By Waandishi WetuMore by this Author INJINIAAA...soma hiyooooo....hao ni mashabiki wa Simba walipokuwa wakishangilia ushindi wa 13 wa chama lao katika Ligi Kuu Bara na kupunguza pengo la pointi dhidi ya watani wao, Yanga wanaoongoza msimamo.
Bao pekee la fundi wa mpira, Bernard Morrison ‘Mzee wa Kuwakera’ katika dakika ya 22 liliifanya Simba ifikishe pointi 42, ikiwa ni nne pungufu na ilizonazo Yanga yenye michezo 20 na kuipa timu yao ushindi wa tatu mfululizo ugenini dhidi ya Biashara United katika mechi za ligi.
Simba bado ina michezo miwili mkononi ambapo kama itashinda yote itawarejesha kileleni baada ya muda mrefu tangu watani wao walipowapora kiti katikati ya duru la kwanza.
Katika mchezo wa jana uliopigwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, mjini Musoma, Kocha Didier Gomes alimuanzisha kikosini Gadiel Michael ambaye hata hivyo alimpumzisha kipindi cha pili na kumuingiza Mohammed Hussein Tshabalala.
Kikosi cha Simba kililianza dakika 45 kilionekana kuwa na mabadiliko makubwa tofauti na kile kilichocheza mchezo uliopita wa Ligi ya Mabingwa Afrika ugenini, Kinshasa na kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya AS Vita kwenye maeneo mawili.
Gomes mbali na kumuanzisha Gadiel, pia eneo la ushambuliaji alianza na Meddie Kagere badala ya Chris Mugalu na kiungo alimchezesha Said Ndemla badala ya Larry Bwalya, huku pembeni Perfect Chikwende na Morrison wakisimama badala ya Clatous Chama na Luis Miquissone.