Mambo ni moto wiki hii katika Ligi ya Championship kutokana na uwepo wa mechi sita za watani wa jadi (dabi) zitakazochezwa katika viwanja na miji tofauti hapa nchini.
Utamu wa dabi hizo unanogeshwa zaidi na nafasi ambazo timu husika zipo kwenye msimamo wa ligi hiyo ambapo matokeo ya mechi hizo zitakazochezwa wiki hii, yatasababisha ama kuongeza pengo la pointi baina ya timu hizo, kuzipandisha baadhi ya timu au kuzidi kuziweka pabaya nyingine katika msimamo.
Dabi tamu zaidi ni ile ya Arusha itakayozikutanisha Mbuni FC na TMA Stars katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, keshokutwa Jumamosi kutokana na timu hizo zote kutokea katika mji wa Monduli, Arusha.
Mbuni iko nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 10 ambapo ikipata ushindi, itaongeza pengo la pointi na watani wao hao kufikia tano kwani TMA Stars kwa sasa ina pointi nane ikiwa ni ya nne.
Ikumbukwe TMA Stars inamilikiwa na Chuo cha Maofisa wa Jeshi Monduli ambacho kinatengenishwa na barabara tu na kambi ya Mbuni inayomiliki Mbuni FC.
Ijumaa kutakuwa na dabi ya Dar es Salaam kati ya Pan Africans inayoshika nafasi ya 13 kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi tatu dhidi ya Cosmopolitan iliyopo nafasi ya 15 na pointi yake moja, mechi ambayo itachezwa katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. Timu hizo kongwe zimewahi kutamba na kubeba ubingwa wa Ligi ya Bara, Cosmo ikinyakua mwaka 1967 na Pan ikafanya yake mwaka 1982.
Kama ilivyo kwa TMA Stars na Mbuni, Jumamosi kutakuwa pia na dabi ya Mwanza kati ya Pamba na Copco huku kukiwa pia na dabi ya Mbeya kati ya Mbeya City na KenGold.
Pamba iliyo nafasi ya tano katika msimamo wa Championship ikiwa na pointi saba, itakuwa kwenye Uwanja wa Nyamagana kuanzia saa 10:00 kuikabili Copco ambayo iko nafasi ya 12 ikiwa na pointi tatu, wakati Mbeya City iliyo nafasi ya tatu na pointi zake tisa itacheza na ndugu zao KenGold kwenye Uwanja wa Sokoine.
Jumapili kuna mechi ya dabi ya maafande, Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo kati ya Green Warriors na Transit Camp, katika Uwanja wa Karume, mjini Musoma Mara wenyeji Biashara United watakuwa na dabi ya Kanda ya Ziwa dhidi ya Stand United kutoka Shinyanga.
Ukiondoa dabi hizo, Ijumaa kutakuwa na mechi baina ya Polisi Tanzania na Fountain Gate katika Uwanja wa Ushirika, Moshi na Jumapili kutakuwa na mechi baina ya vinara Mbeya Kwanza dhidi ya Ruvu Shooting katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.