Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wenga aipa Tanzania mchongo wa Afcon

Wengerrr (15).jpeg Wenga aipa Tanzania mchongo wa Afcon

Sun, 22 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kocha wa zamani wa Arsenal, Arsene Wenger amesema atashirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuhakikisha timu ya taifa 'Taifa Stars' inakuwa na ushiriki mzuri kwenye fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 ambazo zitafanyika hapa nchini kwa kushirikiana na Kenya na Uganda.

Wenger ambaye ni mkuu wa idara ya maendeleo ya mpira wa miguu ya Shirikisho la soka duniani (FIFA) alisema ili Tanzania iwe na timu imara, inapaswa kufanyia kazi hatua tatu muhimu ambazo ni kutafuta vipaji, kuendeleza vipaji na kuvipa nafasi na idara yake itasaidia katika utimizaji wa mpango huo.

"Kuna vipaji vingi duniani lakini mwishoni havipati vipaji vya kutimiza ndoto zao. Nawaahidi siku moja nitakuja hapa. Kuna kazi kubwa ya kufanya lakini sisi kwa pamoja na shirikisho la mpira wa miguu Tanzania na FIFA, tutaleta kocha hapa kuelimisha watoto na tutaleta kocha wa kuelimisha makocha.

"Kwa sababu moja kutafuta vipaji, pili kufundisha na kinachofuata ni kukipa nafasi kuonyesha kipaji. Na nyakati katika hatua ya kwanza tunahitaji msaada katika kutafuta kipaji. Tutaleta timu hapa yenye uwezo wa kuorodhesha vipaji na baadaye kwa pamoja na makocha kufundisha vipaji.

"Tuna miaka minne, mitano mbele yetu na kama tutafanya vizuri, nina uhakika tutakuwa na wachezaji wazuri kila eneo," alisema Wenger.

Wenger alitoa kauli hiyo jana wakati alipotembelea mradi wa ujezi wa kituo cha ufundi cha TFF uliopo Kigamboni, Dar es Salaam ambao uliwekwa jiwe la msingi na Rais wa FIFA, Gianni Infantino na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Patrice Motsepe.

Katika hatua nyingine, mmoja wa nyota wa Simba ambaye hakupenda jina lake kutajwa hadharani amefichua walichoambiwa na kocha Arsene Wenger pindi alipowatembelea katika vyumba vya kubadilishia nguo baada ya mechi yao dhidi ya Al Ahly juzi.

"Wenger alitueleza kuwa kipindi cha kwanza tulicheza chini ya kiwango hatukufuata vizuri maelekezo ya mwalimu, lakini akatupongeza kwa jinsi tulivyocheza kipindi cha pili, alisema kama tungecheza vile vipindi vyote tulikuwa na nafasi ya kupata ushindi kwenye mechi hii.

"Hakuongea maneno mengi, lakini kila alipokuwa anazungumza wale alioongozana naye walikuwa wakitikisa kichwa kuonyesha kuwa wanakubaliana naye," alisema mchezaji huyo.

Wakati huohuo Taifa Stars itafungua dimba la Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2023 zitakazofanyika Ivory Coast mwakani kwa kucheza na Morocco, Januari 17 katika Uwanja wa Laurent Pokou, San Pedro.

Kwa mujibu wa ratiba ya mashindano hayo iliyotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) juzi jioni, mchezo wa pili wa Taifa Stars utakuwa ni Januari 21 ambapo itaumana na Zambia na itahitimisha hatua ya makundi kwa kukabiliana na DR Congo, Januari 24.

Kocha msaidizi wa Taifa Stars, Hemed Morocco alisema kuwa hawapati hofu kwa ratiba hiyo na wanachokifikiria ni kujiandaa vizuri ili waandike historia katika AFCON mwakani.

"Makundi yakishapangwa maana yake utacheza dhidi ya kila timu ambayo ipo kwenye kundi jambo ambalo hata sisi tulishajiandaa nalo. Kinachohitajika ni maandalizi ya uhakika ambayo yatatuwezesha kupata matokeo mazuri katika mechi zote tatu za kundi ili tuingie katika hatua inayofuata.

"Timu zote kwenye kundi letu ni nzuri na ngumu hivyo tungeanza na yoyote yule bado mechi ingebakia kuwa ngumu," alisema Morocco.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live