kama yale jitihada inahitajika zaidi.” Amesema lan Wright
Toney ambaye amehusishwa na Arsenal aliifungia Brentford mabao 20 msimu wa 2022-23 lakini anakibiliwa na adhabu ya kufungiwa miezi minane baada ya kukiri kujihusisha na Kamari.
Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa England atarejea Januari kuendelea na maisha yake ya soka.