Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wengine kusimamishwa Simba SC

Simba Wengineeeee Wengine kusimamishwa Simba SC

Sat, 23 Dec 2023 Chanzo: Dar24

Kuna uwezekano mkubwa wa wachezaji wengine wa Simba SC kukumbana na adhabu kama waliyokutana nayo viungo Clatous Chama na Nassoro Kapama kutoka kwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Abdelhak Benchikha kama wasipobadilika.

Juzi Alhamis (Desemba 21) Simba SC ilitoa taarifa ya kuwasimamisha wachezaji wake Chama na Kapama kwa kile kilichotajwa utovu wa nidhamu kabla ya kupelekwa katika Kamati ya Nidhamu ya timu hiyo.

Nyota hao wote wameondolewa kambini wakati timu hiyo, ikijiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya KMC FC utakaopigwa baadae leo Jumamosi (Desemba 23) kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Mmoja wa mabosi kutoka ndani ya Benchi la Ufundi la timu hiyo, amesema kuwa Kocha Benchikha ameamua kusimamia nidhamu ya kila mchezaji huku akiwaweka wote levo moja kwa lengo la kuondoka ustaa katika timu.

Bosi huyo amesema kuwa katika kikao chake hivi karibuni kocha aliwaambia wachezaji wote wako sawa, hakuna staa, mgeni wala mkongwe na aliyekuwa juu ya mwenzake, huku akimtaka kila mmoja awe na nidhamu.

Amesema kuwa ameanza kuwasimamisha Chama na Kapama ili wawe mfano kwa wachezaji wengine, lengo ni kutengeneza nidhamu ya timu, kamwe hatasita kumsimamisha au kumsitishia mkataba mchezaji yeyote mwenye nidhamu mbaya bila kuangalia ukubwa wa mkataba wake.

Ameongeza kuwa mshambuliaji wa timu hiyo, Mkongomani Jean Baleke alinusurika kusimamishwa na kocha huyo, wakati wa maandalizi ya mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar ambaye alichelewa kufika mazoezini, akamtimua mazoezini na baadae akamrejesha kwa kumpa onyo zito.

“Benchikha anataka kutengeneza nidhamu ya timu hivi sasa katika timu, ameona kuweka pembeni masihara na urafiki kwa wale wachezaji ambao nidhamu yao ni ndogo, hivyo upo uwezekano mkubwa wa wachezaji wengine wakubwa kusimamishwa kama wasipobadilika.

“Kabla ya Chama na Kapama kusimamishwa, Baleke alitimuliwa mazoezini na kuzuiwa kufanya pamoja na wenzake wakati timu ikiwa katika maandalizi ya mwisho ya mchezo wa ligi dhidi ya Kagera Sugar, lakini baadae alirejeshwa kwa sharti la kutorudia tena utovu huo wa nidhamu.

“Benchikha ameondoa madaraja ya wachezaji wapo wale wanaojiona wakongwe, mastaa, wazawa na wageni hivyo kocha hataki kuona hilo likifanyika katika timu yake.

“Hivyo kocha amesisitiza kuwa anataka kuona kila mchezaji akipambania namba ya kucheza katika kikosi cha kwa kumshawishi kuonyesha kiwango bora, lakini siyo kwa kuangalia ukubwa wa jina la mchezaji, mzawa, ukongwe, mgeni au mzawa huku akiahidi nafasi kwa kila mchezaji,” kimesema chanzo hicho.

Mtendaji wa timu hiyo, Imani Kajula hivi karibuni alizungumzia hilo la nidhamu kwa kusema kuwa: “Uongozi tumepanga kutomuingilia kocha katika maamuzi yoyote katika timu, badala yake tutamuunga mkono katika jambo, kwani tunaamini uwezo wa kufundisha timu.”

Chanzo: Dar24