Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wenye rekodi zao za mabao Big Six England hawa

Mabao Epl.jpeg Wenye rekodi zao za mabao Big Six England hawa

Sun, 15 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Maisha yanakwenda haraka. Mohamed Salah amebakiza mabao matatu tu huko Liverpool kwa upande wa Ligi Kuu England kufikia rekodi ya Robbie Fowler.

Lakini, mambo ni matamu pia kwa Harry Kane, ambaye yupo kwenye wakati bora wa kumwondoa Jimmy Greaves kwa wakati wa mabao katika kikosi cha Tottenham Hotspurs. Wakati wakali hao wakikaribia kuweka majina yao kwenye rekodi bora kabisa za mabao katika klabu zao, je huko kwingine kwa upande wa klabu za Big Six zikoje?

Hii hapa orodha ya wanasoka wanaoongoza kwa mabao katika klabu za Big Six na wale wakali waliopo kwenye nafasi nzuri ya kufikia rekodi hizo.

Mambo ni moto na hivi ndivyo mkeka unavyosomeka wa kuhusu vinara wa mabao kwenye vikosi vya Big Six kwenye Ligi Kuu England.

ARSENAL

Kinara wa mabao Ligi Kuu: Thierry Henry (mabao 175, mechi 258)

Kinara wa mabao muda wote: Thierry Henry (mabao 228, mechi 377)

Anayefukuzia kwa sasa: Bukayo Saka (Ligi mabao 23, muda wote mabao 30)

Kwenye kikosi cha Arsenal, Thierry Henry rekodi zake zitakuwa salama kwa muda mrefu, hazionekani kuwa kwenye hatari ya kufikiwa wala kuvunjwa kwa kipindi hiki. Bukayo Saka ndiye mwenye mabao mengi kwa waliopo Arsenal kwa sasa, akiwa amefunga 23 kwenye Ligi Kuu England katika mechi 114 na mabao 30 katika mechi 154 za michuano yote. Saka atabaki Arsenal hadi lini?

CHELSEA

Kinara wa mabao Ligi Kuu: Frank Lampard (mabao 147, mechi 429)

Kinara wa mabao muda wote: Frank Lampard (mabao 211, mechi 648)

Anayefukuzia kwa sasa: Mason Mount (Ligi mabao 27, muda wote mabao 33)

Unapokuwa kiungo na ndiye kinara wa mabao ni jambo kubwa, lakini Frank Lampard anashikilia rekodi za kibabe kabisa huko Chelsea. Ndiye kinara wa mabao wa Chelsea kwenye Ligi Kuu England na kwenye michuano yote. Mason Mount kwa sasa ndiye anayejaribu kupambana kufukuzia rekodi hiyo, akifunga mara 27 katika mechi 121 kwenye Ligi Kuu na mabao 33 katika michuano yote.

LIVERPOOL

Kinara wa mabao Ligi Kuu: Robbie Fowler (mabao 128, mechi 268)

Kinara wa mabao muda wote: Ian Rush (mabao 346, mechi 660)

Anayefukuzia kwa sasa: Mo Salah (Ligi mabao 125, muda wote mabao 173)

Rekodi ya kinara wa mabao kwenye Ligi Kuu England huko Liverpool haina muda mrefu itakuwa chini ya mchezaji mwingine, lakini ile ya kinara wa mabao wa muda wote kwenye kikosi hicho, Ian Rush ataendelea kuwa salama. Supastaa Mohamed Salah, amebakiza mabao matatu tu kumfikia Robbie Fowler mwenye mabao 128, lakini Rush ndiye kiboko ya mabao kwenye michuano yote, 346.

MAN CITY

Kinara wa mabao Ligi Kuu: Sergio Aguero (mabao 184, mechi 275)

Kinara wa mabao muda wote: Sergio Aguero (mabao 260, mechi 390)

Anayefukuzia kwa sasa: Kevin De Bruyne (Ligi mabao 60, muda wote 89)

Straika wa Kiargentina, Sergio Aguero ataendelea kubaki kwenye vitabu vya kumbukumbu bora kabisa kwenye klabu ya Manchester City kwa muda mrefu sana kutokana na kile alichofanya kwenye timu hiyo. Erling Haaland anatishia uhai wa rekodi zake huko Etihad, lakini atadumu kwa muda gani hasa ikiwa kwa sasa hajamfikia hata Kevin De Bruyne kwa mabao ya ligi na michuano yote.

MAN UNITED

Kinara wa mabao Ligi Kuu: Wayne Rooney (mabao 183, mechi 393)

Kinara wa mabao muda wote: Wayne Rooney (mabao 253, mechi 559)

Anayefukuzia kwa sasa: Marcus Rashford (Ligi mabao 66, muda wote 108)

Kwa wakali waliopo kwenye kikosi cha Manchester United kwa sasa wa kumfikia Wayne Rooney watasubiri kwa muda mrefu sana. Kwenye Ligi Kuu England, Rooney ndiye kinara wa mabao Man United, akifunga mara 183 na kwenye michuano yote, ni kinara pia, amefunga mara 253. Marcus Rashford kwa sasa ndiye mwenye mabao mengi Man United, 66 kwenye ligi na 108 mabao yote.

TOTTENHAM

Kinara wa mabao Ligi Kuu: Harry Kane (mabao 198, mechi 300)

Kinara wa mabao muda wote: Jimmy Greaves (mabao 266, mechi 379)

Anayefukuzia kwa sasa: Kane (mabao 265, mechi 412)

Kwenye kikosi cha Tottenham Hotspur, Harry Kane ndiye kinara wa mabao, akifunga mara 198 katika mechi 300. Kwenye upande huo, supastaa huyo Mwingereza hana mpinzani. Linapokuja suala la kinara wa mabao wa muda wote, Kane amebakiza bao moja tu kumfukia Jimmy Greaves aliyekuwa akishikilia rekodi hiyo ya muda mrefu. Hadi sasa, Kane amefunga mara 265 katika mechi 412.

Chanzo: Mwanaspoti