Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wikiendi ya mabingwa... Simba, Coastal zatambiana

Simba Vs Coastal Wikiendi ya mabingwa... Simba, Coastal zatambiana

Sat, 9 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Achana na pambano la jana usiku lililozikutanisha Yanga na Namungo, uhondo wa Ligi Kuu Bara unaendelea leo kwa kushuhudiwa viwanja vitatu tofauti vikiwaka moto, lakini utamu zaidi ni mechi mbili za kibabe zitakazowatanisha mabingwa watupu wa zamani katika miji ya Tanga na Morogoro.

Ndio, kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga kuanzia saa 12:00 jioni kutakuwa na pambano la wenyeji Coastal Union dhidi ya Simba litakalotanguliwa mapema saa 10:00 jioni na mechi ya Mtibwa Sugar dhidi ya Tanzania Prisons, itakayopigwa kwenye Uwanja wa Manungu Complex, Turiani Morogoro.

Mechi nyingine ya leo itapigwa kuanzia saa 2:15 usiku kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma kwa wenyeji Dodoma Jiji watakaoialika Geita Gold.

Kama hujui ni kwamba mechi mbili za mapema zote zinakutanisha mabingwa wa zamani, Simba ndio klabu inayoshika nafasi ya pili kwa kutwaa mataji mengi ya Ligi Kuu baada ya Yanga, ikibeba mara 22, saba pungufu na waliyonayo watani wao wa jadi wenye 29, huku Coastal waliwahi kutwaa taji hilo mwaka 1988.

Pale Manungu, wenyeji Mtibwa ni mabingwa wa misimu miwili mfululizo wa ligi hiyo walikitwaa mwaka 1999 na 2000, huku Tanzania Prisons imeshatwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Muungano (sasa haipo) mwaka 1999, hivyo pambano hilo la Morogoro pia ni la kibingwa zaidi kama ilivyo kwa Wekundu wa Msimbazi dhidi ya Wagosi wa Kaya.

TUANZIE HUKU

Simba inakabiliwa na kibarua kigumu cha kuhakikisha ndoto za kusaka ubingwa kwa msimu huu zinabaki hai wakati itakapokaribishwa na Coastal ambayo tangu iwe chini ya Mkenya David Ouma imeonyesha sio ya kuichukulia poa.

Kitendo cha Simba kupoteza mechi iliyopita mbele ya Tanzania Prisons kiliifanya Simba ijikute ikitengeneza pengo la pointi saba na Yanga kabla ya mechi ya jana dhidi ya Namungo, hivyo kupoteza pointi tatu au hata kutoka sare leo, kimahesabu kutazidi kufifisha matumaini yake ya kutwaa ubingwa wa ligi hiyo msimu huu.

Kwa upande wa Coastal hiyo ni mechi ya kimkakati kwake kwa vile inahitaji kupata ushindi ambao utazidi kuiweka katika mazingira mazuri ya kujihakikishia nafasi ndani ya nne za juu kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Coastal hadi sasa inashika nafasi ya nne ikiwa imekusanya pointi 27 wakati Simba ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 36.

Wakati Simba ikiingia katika mechi hiyo huku ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Prisons kwa mabao 2-1, Coastal yenyewe imetoka kulazimisha sare ya bao 1-1 dhidi ya Azam FC.

Ni mechi ambayo inakutanisha timu moja inayofanya vizuri zaidi katika mechi za nyumbani dhidi ya timu ambayo inatamba ugenini msimu huu.

Coastal mechi tisa ilizocheza nyumbani hadi sasa, imepata ushindi mara tano, kutoka sare mbili na kupoteza michezo miwili wakati Simba katika mechi nane ambazo imeshacheza ugenini, imepata ushindi mara saba na kutoka sare moja.

Wagosi wa Kaya wamekuwa na unyonge wa muda mrefu mbele ya Simba na pengine leo wanaweza kuvunja minyororo ya kuteswa na Simba katika Ligi Kuu kwa kupata ushindi vinginevyo wataendeleza historia ya kuonewa na Wekundu hao.

Coastal ina siku 3,640 (miaka 9 na miezi 11) bila kupata ushindi mbele ya Simba katika Ligi tangu ilipofanya hivyo kwa mara ya mwisho Machi 23, 2014 ilipoibuka na ushindi wa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Kudhihirisha Simba ni wababe wa Coastal, katika mechi 10 zilizopita baina yao kwenye ligi, imeibuka na ushindi katika mechi nane na kutoka sare mbili, Simba ikifunga mabao 30 sawa na wastani wa matatu kwa mchezo huku Coastal ikifunga mabao mawili tu.

Simba katika mechi hiyo haitokuwa na kocha mkuu, Abdelhak Benchikha aliyeenda kwao Algeria kuhudhuria kozi ya kupiga msasa makocha, lakini kocha msaidizi Selemani Matola anaamini watafanya vizuri, akitegemea makali ya Clatous Chama, Willy Onana, Saido Ntibazonkiza, Freddy Michael na Pa Omary Jobe katika kusaka mabao Mkwakwani.

“Tupo hapa Tanga kwa mchezo dhidi ya Coastal Union. Ni mchezo mgumu ukizingatia wenyeji wamekuwa wanafanya vizuri katika siku za hivi karibuni na mara nyingi mechi zetu huwa ngumu lakini tumejiandaa kuhakikisha tunafanya vizuri,” alisema Matola, huku kocha wa Coastal, David Oumma alisema kuwa wanaiheshimu Simba lakini wamejiandaa na wapo tayari kukabiliana nayo.

“Simba ni timu nzuri na kubwa hivyo tunapaswa kuwa waangalifu, ila kwa sasa tumekuwa vizuri na naamini mambo yatakuwa mazuri kwetu,” alisema Ouma atayeendelea kutegemea umahiri wa kipa Ley Matampi anayeongoza kwa clean sheet akiwa na tisa, sambamba na nahodha Ibrahim Ajibu na Charles Semfuko na Crispin Ngushi.

Ushindi wa mechi ya leo kwa Coastal utaifanya izidi kujikita ndani ya Nne Bora kwani itafikisha pointi 30, ikiwa ni sita pungufu na ilizonazo Simba na iwapo itapoteza kisha Prisons kupata ushindi Manungu itashushwa hadi nafasi ya tano.

VITA IPO HAPA

Katika pambano la saa 10:00 jioni, wenyeji Mtibwa watakuwa na vibarua viwili wakati watakapoialika Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Manungu Complex.

Kwanza ni kuendeleza matokeo mazuri baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 katika mechi iliyopita dhidi ya Singida Fountain Gate utakaoifanya ifikishe pointi 15 na kuweka hai matumaini ya kubaki Ligi Kuu kwa msimu ujao kwani inaburuza mkia kwa sasa tena kwa muda mrefu ikiwa na alama 12 tu kupitia mechi 18.

Lakini pili ni kusimamisha kasi ya Prisons ambayo imeonekana kuwa moto wa kuotea mbali katika siku za hivi karibuni, tangu iwe chini ya kocha Ahmad Ally imetoka kucheza mechi nne mfululizo bila kupoteza ikishinda tatu na kutoka sare moja na kuipeleka hadi nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi ilikwa na pointi 27 kama Coastal.

Hii ni mechi isiyotabirika kutokana na timu zote kuwa na uzoefu wa ligi na pia zina wachezaji wanaofahamiana kwa muda mrefu, lakini kila moja ina lengo la kusaka ushindi ili kujikwamua zilipo.

Prisons itaendelea kuwategemea nyota wake, Jeremiah Juma, Samson Mbangula aliyeweka rekodi ya kucheza mechi sita mfululizo za Ligi na kufunga mabao sita, Hamis Zabona, sambamba na wakali wengine kuibana Mtibwa inayowategemea Charles Ilanfya, Rashid Karihe, Ally Hillary, Jimmyson Mwanuke na Nassoro Kapama.

Rekodi zinaonyesha katika mechi tano za ligi zilizopita Mtibwa inayonolewa kwa sasa Zuberi Katwila imeshinda mara moja tu, huku Prisons ikishina tatu ikiwamo ya duru la kwanza la msimu huu, jijini Mbeya ambapo maafande hao walishinda 3-2 na mechi mbili zikiisha kwa suluhu.

Kwa namna namba zinazosomeka ni wazi Manungu kutakuwa na vita ya kibingwa baina ya timu hizo ambazo ziliwahi kujitengenezea sifa katika soka la Tanzania kwa kutandaza soka na kuvitoa nishai vigogo, Simba na Yanga.

DODOMA, GEITA MTEGO

Mechi ya kufungia hesabu za leo ni ile ya kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma wakati wenyeji Dodoma Jiji watapoikaribisha Geita Gold katika mchezo utakaoanza saa 2:15 usiku.

Kocha Francis Baraza wa Dodoma Jiji hapana shaka atakuwa na lengo la kupata ushindi wa pili mfululizo katika ligi kufuatia ule wa bao 1-0 dhidi ya Tabora United katika mechi iliyopita na matokeo hayo yataifanya ifikishe pointi 26 zinazoweza kuipeleka timu yake hadi nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi.

Kwa upande wa Geita, ushindi wa leo ndio unaweza kuwapa ahueni na unaweza kuwatoa katika nafasi ya 15 waliyopo sasa pengine hadi ile ya 11 kwani watafikisha pointi 21.

Dodoma itaendelea kuwategemea nyota wazoefu wa ligi hiyo kama Hassan Mwaterema, Emmanuel Martins na wengine kukabiliana na Geita inayonolewa na Dennis Kitambi yenye wakali kama Tariq Seif, Valentino Mashaka, Elias Maguri, Juma Mahadhi na mkongwe Kelvin Yondani.

Mechi iliyopita kati ya timu hizo msimu huu iliisha kwa sare ya mabao 2-2, lakini kwa ujumla zimeshakutana mara tano katika Ligi Kuu na Geita imeshinda mara mbili, huu Dodoma ikishinda moja na mbili zilizobaki ziliisha kwa sare na Geita imevuna jumla ya mabao saba ilihali wenyeji wao wa leo, Dodoma wakivuna manne tu.

KESHO NAKO

Ligi hiyo itaendelea kesho Jumapili kwa pambano moja tu litakalozikutanisha KMC dhidi ya Tabora United, mchezo utakaopigwa kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja Azam Complex, huku kila moja ikiwa na kumbukumbu ya kutoka kupoteza ugenini KMC ikilala 1-0 mbele ya Ihefu na Tabora pia ikicharazwa 1-0 na Dodoma Jiji, jijini Dodoma.

Ni mechi ngumu kwa timu zote zinazopambana kutaka kujiweka eneo zuri la msimamo wa ligi hiyo iliyopo raundi ya 21, Tabora inayocheza Ligi Kuu kwa msimu wa kwanza ikiwa na presha ya kuondoka eneo la hatari la kushuka daraja, kwani ipo nafasi ya 13 ikiwa na pointi 21 sawa na wageni wenzao wa ligi hiyo, Mashujaa Kigoma.

KMC iliyoanza kazi kwa sasa ina pointi 25 ikiwa nafasi ya sita (kabla ya matokeo ya mechi ya jana) ina kazi ya kusahihisha makosa kutokana na kuteleza kwenye mechi za hivi karibuni, ikijua kupoteza tena itawapa nafasi wapinzani wao kupunguza pengo la pointi kutoka nne hadi kuwa moja tu.

Timu hizo zinazonolewa na makocha wa kigeni, Tabora ikiwa na Mserbia Goran Kopunovic na KMC ikiwa chini ya Mmarekani mwenye asili ya Somalia, Abdihamid Moallins kila moja zitawategemea nyota wao wanaojua kucheka na nyavu, Wazir Junior, Shaaban Idd Chilunda na Daruwesh Saliboko kwa KMC na Eric Okutu akibeba mikuki ya Nyuki.

Wazir ana mabao manane, Okutu ana sita, huku timu hizo zikiwa na kumbukumbu na suluhu mechi ya kwanza.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: