Kuna mastaa walikosekana kuonekana kwa muda mrefu kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu England na sasa mashabiki wanafurahia kurejea kwao baada ya mapumziko ya mechi za kimataifa na bila ya shaka wakali hao wakirudi, kuna mambo kibao yatatokea uwanjani.
NGOLO KANTE (CHELSEA)
Tangu NGolo Kante alipochaguliwa Mchezaji Bora wa Mechi kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Manchester City, Mei 2021 alikumbana na majeruhi mara sita tofauti na kukosa mechi 50.
Hakuonekana uwanjani tangu ilipochezwa mechi ya pili msimu huu, wakati Chelsea iliyokuwa chini ya Thomas Tuchel ilipotoka sare ya 2-2 na Tottenham Hotspur ya Antonio Conte.
Ndani ya muda ambao Kante amekuwa nje ya uwanja, Chelsea imetumia hadi Pauni 600 milioni kusajili mastaa wapya wakiwa na matumaini ya kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo kwenye hatua ya robo fainali waliyotinga wamepangwa kukipiga na Real Madrid. Chelsea kwa sasa ipo chini ya Graham Potter na huenda Kante akajikuta akibadilishiwa nafasi ndani ya uwanja wakati atakaporejea na kupangwa kwenye mechi.
CHRISTIAN ERIKSEN (MAN UNITED)
Kukosekana kwa huduma ya kiungo mchezeshaji Christiaan Eriksen kulionekana si tatizo kwenye kikosi cha Manchester United baada ya wakali wengine kufanya vizuri hasa Casemiro na Mbrazili mwenzake, Fred, wanaomfanya Bruno Fernandes kuwekeza akili zaidi kwenye kushambulia.
Lakini, ukweli utabaki palepale kwenye kikosi hicho cha kocha Erik ten Hag, Eriksen anazidiwa na Fernandes tu kwa kuasisti mara nyingi, yeye ameasisti mara tisa, wakati kiungo huyo wa Kireno ameasisti 10 huku akicheza karibu dakika 1,600 zaidi.
Casemiro amekuwa akisaidia sana kwenye kutengeneza pasi za mbele, lakini kurejea kwa Eriken kikosi kutaongeza kitu muhimu licha ya yimu hiyo kuwa na viungo wengine makini akiwamo Marcel Sabitzer, aliyenaswa kwenye dirisha la Januari.
LUIS DIAZ (LIVEPOOL)
Jurgen Klopp anaamini kwamba staa wake Luis Diaz ataendelea kuwa na mchango mkubwa kwenye kikosi kama alivyokuwa katika hajapata majeruhi.
Staa huyo wa kimataifa wa Colombia alikuwa kwenye kiwango bora na hatari katika safu ya ushambuliaji ya Liverpool kabla ya kuumia na kuifanya timu hiyo kukosa huduma yake muhimu. Liverpool inasaka nafasi ya kumaliza walau kwenye Top Four kwenye msimamo wa Ligi Kuu England ili kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Liverpool imekuwa na washambuliaji wengi kama Mohamed Salah, Darwin Nunez, Diogo Jota na Cody Gakpo, lakini kurejea kwa Diaz kutampa Klopp machaguo ya kutosha kwenye safu yake ya ushambuliaji.
DOMINIC CALVERT-LEWIN (EVERTON)
Everton hali yao ya mambo kwenye Ligi Kuu England imekuwa ngumu na pengine hilo limetokana na kukosa huduma ya mshambuliaji wao hatari Dominic Calvert-Lewin kwa muda mrefu.
Staa huyo alikuwa kwenye ubora mkubwa msimu uliopita na kuhusishwa na klabu mbalimbali ikiwamo Arsenal, ambao walikuwa wakidaiwa kwamba huenda wakapiga hodi Goodison Park kwenye kunasa saini yake.
Lakini, sasa mkali huyo Calvert-Lewin anarejea na jambo hilo litamfanya kocha Dyche kuwa kwenye wakati mzuri kutokana na kurejea kwa mchezaji ambaye suala la kufunga halijawahi kuwa tatizo na kwa sasa Everton inahitaji mabao kuliko kitu kingine chochote.
YOURI TIELEMANS (LEICESTER CITY)
Leicester City itaendelea kuhitaji huduma ya mchezaji ambaye alikaribia kabisa kuondoka kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi na bila ya shaka huenda akaondoka mwishoni mwa msimu huu.
Hata hivyo, Tielemans ni moja ya wachezaji mahiri kwenye Ligi Kuu England na huduma yake imekuwa ikihusishwa na timu nyingi vigogo wakiwamo Manchester United na Arsenal. Chama hilo la kocha Brendan Rodgers, Leicester City lilicheza wiki sita bila ya huduma ya mchezaji huyo, hivyo kurudi kwake kutakuwa na faida kubwa kwenye kikosi kutokana na ubora wake wa ndani ya uwanjani.
Leicester City ina wastani wa ushindi wa asilimia 38 ikiwa na mchezaji huyo uwanjani, wakati ina wastani wa ushindi wa asilimia 20 tu inapocheza bila ya huduma ya Tielemans.