Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wenye ligi yao WPL

FkkgmmdXoAYQ K .jpeg Wenye ligi yao WPL

Mon, 18 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Katika Ligi Kuu Bara kuna mastaa kibao kama vile Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Jonas Mkude, Zawadi Mauya, Shomari Kapombe, John Bocco na wengineo wengi ambao walianza soka muda mrefu na bado wanacheza.

Upande wa soka la wanawake pia kuna wakongwe walioanza kucheza kitambo na bado wanacheza na kuzisaidia timu zao katika mashindano.

Mwanaspoti linakuletea baadhi ya kinadada walioanza kucheza soka tangu enzi ya kocha Boniface Mkwasa na hadi sasa wapo uwanjani wakiitumikia Ligi Kuu ya Wanawake Bara (WPL). Hawa hapa ‘wenye ligi yao’.

1. MWANAHAMISI OMARY ‘GAUCHO’ (SIMBA QUEENS)

Kama ingekuwa upande wa timu za wanaume, basi mshambuliaji huyo wa zamani wa Mburahati Queens angeimbwa sana kutokana na umahiri wake wa kuzifumania nyavu.

Mwanahamisi alikuwa katika kundi moja na kina Asha Rashid ‘Mwalala’, na licha ya kuwapo muda mrefu kwenye soka, lakini kila anapopata nafasi ya kucheza anaonyesha umahiri wake na msimu huu hadi sasa ametoa asisti tatu na kufunga bao moja katika Ligi Kuu ya Wanawake Bara.

Mwanadada huyo ambaye pia ni maarufu kwa jina la Gaucho aliisaidia Simba Queens kuchukua ubingwa wa kwanza msimu wa 2017/18. Nje na kulijua soka la Bongo, pia alifanikiwa kucheza soka la kulipwa Shabab Atlas (Morocco) ambako alisajiliwa kwa mkataba wa miaka minne.

2. FATUMA MUSTAFA ‘KITUNINI’ (JKT QUEENS)

Ukiwataja mafundi wanaojua kucheka na nyavu huwezi kuacha kulitaja jina la Fatuma Mustafa ambaye tangu aanze kucheza soka la kulipwa amekuwa na kiwango bora.

Nyota huyo amekuwa hapewi heshima kubwa kama Mwanahamisi au wachezaji kama Aisha Masaka kutokana na timu anayochezea kutokuwa na mashabiki wengi.

Fatuma anakipiga JKT na licha ya kwamba umri unaonekana kwamba umeenda, lakini amekuwa mchezaji muhimu katika kikosi hicho.

Katika msimu wa 2016/2017 nyota huyo alifunga mabao 18 na uliofuata akafunga 25, ilhali 2018/2019 alifunga mabao 38 na 2019/2020 akatupia 31 na kuibuka mfungaji bora kwa misimu miwili mfululizo.

3. ASHA MWALALA (SIMBA QUEENS)

Miongoni mwa wachezaji ambao nje na soka maisha yamekuwa tofauti na wengine ni Asha Rashid ‘Mwalala’ ambaye ameolewa na mchezaji wa zamani wa Yanga, Hassan Kessy, kwani ni ngumu kuwaona mabinti wanaosakata kabumbu walioolewa na wana watoto.

Mchezaji huyo alipita katika klabu tatu za ushindani yaani Yanga Princess, JKT Queens na sasa anaichezea Simba Queens.

Kwa sasa hapati nafasi kubwa ya kucheza kutokana na ushindani wa ligi ulivyo kwani kuna mabinti wadogo kama Asha Djafar na Vivian Corazone ambao wanafanya vizuri eneo analocheza.

Pamoja na umri kuonekana kuanza kumtupa mkono sambamba na majukumu ya kifamilia, bado uwanjani anaonyesha uwezo na kuwa miongoni mwa wanawake wenye ushawishi katika soka.

4. STUMAI ABDALLAH (JKT QUEENS)

Ukiachana na Fatuma Issa ‘Fetty Densa’ kumudu kucheza nafasi mbalimbali uwanjani, Stumai Abdallah ni miongoni mwa wachezaji wanazitumikia vyema nafasi wanazopewa kucheza uwanjani.

Ukimtazama unaweza kumdharau kwa umbo lake dogo, lakini kiungo huyo ni hatari anapokaribia langoni kwa wapinzani wao akiwa na uwezo pia wa kucheza kama winga, kiungo na mshambuliaji.

Mrembo huyo ambaye wengi wanamfahamu ni namna anavyojiweka kama mtoto wa kike tofauti na baadhi ya wachezaji wengine ambao mionekano yao ni ya kiume.

Amekuwepo katika soka tangu enzi za Boniface Mkwasa kwenye kikosi cha timu ya taifa ‘Twiga Stars’ na hadi sasa ndiye straika tegemeo wa JKT Queens.

5. DONISIA MINJA (JKT QUEENS)

Ni nyota mkongwe kwenye soka la wanawake na alianza kukipiga tangu 2004 akiwa Shule ya Msingi Airwing na 2009 alisajiliwa na Simba Queens hadi 2014, kisha akajiunga na Evergreen na msimu uliofuata alisajiliwa na JKT Queens ambako yupo hadi sasa.

Ni miaka 16 sasa ya kiungo huyo mkabaji tangu aanze kucheza soka akiwa na JKT Queens na ndio timu aliyocheza muda mrefu.

Kiungo huyo amekuwa muhimu ndani ya kikosi cha JKT Queens na amefanikiwa kuisaidia timu hiyo kuchukua mataji matatu ya ligi katika misimu ya 2017/18, 2018/19 na 2022/23.

Tangu msimu wa kwanza hajawahi kuchuja na amekuwa na ubora uliomfanya ajiwekee ufalme kwenye eneo hilo ambalo siyo rahisi kukaa benchi kutokana na utendaji wake.

Mbali na kuisaidia JKT Queens eneo la ukabaji, pia ana uwezo wa kufunga kwani msimu uliopita alifunga mabao 17 akitofautiana na Jentrix Shikangwa wa Simba aliyefunga mabao 19 na kuibuka na kiatu cha ufungaji.

Ukimtazama mwili wake unaweza kumdharau, lakini ni mzuri wa kupiga mipira ya free-kick, hivyo ni vigumu kwa wachezaji wanaocheza eneo lake kupata nafasi.

6. FATUMA BUSHIRI (JKT QUEENS)

Kwa sasa yupo benchi akitoa maelekezo kwa baadhi ya makinda wanaocheza eneo lake kutokana na umri kumtupa mkono.

Kiungo huyo ambaye pia aliwahi kuichezea Yanga Princess, lakini kutokana na ugumu wa nafasi ya kucheza amejikuta akipata nafasi chache za kuanza kikosini.

Bado mkongwe huyo anacheza na amekutana na staa wa zamani wa Sayari, Queens Esta Chabruma ambaye amestaafu kucheza na kugeukia ukocha wa JKT Queens.

7. AMINA BILAL (JKT QUEENS)

Huyu ni kiungo matata ambaye ukimuona anavyocheza unalifurahia boli safi analolipiga.

Kwa nyakati tofauti alipita katika timu mbalimbali za ushindani ikiwamo Simba, Yanga na JKT Queens na kote alifanya vizuri na kuwa tishio.

Safari yake ya soka ilianzia msimu wa 2012/13 kwenye mashindano ya Umissetta akitokea Kanda ya Mashariki na ndipo Kanali Idd Kipingu alipomuona na kumpeleka katika shule yake ya kukuza vipaji ya Lord Baden Powell iliyopo Bagamoyo.

Akiwa anaendelea na masomo kidato cha pili, Amina aliichezea Uzuri Queens na baadaye akatimkia Evergreen Queens na kupata nafasi ya kuitumikia timu za taifa umri wa chini ya U-20.

Nyota huyo ana miaka 11 kwenye soka na bado anaubonda pale kwa wanajeshi wa kike ambao msimu uliopita walikuwa mabingwa wa WPL.

Mastaa wengine kwenye ligi hiyo ambao ni wakongwe ni pamoja na Eto Mlenzi (JKT Queens) ambaye alicheza na kina Mwalala na Zuwena Aziz anayeichezea (Ceasiaa Queens) ya Iringa.

Chanzo: Mwanaspoti