Aliyekuwa Beki wa Klabu za London (Chelsea, Arsenal na Spurs) William Gallas anaamini Mshambuliaji Harry Kane ataondoka Tottenham mwishoni mwa msimu huu kwa sababu si timu ya kupambania mataji.
Manchester United inavutiwa na mpango wa kumsajili nahodha huyo wa England, ambaye atafikisha umri wa miaka 30 Julai mwaka huu.
Kane bado hajabeba taji lolote kubwa katika maisha yake ya soka, lakini ndiye mchezaji mwenye nafasi kubwa ya kuvunja rekodi ya mabao ya Alan Shearer, aliyefunga mara 260 kwenye Ligi Kuu England. Kwa sasa Kane amefunga mabao 207 kwenye ligi hiyo.
Kane ataingia katika mwaka wake wa mwisho kwenye mkataba wa Spurs itakapofika mwishoni mwa msimu huu na sasa yupo njia panda juu ya ama abaki kwenye kikosi hicho au afungue milango ya kutimkia kwingineko. Kitu cha zaidi ni kwamba Spurs hawatapenda kumpoteza bure.
Lakini, beki wa zamani, Gallas, aliyewahi kuichezea Spurs kati ya 2010 na 2013, ambapo alikuwapo uwanjani wakati Kane alipocheza mechi yake ya kwanza Spurs, aliulizwa kama yeye angekuwa Kane angefanya uamuzi gani.
Gallas, aliyewahi pia kucheza Arsenal na Chelsea alijibu: “Harry Kane ataondoka mwisho wa msimu. Harry Kane anapaswa kuondoka. Aondoke. Nataka Harry apate utamu wa kubeba kombe.”