Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wilbo Maseke na ndege acha kabisa

Wilbol Maseke Wilbo Maseke na ndege acha kabisa

Sun, 4 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kila binadamu ana udhaifu wa kuogopa kitu fulani kwenye maisha yake, kama ilivyo kwa kipa wa KMC, Wilbol Maseke kuogopa kupanda usafiri wa ndege na amesimulia tukio kubwa ambalo hatalisahau kwenye maisha yake na lilitokea wakati wakiwa kwenye ndege.

Kabla ya msimu uliopita kujiunga na KMC, Maseke alikuwa Azam FC ambako alifanya tukio lililowaacha wachezaji wenzake na viongozi mdomo wazi.

Amesimulia sababu ya kuogopa usafiri wa ndege "Ilikuwa mwaka 2022 tulikuwa tunakwenda Arusha, sasa kulitokea matukio ya ndege kuanguka, nikamwambia kocha sipandi ndege akanibembeleza hadi nikakubali," anasema na kuongeza;

"Tukafika hadi uwanja wa ndege, tumepanda vizuri tu, wachezaji mara nyingi tunapenda kukaa siti za nyuma kabisa, nakumbuka ile ndege ilikuwa na abilia wa kizungu wasiozidi watano, mara tukaambiwa tufunge mikanda, tukafunga baada ya dakika kadha likatoka tangazo lingine, kuna tatizo kidogo limetokea tutapandishwa ndege nyingine.

Ameendelea kusimulia "Matangazo ni ya Kiingereza, mimi nikasimama nikatoa begi langu, wachezaji wenzangu wakaanza kucheka na kuniona nimechanganyikiwa, nikawaambia ni kweli sijui sana Kiingereza ila nimeelewa, mara wazungu nao wakachukua mabegi yao na kuanza kushuka.

"Baada ya muda fulani wakasema tatizo lilikuwa mlango na wamerekebisha tunatakiwa kuendelea na safari, mimi nikakataa, akaja meneja wa ndege kuniomba nikamkatalia, akaja kocha na meneja wa timu nikasimamia msimamo wangu, nikachwa na kurejea kambini, kila mtu alibaki ananitazama na kunishangaa, ila mimi kwenye kuyatetea maisha yangu sifanyi mzaha kabisa."

Si mara moja kukataa kusafiri na ndege, akiwa Azam ni zaidi ya mara 10 anapanda basi la timu peke yake.

"Kuna kipindi nilipanda basi peke yangu ilikuwa safari ya kwenda Kagera, nilifika miguu imevimba wachezaji wenzangu ambao walitumia muda mchache kufika wakaanza kunicheka na kuniambia wee jamaa una mambo ya ajabu, niwe wazi na mkweli mimi usafiri wa anga siuwezi," amesema.

Chanzo: Mwanaspoti