Wababe wa Ligi Kuu, Simba na Yanga wiki hii watakuwa na mechi za kuamua hatima yao katika mashindano ya Kimataifa.
Simba inashuka uwanjani hapo Jumamosi na Jumapili wiki hii Yanga itakuwa kwenye uwanja huohuo kukipiga na Monastir, ambapo mechi zote zitaanza saa 1:00 usiku.
Hata hivyo, wiki hii ndio inayoonekana kuwa ya moto na yenye uamuzi kwa timu hizo kutinga robo fainali. Kwa Simba mchezo wa nyumbani dhidi ya Horoya ni wa kufa au kupona kwa Simba ikizingatiwa kwamba inamaliza michezo ya makundi mjini Casablanca ambako itaifuata Raja na ndio maana tunaamini kwamba ije mvua au liwake jua Simba inalazimika kuutumia vizuri uwanja wa nyumbani Jumamosi hii.
Hesabu kama za Simba zinapaswa kuchangwa na Yanga ambayo inakutana na US Monastir kwenye uwanja huohuo kwani ndio inayoongoza kundi D ikiwa na alama 10 na huku ikiwa imeshafuzu hatua ya robo fainali.
Ndio maana tunasema, kama ilivyo kwa Simba, Yanga pia inalazimika kushinda mchezo huu wa nyumbani kwa sababu mchezo wa mwisho itaenda kuucheza ugenini dhidi ya TP Mazembe, ambako hakika kutakuwa kugumu zaidi kushinda.
Kila la heri Simba, Yanga.