Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wimbi la Fei, Dube lidhibitiwe kivyetu

Prince Dube Ms Wimbi la Fei, Dube lidhibitiwe kivyetu

Tue, 12 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Mwaka 2013 ulizuka mjadala mkubwa kuhusu mpango wa Arsenal kutaka kumnunua mshambuliaji wa kimataifa wa Uruguay, Luis Suarez kutoka Liverpool nchini England.

Wakati huo, Suarez alikuwa akilazimisha uhamisho kwenda London Kaskazini kwa utashi wake binafsi. Hali wakijua kuna sakata hilo, Arsenal walifanya uchunguzi na kugundua kuwa kuna njia ya kupitia.

Akitokea Ajax Amsterdam, Suarez alisaini mkataba uliowekwa kifungu kilichoeleza kuwa iwapo kutakuwa na klabu inayomtaka na ikaweka dau la Pauni 40 milioni au zaidi, ataarifiwe.

Arsenal wakaweka dau la Pauni milioni 40+1 lakini mmiliki wa Liverpool wakati huo, John Herry aliposikia hilo alikerwa na moja kwa moja akaenda kwenye ukurasa wake mtandaoni na kuandika “hivi huko Emirates wanavuta nini?” Kauli hiyo ilivuruga kila kitu.

Lakini Arsenal walijua kuwa dau lao lilikuwa ni kwa ajili ya kuanzisha mazungumzo ya kumsajili Suarez na kwamba walijua dau hilo halikuwa kifungu cha kununua mkataba (buy-out clause) au dau lililowekwa na klabu iwapo mchezaji atataka kununuliwa (release clause).

Kilichofuata ni mijadala kuhusu dhana hizop mbili na ikaonekana katika baadhi ya nchi kuna vitu vyote viwili na nyingine hazina. Nchini Hispania, ni lazima kila mkataba wa mchezaji uwe na kipengele cha kumuachia mchezaji (release clause) na ndicho walichotumia Arsenal kumnunua Thomas Partey kutoka Atletico Madrid baada ya kuwakilisha dau kwa Ligi Kuu ya Hispania (La Liga) ambayo ikalazimika kuitaarifu Atletico kuwa kiungo huyo ‘ameshawekewa kifunga uchumba’ na hivyo aendelee na mazungumzo na klabu inayomtaka. Hilo haliko England.

Kwa hiyo, si lazima kanuni kuhusu wachezaji kununuliwa au kuvunja mikataba zifanane ‘eti’ kwa sababu Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) limeweka kanuni. Ili mradi tu yale mambo ya msingi yafikiwe. Nasema hivyo kutokana na sakata la wachezaji kuvunja mikataba linaonekana kushika kasi.

Wiki iliyopita ilikuwa ni zamu ya mshambuliaji wa kimataifa wa Zimbabwe, Prince Dube kuvunja na Azam, ikiwa ni miezi michache baada ya Feisal Salum kufanikiwa kuvunja na Yanga, sakata lililofanikishwa na ombi la Rais Samia Suluhu. Sasa si Fei Toto pekee, ukiacha Dube aliyeingia kwenye treni hiyo wiki iliyopita, wako wachezaji kama Habib Kyombo, Adam Adam na Yusuf Kagoma walioomba kuvunja mikataba yao, baadhi wakiwa wanaeleweka wanataka kujiunga na timu gani.

Sakata la Fei Toto ndilo lililotamba zaidi kutokana na Yanga kumkatalia kutekeleza uamuzi wake wa kuachana na vigogo hao wa mitaa ya Twiga na Jangwani.

Kiungo huyo Mzanzibari aliingiza Sh112 milioni kwenye akaunti ya Yanga kama masharti ya mkataba yanavyotaka na kuandika barua ya kuvunja mkataba, lakini Yanga walimkatalia kwa maelezo kuwa kanuni za Fifa zinataka kuwe na sababu zinazoweza kuhalalisha uamuzi huo (just cause).

Sababu za Fei Toto hazikuwa na mashiko na zilikuwa kwenye uwezo wake. Kuthaminiwa na klabu hakuhusiani na wengine kulipwa fedha nyingi, bali uwezo wako wa kuipandisha thamani yako katika mazungumzo ya mkataba.

Kwa hiyo, inawezekana kabisa kuwa Fifa haikubaliani na kitendo cha kumlazimisha mchezaji kuchezea timu ambayo haitaki, lakini lazima kuwe na sababu za kimsingi za kimpira kukubaliana naye kuvunja mkataba tena katika kipindi kinacholindwa, au Fifa wamekiita ‘protected period’.

Hiki ni kifungu ambacho lengo lake ni kuulinda mpira wa miguu, hasa katika ngazi ya klabu ambako mchezaji husajiliwa kwa kipindi fulani na kwa malengo fulani ndani ya kipindi hicho. Kwa hiyo anapotaka kuondoka bila ya sababu za msingi, anaharibu malengo ya klabu (organizational goals) ambayo pia yalitegemea malengo binafsi ya mchezaji (individual goals).

Mpira wa miguu si mchezo kama fani ya uhasibu ambayo unatimua leo na kuajiri mwingine mwenye sifa zinazotakiwa, bali unasajili leo ukitegemea mrejesho baada ya muda fulani ingawa kwa nadra mrejesho huja mara moja.

Halafu huyo mchezaji alianza kutoitaka timu iliyomsajili lini? Alisaini mkataba kwa mtutu wa bunduki? Kama hakulazimishwa kusaini, ni lazima awe na sababu za msingi za kuuvunja.

Kwa hiyo, miongozo ya Fifa kuhusu wachezaji ipo lakini ni muhimu ikatofautiana kulingana na maendeleo ya nchi kielimu, kiuchumi na kiustaarabu hadi hapo itakapofikia kuwa uwezo wetu wa kufikiri na kujenga hoja unaweza kuendana na miongozo ya Fifa au CAF.

Na kizuri zaidi ni kwamba Fifa huwa hawana tatizo na kanuni za soka za nchi ili mradi tu ziwe zimeundwa na chombo husika na hazikuiuki masuala mengine ya kimsingi duniani. Yaani kama mchezaji akienda kulalamika Fifa kuwa hajatendewa haki, ni lazima chombo hicho kinachosimamia uendeshaji wa mpira wa miguu kiangalie kanuni zenu za ndani kama zilifuatwa na ndipo kiamue.

Ndio maana Hispania wana kifungu kwenye kanuni zao kinachoruhusu klabu inayomtaka mchezaji fulani, ilipie dau la kumnunua lililowekwa kwenye mkataba wake na fedha hizo ziwasilishwe La Liga ndipo ligi hiyo iitaarifu klabu inayommiliki mchezaji kwa wakati huo.

Lakini England hawana hilo. Na hata ikitokea kuna kifungu cha kumnunua mchezaji halafu dau likawekwa kubwa, mchezaji anaweza kuwasilisha rufaa Ligi Kuu akijenga hoja kwamba klabu inataka kumzuia asihame kwa kuweka dau ambalo ni kubwa kuliko thamani yake.Kwa hiyo, Ligi Kuu Bara inaweza kuandika kanuni zake kulingana na mazingira ya nchi yetu, kiwango chetu cha ustaarabu na mambo mengine muhimu.

Suala la kuvunja mkataba sasa linaonekana kushika kasi na hatujui nani ataongezeka kesho. Fei Toto alishutumiwa kuwa alifanya hivyo kuitikisa Yanga kabla ya mechi na Azam na hata TFF walipokuwa wakitaja siku ya kusikiliza shauri, iliangukia siku ambayo Yanga ina mechi ya kimataifa na hivyo kuimarisha shutuma kuwa alitaka kuihujumu.

Na sakata la Dube limeibuka siku chache kabla ya timu hizo mbili kukutana na linachukuliwa kama kitendo cha kulipa kisasi kwa alichofanya Fei Toto.

Kikomo cha shutuma hizo ni anga tu. Ili lisifike huko, Bodi ya Ligi haina budi kuliangalia kwa makini, kuulizia uzoefu kwa nchi za wenzetu na hatimaye kulipatia dawa ili kuwezesha klabu kutekeleza malengo vizuri bila kuathiriwa na mambo ya nje ya uwanja, lakini pia kujenga imani kwa wachezaji. Maana wakiingia kwenye shutuma za kuhujumu timu, kujisafisha ni kazi kubwa.

Chanzo: Mwanaspoti