WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Watanzania wanatamani kuona timu zao za Taifa za michezo mbalimbali zinafanya vizuri katika mashindano ya Kimataifa.
Amesema kuwa uwezekano wa timu ya Taifa ya soka ya Tanzania (Taifa Stars) kufanya vizuri katika michuano ya kufuzu kombe la Dunia itakayofanyika nchini Qatar 2022 ni mkubwa kutokana na matokeo mazuri ambayo imeyapata katika michezo ya minne ya awali.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatatu, Novemba Mosi, 2021) wakati wa kikao na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa , uongozi wa TFF pamoja na wadau wa mpira wa miguu kilichofanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Mlimwa jijini Dodoma.
“Tukifanikiwa kushinda mechi hizo mbili zilizobaki kati ya timu ya Taifa na Congo pamoja na mechi ya timu ya Taifa na Madagascar ambayo itachezwa ugenini, itatupa matumaini ya kushiriki katika michuano ya kombe la dunia, hivyo Serikali inaamini ushirikiano kati ya wadau na Uongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ni muhimu katika kufanikisha lengo hilo,” amesema Majaliwa.
Akiongea na wadau hao, Majaliwa amesema michuano ya kombe la dunia ni fursa kwa wachezaji wetu kwani itawasaidia kutambulika katika mataifa mbalimbali duniani hivyo kupata nafasi ya kuhitajika na vilabu vikubwa duniani.
“Tukishinda mechi hizi mbili pamoja na kuvuka hatua ya mtoano itakayotuwezesha kushiriki kombe la dunia tutakuwa tumewasaidia wachezaji wetu kupanua soko lao kimataifa kwa kuwa wataonekana na hata tutakapoita timu ya Taifa tutakuwa tunaita wachezaji wengi wa kimataifa tofauti na sasa ambao ni watatu tu nao ni Mbwana Samatta, Simon Msuva na Novatus Dismas," amesema.
Waziri Mkuu amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema anatamani kuona timu ya Taifa soka ya wanaume (Taifa Stars) inafanya vizuri kama ilivyo kwa timu ya Taifa ya soka wanawake ambayo hivi karibuni ilichukuwa ubingwa kwenye mashindano ya kombe la COSAFA 2021 yaliyofanyika nchini Afrika Kusini.