Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wolves yakomalia bei ya Neto kwa Arsenal, Man City

Pedro Neto Wolves yakomalia bei ya Neto kwa Arsenal, Man City

Wed, 22 May 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Mabosi wa Wolves wapo tayari kumuuza winga wa timu hiyo Pedro Neto katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi lakini haitopunguza hata senti kwenye bei yao ya Pauni 60 milioni waliyoiweka.

Pedro mwenye umri wa miaka 24, huduma yake inawindwa na timu mbalimbali England ikiwemo Manchester City na Newcastle ambazo zote zinaweza kutoa kiasi hicho cha pesa.

Wolves inalazimika kumuuza Neto kwa sababu inataka kupeuka rungu kutoka mamlaka za soka juu ya kukiuka sheria za matumizi ya pesa.

Mbali ya staa huyo, Mbweha hawa pia wamewaweka sokoni Matheus Nunes, Ruben Neves, Raul Jimenez, Nathan Collins na Conor Coady.

Mbali ya kutaka kuepuka adhabu, Wolves inawauza mastaa hao kwa ajili ya kupata pesa ambazo itazitumia kusajilia wachezaji wengine.

Neto ambaye pia anawindwa na Arsenal, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2027. Msimu huu amecheza mechi 24 za michuano yote na kutoa asisti 11.

KATIKA kuhakikisha anasuka upya safu yake ya ulinzi ili kupambana vyema kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa msimu ujao kocha wa Aston Villa Unai Emery amependekeza jina la beki wa Barcelona Ronaldo Araujo, 25, akitaka asajili katika dirisha lijalo.

Araujo ambaye hivi karibuni aliwahi kuhusishwa na Bayern Munich, ni mmoja kati ya mastaa tegemeo wa Barca na msimu huu amecheza mechi 37 za michuano yote.

KOCHA wa Arsenal anaripotiwa kuwaambia mabosi wa timu hiyo kwamba anataka kusajili straika kabla ya kwenda kuanza maandalizi ya msimu ambapo ripoti zinadai aliyemuweka namba moja kwenye orodha yake ni Alexander Isak, lakini kama itashindikana kumpata mchezaji mwingine anayehitaji asajiliwe ni Brian Brobbey kutoka Ajax.

ASTON Villa ipo katika hatua nzuri kumsajili kiungo wa Luton Town na England Ross Barkley katika dirisha lijalo.

Staa huyu mwenye umri wa miaka 30, aliwahi kuichezea Villa kwa mkopo wa msimu mmoja miaka minne iliyopita lakini wababe hawa wa Birmingham hawakushawishika kumsainisha mkataba wa kudumu.

BAADA ya kuona Manchester United imedhamiria kweli kutaka kumsajili beki wao raia wa England, Jarrad Branthwaite, mabosi wa Everton wamenza harakati za kumsajili beki wa kati wa Galatasaray na Colombia Davinson Sanchez, 27, ili akawe mbadala wake.

Man United ilianza kuiwania huduma ya Jarrad tangu dirisha la majira ya baridi mwaka huu na taarifa zinadai wapo tayari kulipa zaidi ya Pauni 50 milioni inayohitajika.

TOTTENHAM ipo tayari kumuuza beki wao kutoka Brazil Emerson Royal katika diisha lijalo la majira ya kiangazi ambapo timu kibao ikiwemo Juventus, AC Milan na Bayern Munich zimeonyesha nia ya kutaka kumsajili na tayari zimeshaanza mazungumzo na wawakilishi wake.

Royal mwenye umri wa miaka 25, mkataba wake wa sasa na Spurs unamalizika mwaka 2026. Msimu huu amecheza mechi 24 za michuano yote.

NEWCASTLE huenda ikamsajili beki wa Bournemouth Lloyd Kelly, 25, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi ambapo atakuwa mchezaji huru baada ya mkataba wake wa sasa kumalizika.

Timu nyingi zimeonyesha kuvutiwa na staa huyu kutokana na kiwango alichoonyesha msimu huu. Msimu uliopita Kelly alicheza mechi 25 za michuano yote.

CHELSEA inahitaji zaidi ya Pauni 25 milioni katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi ili kumuuza beki wao raia wa England, Trevoh Chalobah, 24, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.

Chalobah ni mmoja kati ya mastaa wanaohusishwa kuondoka Chelsea katika dirisha lijalo kwa sababu hapati nafasi ya kutosha kwenye kikosi cha kwanza. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2028. Msimu huu amecheza mechi 17 za michuano yote.

Chanzo: Mwanaspoti